Adverts

Jan 31, 2011

Nani kama mama-9

Nani kama mama-9: "
Alijikuta anashikwa na kigugumizi pale alipofungua mlango na mcho yake yakiwa yametua kitanda alichokuwa amelala yule mgonjwa. Macho yalimtoka pima, na kushindwa kusema, hata ile chupa aliyoshika mkononi ikamponyoka na kudondoka chini, lakini kwa bahati nzuri ilitua kwenye sehemu laini na haikupasuka. Alijikuta akitetemeka kwa woga, na kutamani akimbie, lakini angekimbilia wapi,…akatamani apige yowe, lakini ingesaidia nini…akashikwa na bumbuazi kwa dakika moja, huku akishindwa afanyeje… Je huyo nesi aliona nini? Karibuni tuendelee na kisa chetu, kwa sehemu inayofuata: ******************* ************************ Madakitari walipoona nesi kaingia na badala ya kusema neno, ameduwaa, wakajua kuna tatizo kubwa sana, hivyo wote walikurupuka kutoka nje kuelekea kule alipolazwa yule mama hata kabla hawajamuuliza yule nesi ni nini kimetokea,… Walimpita yule nesi pale aliposimama, kama vile hayupo, mbio kuelekea chumba hicho cha wagonjwa maalumu, kilikuwa chumba cha pili yake kutoka hapo, lakini wenyewe waliona kama chumba hicho kipo mbali ajabu, walipofika mlangoni walishangaa, kwani chumba hicho muda wote kinakuwa kimefungwa, walikuta mlango upo wazi, wakahisi huenda yule nesi kasahau kuufunga ule mlango kwa kuchanganyikiwa. Mbio, mbio wakisukumana kuingia mlangoni, kila mmoja akitaka atangulie yeye kuingia. Waliingia ndani huku kilammoja akiwa na lake kichwani, huyu alikuwa akifikiria mgonjwa, kazindukana na anahitaji huduma ya haraka, wengine walidiriki kuona labda mgonjwa keshakata roho, lakini dakitari kijana, alikuwa na lake kichwani, kuwa mgonjwa kazindukana, na alihitaji huduma ya ziada, kwahiyo yeye alikuwa kapanga akiingia tu, cha kwanza ni kuangalia ile mashine inayoonyesha mwendo wa mapigo ya moyo….! Huku nesi aliachwa peke yake, akiwa anatafakari jinsi gani ya kuitetea, alikuwa kabakia mwenyewe kwenye chumba cha mapumziko wa hawo madakitari, akiwaza, nini afanye, kwani watu wametoka mbio hata kabla ya kusikia kauli yake, akajisema moyoni, ngoja wenyewe wafike wajionee kama nilivyojionea mimi…, najua baada hapo nitatakiwa kujibu maswali mengi, na labda nitaonekana mzembe, lakini watakuwa wamenionea …akasubiri kidogo , halafu akasema, ngoja niwafuate kwani nikiwaachia mpaka warudi hapa watakuja na hasira kubwa na nitashindwa kujitetea…akakurupuka na yeye mbio kuelekea huko walikoelekea madakitari, akiigiza walivyotoka mbio, huku kichwani akisema, `unafanya utani eeh, kibarua kitaota majani, mungu wangu niepushie mbali na hilo…. ‘Nataka mtoto wangu….’ Wakati hayo yanaendela huko hospitalini, katika kitongoji kimoja, nje ya mji, watu walikuwa wakishangaa umati wa watoto, ambao walikuwa wakiwa kama wapo kwenye maandamano, huku wanaimba kwa pamoja..`nataka mtoto wangu..’ na sauti ndogo ya ambayo ilisikikakwa shida ikiwa ni sauti ya mwanamke mtu mzima iliitikia `nataka mtoto wangu…’ Watu wakawa wanashangaa na kila mmoja akawa na hamu ya kumsikia huyo anayeimbisha huo wimbo wa aina yake ni nani, na kitu gani kimewafanya watoto wavutike naye…huku wazazi wakiwa na wasiwasi na watoto wao wakiogopa asije akawadhuru, au isije ikawa mbinu ya kuwaiba watoto wao, kwani visa vingi kama hivyo vilishatokea na watoto wakatoweka kiajabu. Na kwa minajili hiyo watu wakawa nawo wanasogelea kile kikundi cha watoto, na watoto wengine wakawa wanaongezeka kuwafuta hawo watoto wanaoongozana nyuma ya anayeonekana ni mama, kwani waliomuona walisema ni mama, sio mtoto kama watoto wengine, ingawaje mama huyo kajifunika sehemu kubwa ya kichwa chake, na amevaa gauni kubwa, ambalo sio la kawaida. Ni mwanamke mgani kabisa kwao… ‘Nataka mtoto wangu, nataka mtoto wangu…’ sauti ikawa inaongezeka kila muda. Na mama mmoja aliyekuwa kajipumzisha ndani ya nyumba yake, alikuwa kajilaza kitandani baada ya shughuli za ndani, na pilika zahapa na pale, aliona ajipumzishe huku akimsubiri mume wake, ambaye huja kula chakula mchana nyumbani, akawa kajisikia kuchoka, na kausingizi kakawa kamempitia. Akiwa katika usingizi wa malepemalepe, mara akawa kama anaota, watu wanatafuta watoto, na wanapita kila nyumba kuulizia mtoto. Na cha ajabu muulizaji akawa anauliza kama vile anajua kuwa mtoto yupo hapo anasema kwa sauti kali…`nataka mtoto wangu..’ huyu mama akiwa ndotoni, akamjibu, mbona mimi sina mtoto, kwani hata mimi nataka mtoto pia… Mara akakurupuka toka usingizini, na kusikia kelele nje, akainuka na kuangalia dirishani baada ya kusikia kelele hizo. Alipofunua pazia la dirisha na kutizama nje, aliwaona wale watoto wakiwa wanaimba kwa sauti, na kila wakiimba kuna sauti ya mwanamke inakuwa kama inaitikia au ndiyo inayoimbisha kwa maneno ambayo aliyasikia kwenye ndoto…`nataka mtoto wangu…..! Yule mama akashangaa, hii ndoto ina maana gani, na kwanini iwe sawa na tukio hilo linaloendelea huko nje,…! Akapanguso uso na kuwaangalia wale watoto, wanavyoimba kwa furaha, nakuwaza mbali ajabu, aliwaza kuwa kama naye angejaliwa watoto, au mtoto, angekuwa naye anamtizama mwanae akiwa miongoni mwa hilo kundi. Akajikuta machozi ya kimlengalenga, akawaza na kutikisa kichwa huku anasema moyoni, hivi mimi nina kasoro gani, mbona sipati mtoto, mwaka wa kumi sasa, tangu tuoane na mume wangu, lakini hakuna cha mimba au mtoto, angalau ningepata mimba, itoke, nione nina tatizo lakini au la, hakuna hata dalili…Mmmmh mungu wangu, nisije nikawa…mmmh, hapana, kizazi ninacho hii nina uhakaika, sasa tatizo ni nini…mume naye… Akawaangalia wale watoto, huku machoni kukiwa na ukungu wa machozi, yaliyoanza kububujika, …akainua kichwa juu kumuomba mungu kuwa amjuze tatizo lake ni nini, kuwa yeye hatazaa tena, au kuna tatizo gani zaidi. Alikumbuka jinsi gani akimwambia mume wake asivyotka kusikiliza kilio chake kuwa waende hospitli wakapime , ili wajue tatizo nini, lakini yeye hakubali. Huishia kwa maneno mengi, utafikiri yeye ni mtaalamu wa vizazi…na jana tu alisema; ‘Kwani wewe una tatizo gani, unaumwa, unajisikia vibaya, mtoto ni kudura ya mungu, kama tutapata tutashukuru mungu, kama hatukupata, basi ndivyo tulivyopangiwa, mimi sioni tatizo lipo wapi…nakuona siku hizi unawaza saaana, mbona mwanzoni nilipokuambia swala hili ukalipuuza, sasa unajifanya kujisikia uchungu…achilia mbali mawazo hayo…mtoto tutapata tu…’ hayo maneno aliyasema mume wake jana, kabla hawajalala. Ni kweli maneno hayo, kama ingelikuwa yeye na mume wake tu asingelijali, kwani kupata mtoto ni kudura ya mungu, lakini kila wanapokuja mawifi zake inakuwa ndio gumzo, kwanini wifi hupimi, kwanini wifi hampati watoto…kwanini, kwanini…’mazungumzo kama hayo, yanakuwa hayampi raha, ingawaje kwa ukweli, mawifi zake anawapenda kama wanavyompenda yeye, hajaona chuki yoyote kwao, lakini kibinadamu ,lazima watakuwa wanamjadili huko nyumbani kwao vinginevyo. Kwani, eti, nani asiyependa kuona ndugu yao, au mtoto wao ana watoto…raha ya mzazi ni mtoto, mtoto ni tunda na faraja ndani ya familia…oh! Namuonea sana Huruma mama yake mume wangu, najihisi kama mimi ndiyo yeye,halafu natamani mjukuu toka kwa mtoto wangu lakini hapatikani…mmh, mama…namkumbuka mama yangu pia…mama..nani kama mama, sijui huko ulipo na wewe unanikumbuka…’ alishika tama huku anazidi kuwaangalia wale watoto wanaoendelea kuimba! ‘Namtaka mtoto wangu…’ sauti hiyo ilikuwa inazidi kusikia maeneo karibu na nyumbani yao, na kuiona kama kero, na yeye akajikuta akiimba, `na mimi nataka mtoto wangu..’ akawatizama wale watoto wakiwa wanaruka kwa furaha huku yule mama aliyekuwa mbele yao akionekena kuchoka, sijui kwa kutembea sana au ana matatizo ya akili. Akawaza huenda naye ana matatizo kama yake,…huenda kwa kuwaza sana kama yeye amipitikia kuwa kichaa, ndio maana anaimba `kutaka mtoto wake’. Akajaribu kumtizama yule mama , lakini watoto walikuwa wakimzonga kama kumchokoza, ili aimbe hayo maneno, na yule mama akawa anawafukuza,na akifanya hivyo, inakuwa kama mchezo kwa watoto wale, wanamkimbia halafu wanarudi tena, na kila wakirudi yule mama anakuwa kama anawaambia, au kuwaimbia hayo maneno `nataka mtoto wangu…’ na wao huitikia `nataka mtoto wangu…’ Yule mama aliokota fimbo akawa anawatishia kuwachapa wale watoto , na watoto wakakimbia nabaadaye wanamrudia , wakimfikia yule mama anaimba `nataka mtoto wangu’ na watoto nawo wanaitikia `nataka matoto wangu..’ ikawa hivyo hivyo, na bahati mbaya wakawa hawaondoki karibu na nyumba ya huyu mama, kiasi kwamba na yeye aliona ni kero. ‘Watoto wazuri, lakini fuji zao…aah, mimi nawafukuza…’ Akaona atoke nje awafukuze, na wakati anafungua mlango simu ikaita. Aliikimbilia kuisikiliza … ‘Halloh, nani mwenzangu…’ aliuliza kabla hajaangalia nani aliyepiga, aliposikia sauti akajua ni sauti ya mdogo wake, alikuwa akiongea kwa wasiwasi na anaonyesha kama analia. ‘Vipi kuna tatizo gani, mdogo wangu..’ akaingiwa na wasiwasi, kuwa kuna jambo baya limetokea huko anakofanyia kazi mdogo wake. Mdogo wake anafanya kazi hospitali ya mkoa, amehamishiwa karibuni tu, na mara nyingi wanamtegemea sana yeye wakikwama, na hivi karibuni tu kaamua kutafuta chumba huko maeneo karibu na anapofanyia kazi, na kuondoka kwake imekuwa pigo, kwani asilimia kubwa walikuwa wakimtegemea yeye pale wanapokwama, inagwaje sasa hivi hali imekuwa shwari kwani mume wake keshapata kazi, kwahiyo ile hali ya kumuombaomba vijiseni imepungua. Katika familia yao wamezaliwa wawili tu yeye na mdogo wake huyo, kwahiyo wanapendana sana, na kipindi wanaishi pamoja hapo, watu walidiriki kuwaita mapacha, ingawaje yeye alishaanza kuonekana mzee, na ukichanganya na mawazo, sasa hivi anaonakana mama … ‘Unasema kuna tatizo kubwa huko hospitalini, imekuwaje, sema basi mbona unaanza kulia, mimi unanitisha…’ kabala hajasikia vizuri simu ikakatika. Alipoangalia akakuta simu yake haina chaji, akakumbuka kuwa alisahau kuichaji usiku, kwasababu umeme ulikatika, Akakimbilia kuichaji, lakini akakuta umeme hakuna. ‘Jamani sasa nitafanyaje, na umeme hakuna, …’ akajikuta anaujiuliza ‘Nataka mtoto wangu…’ sauti ilikuwa ianzidi kusikika karibu na malngo wake ‘Hata mimi nataka mtoto wangu..onokeni hapo nje, mnanipigia kele, akafoka huku anajaribu kuiwasha ile simu bila mafanikio. Akatoka nje ilia aone kama atapata mtu wa kumuomba simu, lakini alichoona ni wale watoto wakiwa wanazidi kujaa eneo karibu na nyumba yake. ‘Hodi hodi hapa…’ akasikia sauti ya mume wake ikiita kwa nje, naye akakurupuka mbio, akijua sasa muokozi kaja, na akamkimbilia na kumpkoea mfuko uliokuwa umajaa vitu, na akaukimbiza ndani, halafu akarudi haraka kumuwahi mumewe kabla hajakaa chini, na kama kawaida yake akamvua koti,kwani mume wake anapenda sana kuvaa koti, tai utafikiri ni mkurugenzi Fulani.. Almvua mumewe koti, halafu akawa anamkanda kanda mabegani, moyoni akisema, kama nina bahati ni mimi , kumpata mume ninayempenda, na naye ananipenda sana, ila tatizo ni mtoto…lakini sijui yeye ana mawazo gani, akamshika mumewe mkono na kumvuta kwenye kocho ili akae, na akaelekea kabati la vyombo, akatoa gilasi na kuijaza maji ya kunywa, akampa mumewe, … Mumewe alimwangalia kwa makini, huku akiwaza mengi, moyoni alijisifia kuwa kweli kamapata mke mwema, na anampenda sana, hakutaka kabisa kumuuzi, kwani licha yeye kuwa chaguo lake, lakini hawa wazazi na familia yao wanampenda sana mke wak huyu, ila sasa kuna tatizo ambalo hata yeye limeanza kumkera, kuhusu swala la kupata mtoto. Akajikuna kichwa na kuwaza, halafu akanywa yale maji aliyopewa na mkewe. ‘Hivi kumbe swala la kupata mtoto ni swala nyeti sana kiasi hiki…’ akasema kimoyomoyo, alisema hivyo kwani wakati ameongozana na rafiki yake, walikuwa wakilijadili hilo swala, rafiki yake alikuwa akimshawishi aone mke wa pili ili ajaribi bahati huenda akapata mtoto. Alipinga kabisa swala hili, akiwamwambia kuwa yeye na mkewe wanapendana sana na huenda akioa mke wa pili, itakuwa chanzo cha kukosana. ‘Sasa wewe umeoa ili iweje, make tu mapaka uzee, na nani ataiendeleza familia yako, na mali yako..’ akamuuliza rafiki yake ‘Mimi nina mali gani…aah, kama mungu atapenda iwe hivyo, siwezi kukalifisha nafsi..unakumbuka mtume Ibrahim, alikaa miaka mingapi bila mtoto…nyie watoto mnaona ndio kila kitu..hapana, mimi mapenzi ndio muhimu sana, ilimradi tunapendana na mke wangu, sioni sababu ya kukosana naye kwasababu ya watoto…kama tutapata tutapata tu…’ akasema kwa hasira, kwani haya mazunguzmo yamekuwa kero, kila akikutana na jamaa yake yoyote ndio gumzo. ‘Au wewe una tatizo, kwanini huendi kwa wataalamu wakalitizama..’akasema rafiki yake ‘Tatizo…tatizo gani…’ akauliza kwa kushangaa, na aliyosikia kwa rafiki yake yakawa yamemtinga sana akilini, na hata alipofika kwake akawa anawaza sana hayo maneno… ‘Huenda kweli kuna tatizo, mimi au mke wangu,na tutajuaje kama hatutakwenda haospitalini…’ akajisema na kumwangalai mke wake ambaye alikuwa anatizama nje kwa kupitia dirishani... ‘Nataka mtoto wangu…’ sauti ilikuwa ikififia, kwani wale watoto walipomuona baba mwenye nyumba anakuja wakaona sasa watachapwa, na baba mwenye nyumba hiyo hana mzaha na watoto wakorofi, na yule mama aliyekuwa akisumbuliwa na wale watoto akawa kachoka na kujilaza kiamabzani mwa nyumba hiyo. ‘Vipi mke wangu kuna jipya, nakuona umeanza mawazo yako, au sio…’ akasema huku anainuka pale alipokaa na kwenda kusimama pembeni mwa mke wake, na kupitisha mikono yake kiuonini mwa mkewe, akamsogeza karibu yake, huku anatizama nje anapotizama mkewe. Kwa mbele ya barabara, walisimama watoto wawili, wakiwa wanaangalia kuelekea nyumba yao, na sijui walikuwa wakitizama nini. Baba huyu hakujali nini wanatizama, na akamgeukia mkewe, alipomwangalia vyema, akaona michirizi ya machozi ambayo ilishakauka. Akaingiwa na mashaka, kuwa kama wasipotafuta ufumbuzi wa tatizo lao, mkewe anaweza akazurika, kwa mawazo. ‘Mke wangu, nimewaza sana…’ ‘Ndio mume wangu, nilikuwa nasubiri utulie, kuna simu kapiga mdogo wangu toka hospitalini, anasema kuna tatizo, lakini simu ilikatika siunajua tena tatizola umeme, simu sikukumbuka kuichaji, usiku umeme uliporudi, naomba umpigie tusikia kuna tatizo gani…’ akaema mkewe. Na mume ksuikia hivyo, akakimbilia koti lake lilipotundikwa na kuanza kuitafuta simu ya shanejji yake. Shemeji yake wameishi naye tangu akiwa mtoto, wakamsomesha na akapata kazi akiwa mikononi mwake, kwahiyo anamjali sana kama mtoto au mdogo wake, kuliko hiyo `shemeji’ akawa anasilikza simu ikiita upande wa pili. ‘Halloh, shemeji kuna tatizo gani huko..’ akauliza kabla hawajasalimiana. Akasikiliza upande wa pili ukiongea, na huku anamtizama mkewe ambaye alikuwa kakaribia ili ajaribu kusikia nini kinaongewa upande wa pili. ‘Nataka mtoto wangu..’ sauti ya watoto ikasikika nje, na baba mweny nyumba akatizama nje, akagundua kuwa ni wale watoto wawili wamkuja hapo nje ya nyumba yake wakiimba hayo maneno, na akawa na hamu kuangalia nini kimewavuta hadi kuja eneo la nyumba yake, huku akiwa bado anasikiliza simu. ‘Sasa sikiliza shemeji, usiwe na shaka, kwa vile wanataka kukaa kikao kulijadili hilo, wewe subiri kwanza, usijiweke roho juu, kwani huna hatia, kwa maelezo yako, hilo lingetokea kwa yoyote…sidhani kwamba wao watachukua hatua kama hiyo ya kukufukuza kazi…’ maneno hayo ya mwisho yalimshitua sana mke wake. Ina maana kuna tatizo la kufikia hadi kumfukuza kazi mdogo wake, …haiwezekani, kwanini wamfukuze kazi…’ ‘Namtaka mtoto wangu…’ sauti ikawa inazidi huko nje, na baba mwenye nyumba akaona ni kero akatizama nje kuwatimua hawo watoto na macho yake yakafuatilia wanapotizama wale watoto, ni pembeni mwa nyumba yake, akajaribu kutizama, lakini ilikuwa vigumu kuangalia nini wanakitizama, akawa na hamu sana kuona watoto wanamtizama nani, kabla hajamwambia nini kimetokea huko mjini akaona amalizane na hilo tatizo la nje, kwani halitawapa nafasi ya kuongea na mkewe. ‘Nyie watoto hebu muwe na adabu kidogo..’ akasema huku anaufungua mlango, na kabla hajasema zaidi macho yake yakatua pembeni mwa nyumba na akajikuta akishituka na kubakia kukodoa macho ….ajabu kabisa…..! Kabla hajatizama vyema, yule mwanamama akashituka toka usingizini na kujifunika haraka, halafu akainuka na kupotelea mitaa ya pili. Yula baba akawa anawaza mengi, kuwa huyu mama kapata masahibu gani na ni kichaa au … ‘Vipi mume wangu wamesemaje huko hospitalini..’ ‘Mmmm, kuna tatizo, la kikazi, na inavyoonekana ni kuwa mdogo wako alikabidhiwa mgonjwa kumuhudumia, na mgonjwa huyo alikuwa kafanyiwa upasuaji, alikuwa hajazindukana, na katika kumhudumia, akatoka kidogo kufuata dawa, aliporudi huyo mgonjwa akawa….’ Mara simu ikalia na kumkatisha mazungumzo…... ******* Naona tushie hapa kwa leo, kwani matukio mengi yametokea kwa pamoja, ili tuweze kutafakari na kuyaweka pamoja, tuonane kwenye sehemu ijayo...TUWEMO! Ni mimi: emu-three
http://miram3.blogspot.com/feeds/posts/default?alt=rss

"