May 29, 2013

MBOZI SHWARII

 Naibu waziri wa Elimu Kassim Majaliwa akisalimiana na Mbunge wa Mbozi Godfrey Zambi siku alipofika wilayani Mbozi, wilaya ya Mbozi imo kwenye mchakato wa kupata mkoa wake
 Mkuu wa wilaya ya Mbozi Dr Kadeghe akimtambulisha naibu waziri kwa kaimu Mkurugenzi Mbozi Dr Charles Mkombachepa
 Walimu wakimsikiliza naibu waziri

walimu wakifuatilia majadiliano

May 28, 2013

MGAWANYO WA MKOA WA MBEYA WAJIELEKEZA KUVUTIA KIMAKABILA


Na Mwandishi wa Indaba Africa,

Mnyukano wa ugawaji wa mkoa wa Mbeya umeendelea kujenga sura ya uasilia wa waliopo kwenye madaraka kutokana na wanasiasa kuvutia maeneo walikotoka bila kujali vigezo vya msingi ikiwemo idadi ya watu.

Kulingana na vikao vinavyoendelea, wilaya ya Rungwe tayari imeshajitengenezea mazingira mazuri ya kupigiwa debe kuwa mkoa kwa kile kinachobainishwa kuwa madiwani wengi katika mkoa wa Mbeya asili yao ni wilaya ya Rungwe

Dhana ya “kumitu kukhaja ” inaonekana wazi wakati huu  kwenye mchakato wa kutoa mapendekezo ya wapi na maeneo yapi yaunganishwe kuunda mkoa wa mpya  baada ya Mh Rais Kikwete kutamka wazi na kubariki mchakato huo wakati wa maadhimisho ya siku ya wafanyakazi mei mosi.

Mfano wa kujipigia debe unaonyesha kuwa Mwenyekiti wa halmashauri ya Mbarali Keneth Ndingo ni mkazi wa Rungwe hivyo maamuzi ya baraza la madiwani la Mbarali yanaonekana kuwa na msukumo wa nyumbani, ambapo wamependekeza makao makuu yawe Rungwe

Maajabu ya musa yanajitokeza katika ugawaji unaopendekezwa ambapo inaelezwa kuwa Mbarali wanapendekeza halmashauri za Busokelo, Rungwe, Kyela, Ileje na Mbozi ziunde mkoa mpya wakati kijiografia havina uwiano kati ya Mbozi na Rungwe.

Kulingana na takwimu za sense ya mwaka2012, wilaya ya Mbozi kabla ya kugawanywa kupata Momba ilikuwa na wakazi 740,719 idadi ambayo ni sawa na idadi za wakazi wa wilaya za Kyela, Rungwe na Ileje ambazo kwa pamoja ni wakazi 685,098 hivyo kuwepo kwa pengo la 55621 zaidi kwa upande wa Mbozi

Kulingana na jiografia ya mkoa wa Mbeya, Mkoa ambao kwa sasa ungeweza kuundwa kwa kuunganisha wilaya za  Ileje, Mbozi, Momba  na sehemu ya wilaya ya Chunya  (jimbo la Songwe) ambalo limejitenga na eneo la Lupa kwa umbali wake.

Kwa takwimu hizo hizo mkoa wa  huo ungeweza kuwa na idadi ya wakazi 1,201,327 ambao  ni asilimia 44.4 ya takwimu za sasa za wakazi wa mkoa wa Mbeya wanaofikia 2,707,410.

Ingawa jitihada za kujipanga zimeanza kwa upande wa wilaya za Rungwe, Mbarali na Kyela kwa kufanya ushawishi wa mbinu,ukweli unabakia kuwa wilaya ya Mbozi peke yake inavigezo vyote vya kupata mkoa mpya kuanzia idadi ya watu, eneo la utawala,makazi, uwezo wa raslimali za ndani kujiendesha na fulsa za kiuchumi zilizopo na zinazoweza kupatikana.  

May 27, 2013

KIMONDO YAANZA RAUNDI YA PILI YA MABINGWA WA MIKOA KWA KUTOA KICHAPO CHA BEBERU JIZI!




Timu ya Kimondo SC ya wilayani Mbozi katika mkoa wa Mbeya imeendelea kutakata katika raundi ya pili ya ligi ya Mabingwa wa Mikoa baadaya kuisukutua bila dawa timu ya Mji ya Njombe bao 1-0 juzi katika mchezo uliofanyika uwanja wa sabasaba  mjini Njombe

Katika mchezo huo ambao tangu kuanza kwake ulikuwa ukionyesha jitihada za wazi za kuhitajika mbeleko kwa timu ya wenyeji, hali iliendelea kuwa tete kadiri dakika zilivyokuwa zikienda mbele kutokana na mbinu za hapa na pale za mwamuzi kushindwa kupenya ili kuleta madhara kwa upande wa Kimondo.

Kimondo licha ya majaribio kadhaa vipyenga vya kuotea vilionekana kuharibu ladha ya mchezo kiasi cha mashabiki wa Njombe kushindwa uzalendo na kuamua kushabikia timu ya Kimondo ambayo ilionekana kutandaza soka lenye ladha mithiri ya asali ya Ilomba na Idiwili.

Katika dakika za mkiani, baada ya majaribio kadhaa ya kuingia eneo la hatari na kupigiwa vipyenga vya kuotea, ndipo staili ya “mpime huko huko mbali” ilipoanza na haikuchukua muda mrefu kwani gonga kama nne kutoka kwenye lango la Kimondo zikielekezwa kwenye lango la timu ya Mji Njombe ziliwezesha shuti la umbali wa mita 52.56  kuleta sherehe kwa upande wa Kimondo baada ya kumpima kipa wa Mji Njombe na katika maeneo hatarishi na kusababisha timu ipumulie mashine mbele ya mashabiki wake uwanja wa nyumbani.

Ushindi huo ulipakatwa kama mwali na timu ya Kimondo kwani jitihada zote za kujaribu kuondoa aibu uwanja wa nyumbani kwa Mji Njombe hali iliendelea kuwa ngumu na hadi dakika kumi zilizoongezwa na mwamzi kumalizika bado Njombe walionekana kuzidiwa pumzi.


Nyongeza ya dakika ilionekana dhahiri shairi kutaka kusababisha kilio cha bao la pili hivyo mwamzi akajikuta anapuliza filimbi huku akiangalia huku na kule kuhofia uongozi wa mkoa uliokuwa upo uwanjani na kushuhudia timu yao ikitoka imetota huku wageni kutoka Mpakani wakizungumza Kinyiha,Kiwemba,Kinyaki na  kinyamwanga huku maneno “Nyinza sana” tununu fijo”, natemwa, na tukuvifyondomola” yakisikika kwa furaha


Mchezo wa marudiano baina ya  Kimondo SC ya Mbeya  na Mji Njombe unatarajiwa kufanyika katika uwanja wa sokoine mjini Mbeya Jumapili Juni 2 mwaka huu.

Chachandu ya ligi hiyo inashamihilishwa na namna timu zilivyojipanga kuhakikisha ushindi kwa kufanya usajiri wa kusugulia meno kwa tupa!!

 Meneja wa timu ya Kimondo ambaye pia ni mwenyekiti wa halmashauri ya Mbozi Erick  Minga anafafanua kuwa mchezo wa marudiano itakuwa ni kuanika unga wa mhogo kiangazi, kwani timu yake imejaindaa vilivyo.

 Timu zingine zinazoshiriki ligi hiyo na mikoa yake kwenye mabano ni pamoja na Friends Rangers ya Dar es Salaam, African Sports ya Tanga, Abajalo ya Dar es Salaam,Kariakoo ya Lindi, Machava FC ya Kilimanjaro ,Mpwapwa Stars ya Dodoma,Stand United FC ya Shinyanga na Magic Pressure ya Singida


Nyingine ni Polisi Jamii ya Bunda mkoani Mara, Biharamulo FC ya Kagera, Saigon FC ya Kigoma na Katavi Warriors ya Katavi.

Timu zitakazofuzu kucheza raundi ya tatu zitacheza mechi za kwanza kati ya Juni 8 na 9 mwaka huu wakati mechi za marudiano zitakuwa kati ya Juni 15 na 16 mwaka huu.

 

 

May 26, 2013

ZAMBI AFAGILIA JK KUVUNJA BODI YA KAHAWA


 

Na Danny Tweve Mbozi,

 Mbunge wa Mbozi Godfrey Zambi amesifu hatua ya Mheshimiwa rais Jakaya Kikwete  kusikiliza hoja aliyoiibua bungeni na hatimaye kuivunja bodi ya Kahawa aliyowahi kuilalamikia bungeni kuwa  imeundwa kwa upendeleo wa ukanda.

Akizungumza jana kwenye mkutano wa hadhara ulioambatana na ugawaji  wa madawati kwa shule ya msingi ya Ichenjezya katika mamlaka ya mji wa Vwawa, Mbunge huyo amesema ingawa hoja hiyo ilionekana kubezwa hatimaye imezaaa mabadiliko aliyoyafanya mheshimiwa rais kwa kuteua bodi mpya ambayo sasa itaongozwa na Dr Juma  Ngasongwa

Alisema mwaka jana alimwandikia waziri wa Kilimo Christopher Chiza  kupinga uteuzi uliofanywa na waziri wa Kilimo wakati huo Profesa Jumanne Maghembe ambapo Dr Eve Hawa Sinare iliteuliwa kuwa mwenyekiti wa bodi hiyo huku wajumbe watano wa kamati hiyo wakitokea  mkoa mmoja.

Katika barua yake ya Juni 4, 2012, Mh  Zambi pamoja na kumwandikia waziri wa kilimo pia alinakili barua hiyo kwa Mh Rais Kikwete, Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro  akielezea kukiukwa kwa sheria na utungwaji wa kanuni za zao la kahawa bila kuzingatia taratibu.

Anasema bodi hiyo ya awali ilikuwa na wajumbe ambao wengine walikuwa na migongano ya kimaslahi na wengine kutojulikana makundi wanayowakilisha tofauti na bodi ya sasa ambapo imehusisha wajumbe kutoka maeneo yote ambayo Kahawa inalimwa.

Anaeleza kuwa anafurahi kusimama mbele ya wananchi kuwa rais amesikiliza kilio hicho na kuivunja bodi hiyo pamoja na kuiteua bodi nyingine ambayo sasa inahusisha maeneo yanayozalisha zao hilo.

“ ninafuraha kuwaelezeni leo hii kuwa tarehe 30 na 31 mwezi huu wadau wa kahawa watakutana mkoani Morogoro kuzungumzia maendeleo ya zao la Kahawa mkiwa na bodi mpya ambayo ina uwakilishi niliokuwa naupigania na kuusimamia” alieleza Mh Zambi.

Amesema katika suala la kutetea maslahi ya wananchi wake yupo tayari kuitwa vyovyote ilimradi anasimamia ukweli, na kwamba katika hilo kuna wakati alilaumiwa na kuonekana akitofautiana na waziri aliyeteuliwa na chama chake, na kwamba alifanya hivyo kwakuwa anatambua kuwa alikuwa akiwakilisha maslahi ya wapiga kura wake na wazalishaji wa kahawa nchini kote.

Amesema ni vyema pia wananchi wake wakatafakari kwa makini kauli iliyokuwa ikisisitizwa na Mbunge wa awali wa jimbo hilo marehemu Halinga kuwa wananchi wa wilaya hiyo wanapaswa kuwasomesha watoto wao ili kuepuka kuwa chakula cha wasomi.

Alisema neno hilo si zuri sana kulizungumzia mbele ya jamii lakini ni ukweli kwamba pasipo kusomesha watoto wao, wataendelea kuwa watumwa wa jamii iliyosoma ambayo ndiyo yenye fulsa za kufanya maamuzi huku wao wakiwa watekelezaji tu

Akiwa kwenye mkutano huo uliofanyika nje ya uwanja wa shule  ya msingi ya Ichenjezya Mh Zambi alitoa msaada wa madawati 100 yenye thamani ya shilingi Milion sita kwa shule ya Ichenjezya na kufikisha idadi ya madawati 180 ambayo amekwisha yatoa kwa shule hiyo kwa ushirikiano na mamlaka ya bomba la mafuta TAZAMA.
MWISHO

May 25, 2013

MEELA ASIKIKITISHWA NA HALI YA WANAHABARI MBEYA, ATIA MKONO KUANZISHA SACCOS


MKUU wa wilaya ya Rungwe Bw. Chripin Meela amesema, changamoto zinazokabili sekta ya habari na  vyombo vya habari  kwa ujumla ni matokeo ya umuhimu wa taaluma hiyo katika ukuaji wa demokrasia nchini
Akizungumza kwenye mkutano wa uchaguzi wa klabu ya wandishi wa habari mkoa  Mbeya unaoendelea ukumbi wa Royal Tughimbe, Mkuu wa wilaya ya Rungwe Chrispin Meela amesema, wananchi wana matumaini makubwa na vyombo vya habari na pale kipapota doa la utendaji ni muhimu kujirekebisha kabla ya kutengeza picha mbaya mbele ya jamii wanayoihudumia
Amesema hali iliyojitokeza hivi karibuni kwenye klabu hiyo inahitaji kuweka misingi imara ya kiutendaji  na kwamba jitihada za kufanya uchaguzi  wakati huu ni hatua muhimu za kuimarisha mfumo wa kujiwajibisha kama taasisi ya taaluma.
Amesema ikiwa viongozi wa dini na vyombo vya habari vitajihusisha na ubadhirifu na wizi ni dalili kuwa hakutakuwa na mwingine wa kukemea jamii itakayokuwa huru na yenye kukemea vita dhidi ya rushwa
Bwana Meela amesema inashangaza kuona hata vyombo vya habari vinaingia kwenye ufisadi na akaohoji  ninani atakayehoji ufisadi serikali na kwingineko kama nanyi mnaingia kwenye mitego hiyo hiyo?
Katika hatua nyingine amependekeza  Vyombo vya habari kujenga utamaduni wa kujihusisha na ufuatiliaji wa maendeleo vijijini na kwa kufanya hivyo kutawezesha wananchi kuwasilisha changamoto zinazowakabili kwa watunga sera.
Amesema katika kufikia hilo  ni vyema pia Viongozi wa serikali ngazi za chini kuondoa uoga  katika kufanya kazi na vyombo vya habrari na kwa kufanya hivyo kutasadia kusukuma mbele jitihada za maendeleo
Katika hatua nyingine Bwana Meela amechangia kiasi cha shilingi 400,000 kwaajili ya uanzishaji wa chama cha kuweka na kukopa cha wanahabari  SACCOS  ili kuwezesha kuwapa fulsa wana habari  kujisimamia kiuchumi  na kupunguza changamoto za kimaisha zinazowakabili
Katika kufanikisha hilo wanachama wa Mbeya Press club walijitokeza kuchangishana wenyewe ambapo wamefanikiwa kukusanya mtaji wa papo kwa papo kiasi cha shilingi 1,400,000/=
Aidha ameshauri klabu ya wandishi wa habari kuwa na ofisi yake na hvyo kwa kuomba kiwanja kwenye mamlaka za majiji itasaidia kuwapa nguvu katika kusimamia haki zao wakiwa na uhuru wa kuwekeza kwenye majengo yao.

 

MEI MOSI UWANJA WA SOKOINE, KUMEKUCHA

 Uwanja wa Sokoine ambao unakumbukwa kwa hotuba aliyoitoa mwalimu Nyerere Mwaka 1995 ambayo imeendelea kuwa ujumbe wa kila siku kwenye vyombo vya habari hasa kwenye harakati za kusaka madaraka ya kuingia Ikulu
 Mpiga picha wa TBC akiwa tayari kwa kazi ya kuleta  picha na hatmaye kuunganishwa moja kwa moja kwenye matangazo yanayoendelea kupitia kituo hicho katika uwanja wa sokoine mjini Mbeya
 Wandishi wa habari wakiendelea kufanya kazi zao uwanjani hapo.

 Bendi ya Sikinde wakitumbuiza kwenye uwanja wa sokoine wakati wa maadhimisho kabla mhe Rais hajawasili uwanjani hapo kupokea maandamano
 Mkuu wa mkoa wa IRINGA Christine Ishengoma akiwasili uwanjani hapo na kusalimiana na timu ya mapokezi
 Hapa Mkombe Zanda wa Star Tv akizungumza na mpigapicha katika safu ya mawasiliano Ikulu Fred Maro katika uwanja wa sokoine
 aisee Mbeya yetu Mnatisha, picha zenu nimekuwa nikizifuatilia " ndivyo anavyoeleza Fred Maro wakati wakisalimiana na Joseph Mwaisango mwandishi wa Mbeya yetu
 Mwandishi mkuu wa Mbeya yetu Joseph Mwaisango akisalimiana na mdau Fred Maro kwenye uwanja wa sokoine
 Ngoma ya kabila la wasafwa ikiburudisha wakazi watu waliofurika uwanja wa sokoine kwenye maadhimisho ya siku ya wafanyakazi
Timu ya Uhuru Publication ikiwa uwanjani hapo kunadi bidhaa wanazozizalisha ambapo gazeti lao leo lilipata soko uwanjani hapo

Na Timu ya INDABA BLOG

Maadhimisho ya siku ya wafanyakazi mkoani Mbeya yameambana na ukaguzi mkali katika milango ya kuingilia ambapo mabango na zana zote zimekuwa kichekiwa kwa vyombo

Hatua hiyo inalenga kuimarisha usalama uwanjani hapo kwa kuzingatia kuwa ni jukumu muhimu katika kuwezesha nchi kutulia

Imeelezwa kuwa mabango yenye ujumbe wa kejeli yamekuwa yakiishia mikononi mwa maofisa wa idara za usalama na kufanyika screening ya ujumbe unaoingizwa uwanjani
Kwa ujumla uwanja wa sokoine umefurika huku kila kona kukiwa na makundi ya watu wanaotaka kuingia na kushuhudia kupanda ama kimya kwa mishahara na mambo mengine ya wafanyanyakzi ambao kwa namna moja ama nyingine wanaathiri maisha ya kila siku ya ndugu zao

hadi wakati huu saa 5.15 bado kupo shwari na mandamano yanasubiri kiongozi wa nchi Mh Rais Jakaya Kikwete aingie ndipo waendelee na shughuli za kupita mbele ya jukwaa na kukaguliwa