Na Danny Tweve –Mbozi
Naibu waziri wa Kilimo
na Ushirika Mh Godfrey Zambi hatimaye ameungana na watafiti kuunga mkono matumizi
ya Mbolea ya Minjingu na kuwataka wananchi kuwa tayari kushiriki mashamba
darasa yanayokusudiwa kufanywa kwenye maeneo ambayo mbole hiyo imekuwa
ikilalamikiwa.
Akizungumza na
watendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbozi kabla ya kuanza ziara ya kikazi ya
siku tatu wilayani humo , Mh Zambi amesema hatua hiyo haitokani na uteuzi wake
kuhofia kutofautiana na serikali yake bali ni kutokana na matokeo ya utafiti ya
kitaalamu yaliyowasilishwa na taasisi zinazoaminika
Mh Zambi amesema licha ya kutafsiriwa kuwa ni
mpinzani wa mbolea ya Minjingu, bado jukumu lake kubwa kama mtetezi wa wananchi
ilikuwa ni kuisukuma serikali kusikiliza malalamiko ya wananchi na kwamba hatua
ya sasa ya kuanzisha mashamba darasa italeta suluhu ya tatizo hilo.
Alisema ni dhahiri
mbolea hiyo bado inalalamikiwa, lakini njia bora ni kutoa elimu kwa wananchi namna
ya kuitumia na kwamba mkakati wa majaribio zaidi kupitia mashamba darasa kwenye
maeneo ambayo mbolea hiyo imeonyesha udhaifu utaweza kutoa matokeo bora badala
ya malalamiko yasiyo na takwimu za kitaalamu.
Amesema juzi akiwa
ziarani kutembelea kiwanda cha minjingu pia amekutana na malalamiko hayo hayo
kwenye kijiji ambako kiwanda kimejengwa na kwamba malalamiko pia yamethibitishwa pia kupokelewa na uongozi wa
kiwanda juu ya matumizi ya mbolea ya
minjingu mazao.
Hata hivyo amesema
walichokubaliana na uongozi wa kiwanda hicho
kuanzisha mashamba darasa ya kutosha katika kila eneo linalolalamikiwa
kuwepo utendaji usioridhisha wa mbolea hiyo.
Ameeleza kuwa awali
uongozi wa kiwanda cha minjingu
walimweleza wazi kuwa walikuwa
na hofu juu yake baada ya kuteuliwa kwenye wizara ina uhusiano wa moja kwa moja
na bidhaa yao, huku akiwa ni miongoni mwa wabunge waliokuwa misumari bungeni
kwa kuwa na misimamo mikali kuhusiana na mbolea ya minjingu
Mh Zambi amesema tayari
wameshapokea matokeo ya utafiti kutoka chuo Kikuu cha Kilimo SUA mbao
wamethibitisha utendaji mzuri wa mbolea ya minjingu ikilinganishwa na Mbolea ya
DAP inayopigiwa debe na wananchi wa wilaya ya Mbozi .
Amesema njia pekee ya
kuwashawishi wananchi ni kuanzisha mashamba darasa mengi kadiri iwezekanavyo ili kuthibitisha
matumizi sahihi ya Mbolea hiyo na kwamba
changamoto za mbolea hiyo zitatatuliwa kupitia maonyesho hayo na kwamba
ushirikiano baina ya serikali kuu,watafiti, kiwanda cha minjingu na halmashauri
za wilaya
Kuhusiana na utaratibu
wa utoaji wa pembejeo kwa njia ya ruzuku, Naibu waziri amesema kwa msimu ujao
serikali haitatoa tena ruzuku kwa utaratibu wa vocha na badala yake pembejeo
zitapitia vyama vya ushirika ambavyo sasa vitasimamiwa na sheria mpya ya mwaka
2013.
Amesema katika kipindi
cha miaka mitatu mfululizo ya utoaji ruzuku ya Mbolea kwa njia ya vocha jumla
ya vocha zenye thamani ya shilingi Bilion 70 zimebainika kuibiwa ama kutumiwa
kinyume na taratibu na kwamba kamati ya bunge ya Kilimo imemwagiza Mkaguzi na
mdhibiti wa hesabu za serikali kufanya ukaguzi ili hatua zichukuliwe
Amesema ni vyema
halmashauri za wilaya kuanza kuwaandaa wananchi katika mfumo mpya wa kupata
pembejeo ambao hautahusisha vocha na akawataka maafisa ushirika kujenga uwezo
kwa vyama vya ushirika ili kuviandaa katika utoaji huduma hiyo.