Adverts

Jan 25, 2011

Tusitorokane, jamani tupime VVU kwa pamoja kuonyesha upendo wa kweli.

Tusitorokane, jamani tupime VVU kwa pamoja kuonyesha upendo wa kweli.: "

Na Zaina Malongo

RAIS Jakaya Kikwete na mkewe Salma, walipima pamoja virusi vya Ukimwi. Walifanya hivyo ili kufahamu afya zao lakini jambo kubwa zaidi walikuwa na lengo la kuwahamasisha watanzania kujenga utamaduni wa kupima pamoja wakiwa na wenza wao.

Hatua hiyo ilifikiwa baada ya takwimu kuonyesha kwamba watu walioko kwenye ndoa walikuwa katika kundi lenye maambukizo makubwa ya virusi vya Ukimwi.

Takwimu za kiutafiti kutoka katika Tume ya Kudhibiti maambukizi ya Ukimwi Tanzania (TACAIDS) ya mwaka 2007-08, zinaonyesha kuwa asilimia sita ya wanandoa, mmoja wapo ameambukizwa VVU wakati asilimia 2.5 ya wanandoa wote wawili wana maambukizi.

Lakini jambo la kujiuliza ni kwa nini wanandoa wanahamasishwa kupima virusi vya Ukimwi pamoja na wenza wao.

Muelimisha rika wa Mtandao wa Watu wanaoishi na vvu wilaya ya Ilala, Karoline Katunzi anasema bado wananchi wengi hawana uelewa wa masuala ya Ukimwi hivyo hawaelewi umuhimu wa kupima hasa huko vijijini ambao utatikanaji wa elimu ni shida.

Anasema hata viongozi wa dini ambao ni waelewa wengi wao hawaelewi umuhimu wa kupima wakiwa na wenza wao kwa sababu wengi hawajaelimishwa.

Pia anasema mfumo dume umesababisha wanandoa kutopima pamoja kutokana na wanaume kutotaka kushinikizwa na wake zao kuhusu masuala mbalimbali yanayowahusu.

Aidha muerimisha rika huyo anasema faida ya wanandoa kupata ushauri nasaha na kupima vvu pamoja ni kama mmoja wao anapatikana na virusi na mwingine hana, watapata ushauri nasaha namna wanavyoweza kujamiiana bila kuambukizana. Pia wataelimishwa namna ya kuishi maisha marefu wakiwa na virusi vya ukimwi.

Anasema kwa wanandoa ambao wote watapima na kuonekana kuwa na virusi , watapata ushauri nasaha namna wanavyoweza kujamiiana bila kuambukizana au kubadilishana virusi kama njia ya kuwafanya waongeze muda wa kuishi.

Hata kama wanandoa wote wanaishi na virusi vya ukimwi, hawatakiwi kufanya tendo la ndoa bila ya kinga, kwani virusi vipo vya aina tofauti, vinapochanganyika madhara yake huwa makubwa kwa wahusika.

Anasema pia watashauriwa namna wanavyoweza kupata watoto wasiokuwa na maambukizi ya virusi kupitia mpango wa kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

Kwa mujibu wa TACAIDS, mtoto ambaye wazazi wana vvu, anaweza kuwa salama ikiwa wazazi walitumia mpango huo.

Aidha faida nyingine, muelimisha rika huyo anasema, kama wanandoa wanapima na majibu kuonyesha kwamba wote hawana vvu, pia watashauriwa namna wanavyoweza kujikinga wasiambukizwe.

“ Ikumbukwe kwamba upimaji wa pamoja kwa wanandoa au marafiki walio kwenye mahusiano ya kimapenzi unaimarisha mahusiano bila kujali ni matokeo gani yamepatikana baada ya kupima, hii itawasaidia kufungua ukurasa mpya wa mahusiano kwa kufuata ushauri nasaha mliyopewa kutokana kwa wataalam,” anasema.

Changamoto zilizopo katika uhamasishaji kwa wanandoa katika kupima vvu ni kwamba, vituo vya ushauri nasaha na kupima havitosherezi mahitaji ya wananchi hasa vijijini ambako hutakiwa kusafiri umbali mrefu ili kufuata huduma hiyo.

Muelimishaji rika huyo anasema jambo la kufanya, ni kuendelea kutoa elimu, hasa kwa kuwatumia viongozi wa dini kwa sababu wanaheshimika katika jamii.

Anasema viongozi hao wako kila mahali hivyo ni rahisi kuwafikia wananchi walio wengi zaidi.

"