Kwenye sehemu iliyopita tuliona jinsi gani baadhi ya wanaume wanavyoutumia mfumo dume wao vibaya. Wengi wanatafsiri vibaya, wadhifa wa mwanaume kuwa kichwa cha familia, na tafsiri hiyo hupotoshwa na kutumiwa sivyo ndivyo. Wengine hudiriki kuvuka mipaka na kutoa adhabu za kipigo, au ukandamizaji wa namna fulani, hili bado lipo katika jamii zeti. Pia tumeona jinsi gani ndoa nyingi zinaingia kwenye migogoro, kwa vyanzo mbali mbali, hasa sababu ya kukosa mtoto, tunasahau kuwa yote ni mjaliwa ya Mungu. Mambo kama haya yakitokea inatakiwa tutulie, tuangalia nini sababu, kwani inawezekana ikawa ni tatizo dogo la kiafya au kumbe tatizo lipo kwa mwanaume, lakini mara nyingi mlaumiwa wa kwanza ni mwanamke….
Pia tumeona katika kisa hiki kuwa jamii zetu ndoa bado ni za kulazimisha, wazazi wanakutana na wazazi wenza wanakubalina kuozesha mtoto wao, binti hajui nini kimeendelea, mwisho wa siku anaambiwa unaolewa, akiuliza na nani, anaambiwa mzee Fulani au mtoto wa mzee Fulani, yeye hajawahi kukutana naye kimaongezi. Hili linakuja kuleta migogoro baadaye kwani hakuna pendo, hakuna mawasiliano ya mwanzo ya kuridhiana. Hii bado ipo kwenye jamii zetu kuwa wanawake wanaolewa kama bidhaa
Hebu tuendelee na kisa chetu hiki , tukielekea moja kwa moja kwenye hospitali ya mkoa, ambapo mama wa rafiki yangu alipelekewa huko. Hii ni sehemu ya saba ya kisa chatu cha Nani kama mama .
***
Dakitari bingwa, aliwaita madakitari wenzake, na kuwaelekza nini cha kufanya. Hili lilikuwa zoezi lakumuokoa mtoto au mama wa mtoto kwa jinsi hali ilivyoonekana. Tukumbuke mama huyu alifikishwa hapo hajitambui, hata kauli hana. Damu nyingi zilimvuja, licha ya vidonda vya miba iliyomchoma usoni na sehemu nyingine za mwili. Majeraha yalikuwa makubwa, kiasi kwamba, uso ulihumuka. Na kwasababu alikaa kwenye maji bila ya matibabu vidonda vilishaingiwa na virusi.
‘Hapa tuna mitihani, kwani mama anahitaji matibabu ya vidonda, lakini hilo sio muhimu kwasasa inabidi tulitulize kwa dawa maalumu, ila cha muhimu ni huyo mtoto aliyepo tumboni, inaonyesha dhahiri kuwa tusipofanya juhudi za haraka, tutawakosa wote wakiwa hai, kwahiyo tukimbilie hili kubwa la kumuokoa mtoto. Akasema yule dakitari kuwaelekeza wenzake.
Ndani ya lile jopo kulikuwepo na dakiatri kijana, huyu alikuwa kaja pale kupata uzoefu baada ya kupata masomo yake huko nje. Aliporudii na ujuzi wake,hakutaka kusubiri likizo imuishie nyumbani tu, alimua kujitolea kwenye hospitali hii, pamoja na kupata ujuzi wa kazi yake, na nia yake kubwa ilikuwa nadhiri yake ya kuwasaidia akina mama ambao huishia kufa, kwasababu ya kuvuja damu au matatizo ya uzazi. Yeye aliahidi kuwa katika kazi yake hiyo, inapofikia hatua ya kuchagua nani apone, yeye, atachagua wote wapone.
‘Dakitari kijana , jana tulikuwa tukiongelea swala kama hili, ukasema una hamu sana ya kuokea mama na mtoto , pale inapofikia hatua ya kuchagua nani apone, je katika hali kama hii unaweza ukasemaje, …najua wewe sio mzungumzaji ni mtendaji, naombe ushike usukani wa kuokoa maisha ya huyu mama au mtoto….
Labda kabla sijaenda mbali niwakumbushe kuwa katika nchi yetu hii kuna hospitali za rufaa zilizojaliwa kuwa na madakitari wazuri, na moja ya hospitali hii ni hii huyu mama alipofikia. Ubora wake ulitokana na kutembelewa na madakitari mbali, mbali waliokuwa wakija kutoa huduma, za kujitolea, pia na wanafunzi huja kupata elimu kwa vitendo. Kipindi hicho kulikuwa na hata madakitari wazungu waliofika kufanya tafiti mbalimbali pamoja na kuwafunza madakitari waliomaliza Muhimbili ambao walishapangiwa kazi kwenye hizo hospitali. Na huyu dakitari kijana akawa miongoni mwa waliokuwepo humo, licha ya kuwa yeye hakumalizia Muhimbili.
Huyu dakitari kijana licha ya kuwa dakitari mwanafunzi lakini ubora wake ulikuwa wa hali ya juu. Huko alipokuwa akisomea, walimuhitaji sana abakie kwenye nchi hiyo, lakini alikumbuka ahadi yake ya kutaka kuisaida jamii yake, na alishuhudia akina mama wengi wakikosa huduma hiyo alipokuwa mdoho, akaahidi kuwa , akipata bahati ya kusoma atajitolea kwa moyo wake kuwasaidia akina mama. Na ndoto yake ikatimia, na leo anapewa jukumu la kumuokoa mama, ambaye hali yake ilikuwa mbaya sana.
Sasa tuelekee chumba cha upasuaji. Chumba hiki kilitengwa pembeni kidogo ya jengo na kilijengwa kwa utalaamu wa hali ya juu, kilikuwa na sehemu nne, na zote zingeweza kutumika kufanyia kazi zote za upasuaji. Moja ya chumba hiki cha upasuaji ndipo alipokuwepo mama tunayemzungumzia, chumba kilikuwa kimya na sauti iliyosikika na mashine ya kupozea hali ya hewa. Usingeamini kuwa ndani yake walikuwepo madakitari wakijaribu kuyaokoa maisha ya huyu mama au mwanae aliyepo tumboni.
Dakitari kijana akifanya kazi yake chini ya dakitari bingwa wa akina mama, alikuwa kayaweka mawazo yake kwa kile anachokifanya, na siri kubwa ilikuwa kichwani mwake. Akiwa anaongozwa kuwa akiweza amuokoe mtoto, kwani mama hali yake haitamaniki. Humu ndani kilichokuwa kikongea ni mikono, na jopo la wataalamu wa upasuajililikuwa likijitahidi kila mmoja kwa nafasi yake. Dakitari kijana alijitahidi kufanya kazi yake kwa makini, huku akimuomba mungu aweze kufanikiwa, kwani ile ilikuwa moja ya mitihani yake, lakini licha kuwa ni moja ya mitihani yake, nia yake kubwa ni kutimiza ahadi yake ya siku nyingi!.
Baada ya kazi ngumu ya kumuokoa mtoto , kama agizo lilivyokuwa, madakitari walitoka chumba cha upasuaji kwa muda kujadili jambo wakiwa wamekata tamaa, kwani hali ya mtoto mwenyewe ilikuwa mbaya, na mawazo ya mama mtu yalikuwa hayasemwi kwani walijua yeye ni marehemu tu, kutokana na hali waliyoiona toka awali. Kinyume na madakitari wenzake, dakitari kijana alikuwa na mawazo tofauti alikuwa na yake kichwani ambayo hakupenda kuwaambia wenzake kwa muda huo. Alimuomba mola alichokifanya kizae matumaini.
Walipotoka nje yule dakitari kijana akaiinua mikono juu na kumshukuru mungu, na tendo hili liliwashangaza madakitari wenzake iweje amshukuru mungu wakati zoezi lakumuokoa mmoja kati ya mtoto au mama yake lilinaonekana kama limeshindikana.
`Halijashindikana, na hamtaamini kitakachotokea baadaye, nyie subirini ile dawa ifanye kazi yake' alisema na kurudi chumba cha upasuaji peke yake. Alitaka kuhakikisha kuwa alichokuwa kakifanya kimeenda kama alivyotaka.
Baada ya nusu saa miujiza ya mungu akaanza kufanya kazi yake, mtoto akaonyesha dalili ya kuishi ingawaje mama mtu bado alikuwa katika hali mbaya. Dakitari kijana na dakitari bingwa walitumia ujuzi wao wote kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa, na kwa muda ule dakitari kijana alikuwa peke yake ndani ya kile chumba , alikuja kuhakikisha kuwa alichofanya kimezaa matunda! Alifikiria moyoni kuwa kama alichofanya hakikufanikiwa basi, ina maana alichojifunza kina walakini, lakini hakukata tama, akajipa moyo kuwa itawezekana tu!
Akamsogelea yule mama pale alipolala na kutafakari lile alilolifanya kwa yule mama, na alichojifunza masomoni na kugundua kuwa kafanikiwa, kama kafanikiwa kosa lipo wapi, mbona haoni dalili njema, je aliyafuata maelekezo kama ilivyotakiwa, akakiri kuwa alifanya vyema zaidi. Basi akasema moyoni, iliyobakia sasa ni kumuomba mungu, kwani hata ufanyaje kama mungu hakupenda iwe haitakuwa. Hii ilikuwa moja ya imani zake…Alikumbuka nyaraka zake alizokuwa keshazitayarisha kuhusina na ugunduzi wake, akamuomba mungu, zoezi hili lifanikiwe ili liweze kukamilisha ugunduzi wake huo.
Lakini huyu mama alikutwa na masahibu gani, akawaza yule dakitari kijana, alimwangalia yule mama alivyoharibika uso, na akilini mwake akasema, labda alikutana na simba, akawa amemburuza kwenye miba., Vinginevyo, kwanini uso uraruliwe kiasi hicho. Kila mara dakitari yule alikuwa akikumbuka yale maneno ya yule mama alipokuwa akiweweseka kabla kazi haijaanza ya kumfanyia hiyo operesheni, mama huyu alisema `muokoeni mwanangu, lakini mimi niachane nife, na nikifa nileleni mwanangu' alijiuliza sana kwanini yule mama alisisitiza sana kuwa mwanae alelewe na hospitali na wala sio jamaa zake. Alisema moyoni kuwa huenda ni ile hali aliyokuja nayo yule mama, au huenda kuna ugomvi huko alikotoka, au aligombana na mumewe,lakini haiyamkini kwa binadamu kuwa na unyama kiasi kile, kumpiga mama mjamzito na kumtoboatoboa usoni kiasi kwamba sura ilikuwa haitamanaiki.
Baada ya siku tatu mtoto akawa amechangamka na kuondokana kabisa na dalili zozote mbaya, lakini mama mtu bado alikuwa hajazindukana, na hali hii iliwatia wasiwasi madakitari wakijua kuwa hawataweza kufanya lolote kumsaidia yule mama kuzindukana. Ilibidi waitane tena kushauriana ili kama imeshindikana wayaondoe yale mashine ya kumsadia mgonjwa kupumua,
Lakini dakitari kijana akakataa, akasema ana imani mgonjwa atazindukana muda mchache ujao.
‘Wewe bado kijana una munkari na kazi bado, na hili ni jambo jema kabisa, endeela na moyo huo, sisi kazi hizi tuna uzoefu nazo, hali kama hii…, sijui, labda tuache tuone ulichojifunza, na kukifanyia kazi leo, huenda ukaleta jambo jema,…’ akasema yule dakitari bingwa, akiwa na nia ya kumpa yule kijana uzoefu wake wote, kwani kijana huyo alionekana kuipenda kazi yake vyema. Alisema kichwani, huyu yupo kama mimi nilipokuwa makamo yake, nilipenda sana kusaidia watu…kama nchi yetu ingetujali sana,huenda mimi ningekuwa mbali sana, lakini…
Walipotoka ndani ya kikao hicho wakajikuta wakihangaika na mgonjwa mwingine aliyeletwa akiwa naye na hali mbaya. Na alihitaji upasuaji ili kuokoa maisha yake, kwahiyo jopo zima likaelekea kumhudumia huyo mgonjwa mpya. Wote wakawa katika kazi ya kuhakikisha wanamsaidia ili apone. Ilibidi wamsahau mgonjwa wa zamani kwa muda, nah ii ilikuwa kawaida kwani mgonjwa wa awali alikuwa anasubiriwa azindukane ndipo matibabu mengine yaendelee. Walichofanya ni kumuachia nesi majukumu ya kuangalia mambo mengine yanakwenda sawa, huku wakimwambia kama kuna badiliko lolote atoe taarifa haraka iwezekanavyo.
Kazi ya kumfanyia operesheni mgonjwa mpya iliwatinga kiasi kwambao mpaka wanamaliza kumhudumia huyo mgonjwa mpya ikawa imeshafika jioni, na kwa vile walishaacha majukumu kwa nesi hawakuingiwa na wasiwasi wa mmojawapo kwenda kuangalia nini kinaendelea, na baada ya kuhakikisha wamemaliza kazi kubwa ya mgonjwa mpya, yule dakitari bingwa akamtuma mwenzake aende kumwangalia mgonjwa wao kuwa kazinduka au anaendeleaje.
Mara wakiwa wanavuavua vizuizi vya mkononi, mlango ukafunguliwa ghafula hata kabla yule dakitari aliyetumwa hajaondoka,na aliyeingia mle ndani ni nesi aliyekabidhiwa majukumu ya kumwangalia yule mama aliyefanyiwa upasuaji mwanzaoni. Aliingia huku kashikilia vifaa vya kumuongezea mgonjwa maji, na usoni alionyesha woga na kutahayari. Wenzake walipomuona katika ile hali walijua kuna jambo kubwa limetokea kwa yule mama,….
***Jamani mbona muda unakwenda haraka hivyo, naona tushie hapa, huku tukiomba miujiza itokee labda mama atapona, ...mtoto keshapona, Je ataishii bila mama?. Tuendelee kuwepo!
Ni mimi: emu-three
http://miram3.blogspot.com/feeds/posts/default?alt=rss
"