Adverts

Jan 21, 2011

Nitaendelea Kupinga Malipo Dowans-Sitta

Nitaendelea Kupinga Malipo Dowans-Sitta: " SIKU moja baada ya vyombo vya habari kuripoti kuwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Samwel Sitta amefungwa mdomo na Baraza la Mawaziri ili aache kuzungumzia suala la Dowans, ameibuka na kusema hawezi kufungwa mdomo kupinga malipo ya sh bilioni 94 kwa kampuni ya kitapeli. 'Naomba wananchi wafahamu kuwa siwezi kufungwa mdomo kupinga malipo kwa kampuni ya kitapeli ya Dowans,' alisema Bw. Sitta alipozungumza na baadhi ya vyombo vya bahari Dar es Salaam jana. Kulingana na taarifa za gazeti moja jana, Bw. Sitta pamoja na Naibu Waziri wa Ujenzi, Dkt. Harrison Mwakyembe wamebanwa katika kikao cha Baraza la Mawaziri na kutakiwa wasizungumzie tena suala hilo hadharani 'ili waache mipango ya serikali iende kama ilivyopangwa'. Bw. Sitta ambaye alikuwa Spika wa Bunge la Tisa wakati mjadala wa Mkataba wa kampuni ya feki ya Richmond na baadaye Dowans unatikisa nchi, alisema hajawahi kutishwa wala kufungwa mdomo kuhusu msimamo wake. 'Sijawahi kuitwa popote wala na mtu yeyote na kuambiwa nisizungumze suala hilo, nitaendelea kupinga malipo ya Dowans. Hivyo wananchi wasifikiri nimebadili msimamo. 'Taarifa zinazosambaa ni za kupikwa tu, zisije zikawapotosha wananchi wakadhani nimewasaliti katika hili, narudia tena sijafungwa mdomo,' alisisitiza Bw. Sitta ambaye pia ni mbunge wa Urambo Mashariki. Mbunge huyo ambaye alitemwa asigombee uspika kwa mara ya pili na Kamati Kuu ya CCM kwa kilichodaiwa kuzingatia suala la jinsia, alifafanua kwamba sauti yake haitasikika tu kwa suala la Dowans pakee, bali ataendelea kupinga mambo yote machafu nchini. 'Nchi inahitaji viongozi wenye kusimamia vema maslahi ya taifa bila hofu ili kulinda haki za wananchi na kuboresha maisha yao, alisema Bw. Sitta. Akizungumzia madai ya kukiuka kiapo cha uwajibakaji wa pamoja, Waziri huyo alisema kama dhana hiyo ingekuwa inaheshimika uamuzi wa kuilipa au kutoilipa Dowans ungefanywa kwa pamoja, badala ya kutangazwa tu na Waziri wa Nishati na Madini. Alisema haiwezekani dhana ya uwajibikaji wa pamoja ifanyike bila kushirikisha wengine halafu mwisho itolewe taarifa ya uwajibakaji wa pamoja. 'Halafu kuna watu wanazungumzia nimekiuka dhana ya uwajibikaji wa pamoja, uwajibikaji wa pamoja ni lazima uamuzi ushirikishe wengine si mmoja kuamua halafu ifahamike ni uwajibakaji wa pamoja,' alisema. Kiongozi huyo alisisitiza madai yake dhidi ya uharaka wa kulipa tuzo ya Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Kiabiashara (ICC) kuwa unatia mashaka.'Hii haraka ya kuilipa Dowans ni ya nini? Nchi hii ina madeni ya muda mrefu kama yale ya Benki ya Dunia na IMF lakini hakuna uharaka wa kulipa kama huu, sasa kasi hii inatoka wapi?' alihoji. Kauli hiyo ya Bw. Sitta imekuja ikiwa ni siku moja baada ya Hukumu ya Dowans kudaiwa kuwasilishwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania kwa ajili ya usajili ili taratibu za malipo zianze, huku wanaharakati wa haki za binadamu, wakiongozwa na Kituo cha Sheria na Utawala Bora (LHRC) wakiwa wameshatangaza nia yao ya kufungua kesi kupinga malipo hayo. Habari zilizotufikia wakati tunakwenda mitamboni zimesema kuwa Waziri Sitta na Dkt. Mwakyembe kwa pamoja wamewasilisha nia ya kulishtaki gazeti moja la kila siku ambalo liliripoti taarifa za kunyamazishwa kwa viongozi hao, wakidai kuwa ni za uongo. Katika barua yao kwa Mhariri Mtendaji wa gazeti hilo, mawaziri hao walisema: 'Tunakuandikia barua hii upime mwenyewe utuombe radhi kwa uongo huo uliotutungia ukurasa wa mbele wa gazeti lako au usubiri tukuburuze mahakamani kukukumbusha kuwa Tanzania si 'Banana Republic' bali ni nchi yenye kuheshimu utawala wa sheria.
"