Adverts

Jan 20, 2011

COASTER YACHOMWA MOTO BAADA YA KUGONGA-MBOZI

BARABARA YA TUNDUMA MBEYA YAFUNGWA KWA SAA TISA,
WANANCHI WADAI MATUTA!
Na Danny Tweve -Mbozi.
Wananchi  wenye hasira wameliteketeza kwa moto  basi aina ya Toyota Costa linalofanya safari zake kati ya Tunduma na Mbeya baada ya basi hilo kumgonga mwenda kwa miguu.
Tukio hilo limetokea leo jioni katika kijiji cha Ihanda kilometa 15 kutoka makao makuu ya wilaya ya Mbozi ambapo kutokana na kifo hicho wananchi waliliteketeza kwa moto basi hilo lenye namba za usajiri T 196 AUC  na kufunga barabara ya Tunduma Mbeya kwa muda wa saa 9 kuanzia saa 12 jioni hadi saa 7.11 Usiku.
Taarifa kutoka kijijini hapo zimemtaja aliyegongwa hadi kufa kuwa ni Charles Sikanyika mkazi wa kijiji cha Sumbalwela ambaye aligongwa wakati akivuka.

Imeelezwa kuwa coaster hiyo mali ya Bwana Tusubile Mwampamba ijulikanayo kama Mbombo Line Express ilikuwa ikiendeshwa na dereva Dankel Mwamasika ambaye alipojaribu kutoroka na gari hilo, lilizima ghafla umbali wa mita 100 kutoka eneo alipomgonga mwenda kwa miguu na kulazimika kupasua kioo cha mbele kujiokoa kwa mbio.

Kufuatia hali hiyo abiria waliokuwemo pamoja na Kondakta wake walijichanganya na wananchi ili wasipigwe ambapo mali na mizigo iliyokuwa kwenye basi hilo iliteketezwa kwa moto na baadaye wakaharibu pia basi la Hood lililotoka Dar es salaam kwenda Tunduma ambalo limevunjwa na kuchomolewa vioo upande mmoja na kuvunjwa taa za nyuma.

Jitihada za Mkuu wa polisi kujaribu kuwatuliza wananchi hao ziligonga mwamba tangu saa 1 jioni hadi saa 5 usiku killipowasili kikosi cha Polisi kutoka Mbeya kikiongozwa na staff Officer na Mkuu wa Usalama barabarani bwana Mgeni maarufu kama  Obama ambaye licha ya kufanya ushawishi hali ilikuwa ngumu kwa vijana hao ambao walikuwa wamepanga mawe na vyumba barabarani.

Katika maelezo yao wananchi hao wanadai kuwa Mkuu wa wilaya ya Mbozi aliwaahidi kuwa matuta yangewekwa eneo hilo tangu mwezi wa Decemba lakini, ahadi hiyo imeendelea kuwa hadithi huku wakiendelea kupoteza maisha.

Wakaendelea kudai kuzuiwa kwa magari kunalenga kufikisha salama zao kwa Wwaziri wa Miundombinu /Barabara  Dr Magufuli na kwamba walitarajia kuwa maiti hiyo ingeondolewa wakati matuta yakiwekwa.

Hata hivyo baada ya majadiliano ambayo yalionyesha kutokuwa na matunda askari mmoja aliyefahamika kwa jina la Justin aliamua kuongoza kikosi kwa kuwataka wananchi kupisha vinginevyo matumizi ya nguvu yangechukua nafasi, hatua hiyo ilienda sambamba na kuondoa vizuizi vilivyokuwa barabarani ambapo aliyendelea kuongoza magari hadi eneo la ajali na kuzingira eneo hilo na hatimaye kupakiza maiti hiyo majira ya saa 7.11 usiku.

Katika hali ya kujihami Mkuu wa wilaya ambaye alikuwa akitafutwa na wananchi hao kwa kile walichodai aliwadanganya kwa kuwaahidi matuta, alilazmika kuvaa kama mwarabu kichwani ili kupoteza sura yake hatua ambayo wananchi walishindwa kumtambua.

Yeye na mkuu wa kituo cha Polisi VWAWA afande Malima walivaa vitambaa kichwani kama wasomali ama waarabu hali ambayo iliwabadilisha kabisa na kutotambulika kirahisi hasa baada ya kusikia kama mkuu wa wilaya yupo hapa asionekane tutamfanyia".
mwisho