Adverts

Jan 5, 2016

Msimu wa upandaji miti Mkoa wa Njombe waanza

Wakazi wa mkoa wa Njombe wameanza msimu mpya wa upandaji miti ambapo shughuli hizo sasa zimepewa umuhimu mkubwa tofauti na hapo nyuma ambapo programu mbalimbali za uhifadhi mazingira zilitekelezwa na kuhamasisha wananchi bila mwitikio mzuri.
Katika vijiji vya Kigala, Mlengu, Ikuwo,Matenga na Nkondo,wananchi wamejiwekezea akiba zao kwenye upandaji miti ambapo sasa angalau kila kaya ina angalau ekari moja ya miti hali inayoashiria kuwa miaka michache ijayo kutakuwa na mabadiliko makubwa.
Tishio lililopo kwa sasa ni kuwepo kwa taarifa kuwa Pori la akiba la Mpanga -Kipengere linakusudiwa kupanuliwa hivyo kuvifuta baadhi ya vijiji, hali hii inapunguza ari ya wananchi kupanda miti kwa kasi katika maeneo yao licha ya kupokea vyema mpango wa upandaji miti.Mzee Mafundihano Nzilani pichani anaeleza kuwa amejijengea utamaduni wa kupanda miche 100 kila mwaka na kwamba tayari keshaanza kufaidi matunda ya miti aliyoipanda miaka 15 iliyopita.