Adverts

Jan 25, 2011

Sakata La Dowans Kutorudishwa Bungeni:Pinda

Sakata La Dowans Kutorudishwa Bungeni:Pinda: " SERIKALI imesema mjadala kuhusu fidia ya kampuni ya Dowans hautarudishwa bungeni na badala yake itafuata taratibu za kisheria kwa kwenda mahakamani ili mkondo wa sheria uchukue mkondo wake. Mahakama ya kimataifa ya usuluhishi wa migogoro ya kibiashara hivi karibuni ililiamuru shirika la uzalishaji na ugavi wa umeme nchini (TANESCO) kuilipa Dowans fidia ya shilingi bilioni 94 baada ya kulitia hatiani kwa kuvunja mkataba baina yake na kampuni hiyo kinyume cha taratibu za kisheria. Msimamo mpya kuhusu Dowans ulitolewa jana na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, katika mkutano wake na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika semina ya siku tatu kwa wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM), iliyofanyika Blue Peal Hotel, Ubungo Plaza, jijini Dar es Salaam ambapo alisisitiza kwamba suala la fidia ya Dowans halina ujanja kwani ni la kisheria na kwa hiyo ni lazima tulishughulikie kisheria. “Hatutalipeleka suala hili bungeni….kulipeleka huko itakuwa ni kwenda kujadili siasa na si sheria. Na kwa hili tayari kuna timu ya wabunge wa CCM ambao ni watalaamu wa sheria pamoja na timu itakayoundwa na serikali, timu hizo zitakaa na kupitia kwa makini suala hili ili twende tukatafute ufafanuzi huo wa kisheria,” alisema Pinda. Alisema mjadala huo wa hukumu ya Dowans umeibua hisia za watu mbalimbali nchini na hata kupelekea baadhi ya viongozi wa serikali kuingilia kati na kutoa misimamo yao hali ambayo haikuleta taswira nzuri kwa taifa. “Kila mtu ana uhuru wa kutoa maoni yake, na hata mawaziri waliopishana kauli ni ugeni wa masuala ya serikali tu, lakini jambo hili ni letu sote kama serikali na hivi sasa tumejiweka sawa ili kuepusha hali kama hii isijirudie tena,” alisema Pinda. Akisoma maazimio ya semina hiyo Kaimu Katibu wa Kamati ya Wabunge wa CCM, Jenista Mhagama, alisema kamati yao imeishauri serikali kutafakari kwa makini hukumu hiyo na kutumia njia za kisheria kuangalia uwezekano wa kutolipa fidia hiyo. “Kuhusu deni la Dowans kwa TANESCO la sh 94 bilioni kamati ya wabunge wa CCM wameitaka serikali kupitia njia za kisheria itazame upya suala hilo kwa nia ya kutafuta uwezekano wa kuwaepushia Watanzania mzigo huu,” alisema Mhagama. Alisema wabunge wa CCM wametakiwa kutumia kamati ya wabunge kwa ukamilifu kujadili masuala yote na hata kukosoana ndani ya vikao vya kamati kwa uwazi ili kulinda maslahi ya wananchi na taifa kwa ujumla. Hata hivyo Mhagama alisema semina hiyo imewapa uhuru kamili wabunge hao kuikosoa serikali na kutoa mawazo yao kuhusu masuala yote yenye maslahi kwa taifa ili mradi watumie lugha ya ufasaha. “Hotuba ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete, imetupa uhuru wa kuikosoa serikali na vyombo vyake ili mradi tu lugha ya ufasaha itumike katika kutoa maoni,” alisema Mhagama. Alisema wabunge hao wameunda kamati ndogo ya kufanya marekebisho ya kanuni za wabunge wa kamati wa CCM na kuwa na wajumbe kumi ambao wataongoza timu hiyo. Aliwataja wajumbe wa kamati ya marekebisho ya kanuni za CCM kuwa ni Jenista Mhagama, Dk. Maua Daftari, Pindi Chana, Bernadeta Mushashu, Christopher Ole Sendeka na Andrew Chenge. Wengine ni Dk. Harison Mwakyembe, Gosbert Blandes, Mshadhi Maalim na George Simbachawene.
"