Adverts

Jan 28, 2011

Taarifa kwa Vyombo Vya Habari - Mazungumzo ya Rais Kikwete na Balozi wa Marekani Tanzania

Taarifa kwa Vyombo Vya Habari - Mazungumzo ya Rais Kikwete na Balozi wa Marekani Tanzania: "
Tanzania imeteuliwa kuwa moja ya nchi nne duniani itakayofaidika na mpango maalum wa serikali ya Marekani unaojulikana kama Feed The Future (FTF). Balozi wa Marekani nchini Tanzania Mhe. Alfonso E. Lenhardt amemueleza Rais Jakaya Mrisho Kikwete leo mchana katika Ikulu ya Dar es Salaam.
“Huu ni mpango maalum unaolenga katika kuendeleza na kukuza kilimo, kuongeza uzalishaji wa chakula na kupunguza uhaba wa chakula” Balozi Lenhardt amemweleza Rais Kikwete na kumhakikishia kuwa Marekani imekusudia kushirikiana na Tanzania katika juhudi hizi.
Balozi Lenhardt amesema mpango huu sio tu utaongeza upatikanaji wa chakula nchini lakini pia utaongeza uwezo wa Tanzania katika kufanya mambo mengi zaidi katika sekta hii ya Kilimo.
'Mpango huu utaipatia Tanzania vitendea kazi na kuiwezesha kujenga uwezo wake wa kuzalisha zaidi na kutengeneza fursa nyingi zaidi' Balozi ameongeza.
Nchi zinazolengwa katika mpango huu ni Tanzania, Ghana, El Salvador na Ufilipino.
Balozi Lenhardt amesema Tanzania na nchi zingine tatu hizi zimechaguliwa kutokana na juhudi zake katika utawala bora, juhudi za nchi hizi katika masuala ya kilimo, ardhi ya kutosha, maji ya kutosha.
'Uongozi wako makini ndiyo ulioiwezesha Tanzania kuwa moja ya nchi hizi duniani, umetoa nafasi kwenye sekta binafsi ktk kuwekeza ktk Kilimo na tupo hapa kukunga mkono kwenye vipaumbele vyako na mipango yako' Balozi Lenhardt amemueleza Rais Kikwete.
Maeneo yatakayo anza kufaidika na mpango huu ni Zanzibar, Morogoro, Dodoma, Manyara, na maeneo ya kanda za juu Kaskazini na za Kusini mwa Tanzania. Rais Kikwete ameishukuru serikali ya Marekani na amemweleza Balozi Lenhardt kuwa msaada huu ni muhimu na nyeti sana kwa Tanzania katika sekta hii ya Kilimo
ambapo asilimia 80 ya watanzania wanategemea Kilimo.
'Tukiongeza uzalishaji katika kilimo tutaweza kuwafikia Watanzania kwa asilimia 80 ambao wanategemea kilimo, na huo ni msaada na juhudi kubwa sana”. Rais amesema.
Imetolewa na Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
Ikulu.
Dar es Salaam.
24 Januari, 201
"