2.0 CHUO KIKUU KISHIRIKI CHA RUAHA, IRINGA (RUCO)
Zaidi ya wanafunzi 600 wa mwaka wa kwanza wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Ruaha waligoma Jumanne Januari 25, 2011 wakiwa na madai ya kutolipwa mikopo ya chakula na malazi kwa robo ya pili ya mwaka.
Hapo awali, mikopo ya chakula na malazi ya siku sitini (60) kwa robo mwaka ya kwanza kwa wanafunzi hao yalifanyika mapema tarehe 21 Oktoba, 2010 kabla ya chuo hicho kufunguliwa mnamo tarehe 8 Novemba, 2010. Kama ilivyo kawaida, orodha ya wanafunzi inayoonyesha namba zao za usajili pamoja na namba zao za akaunti za benki ilitakiwa kuwasilishwa Bodi ndani ya siku 30 (yaani kabla ya tarehe 8 Desemba, 2010) ili Bodi ipate muda wa kutosha wa kuandaa malipo ya robo mwaka ya pili ambayo yangetakiwa kufanyika kupitia akaunti zao za benki kabla ya tarehe 8 Januari, 2011.
Lakini orodha hiyo iliwasilishwa Bodi tarehe 30 Desemba, 2010 yaani uchelewesho wa zaidi wiki tatu. Baada ya kupokea taarifa hiyo, Bodi iliweza kushughulikia malipo hayo kwa haraka sana na tarehe 6 Januari, 2011, malipo ya jumla ya sh. 315, 000, 000.00 kwa ajili ya wanafunzi wapatao 1,050 yalitayarishwa, kupitia hundi Na. 972928. Hata hivyo, ilibidi hundi hiyo ipelekwe Benki tarehe 21 Januari, 2011 baada ya kupokea kiasi cha sh. 15 bilioni kutoka Hazina tarehe 20 Januari, 2011, uchelewesho ambao ulitokana na ukweli kwamba Bodi haikuwa na fedha za kutosha katika akaunti yake, kabla ya tarehe hiyo.
Katika matukio haya, Bodi inapenda kuwakumbusha Wadau wote juu ya umuhimu wa kuzingatia taratibu za utoaji mikopo hususan muda uliopangwa wa kupokea maombi ya mikopo na muda uliowekwa wa taarifa muhimu kuwasilishwa Bodi ili kurahisisha mchakato wa utoaji mikopo.
Aidha, Bodi inasisitiza kwamba mikopo haitatolewa kwa wanafunzi ambao hawajapitishwa na TCU na NACTE kwenda kusoma elimu ya juu. Hivyo, wanafunzi wengi wa kundi hilo wawasiliane na vyuo vyao ili taarifa zao zipelekwe TCU na vyuo vyao ili TCU waweze kuhakiki taarifa zao na kisha kuzileta Bodi, badala ya kuipigia kelele Bodi.
Pia, kama ambavyo Bodi imewahi kutoa tamko juu ya umuhimu wa kutafuta ukweli juu ya mwenendo wa utoaji mikopo, wadau wote wanahimizwa kuwasiliana na Bodi mara kwa mara ili kupata taarifa sahihi badala ya kukimbilia kuilaumu Bodi bila sababu za msingi.
IMETOLEWA NA:
MKURUGENZI MTENDAJI
BODI YA MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU