Na Mwandishi Wetu
WAJUMBE wa Kamati ya maandalizi ya tamasha la Pasaka ya Msama Promotions wanakwenda nchini Afrika Kusini kwa ajili ya kukutana na wasanii wa muziki wa Injili watakaokuja kutumbiza nchini.
Waimbaji hao wa muziki wa Injili watakaoteuliwa wanakuja nchini kwa ajili ya kutumbuiza kwenye tamasha kubwa la nyimbo za kumsifu Mungu litakalofanyika siku ya sikukuu ya Pasaka Aprili 24 mwaka katika ukumbi wa Dimond Jubilee.
Mwenyekiti kamati ya Msama Promotions waandaaji wa tamasha la pasaka, Alex Msama amesema kwamba lengo la kamati hiyo kwenda nchini Afrika Kusini ni kwa ajili ya kuangalia waimbaji gani wa muziki wa Injili wenye majina makubwa ambao watakuwa na sifa ya kuja kutumbuiza katika tamasha hilo kubwa hapa nchini.
Pia Msama amesema kwamba waimbaji nane wa muziki wa Injili kutoka Kenya na wengine saba kutoka nchini Rwanda wamethibitisha kushiriki katika Tamasha hilo.
“Tumewapata waimbaji nane wa injili kutoka Kenya ambao wamethibitisha kuja nchini kutumbuiza siku ya tamasha la Pasaka na wengine saba kutoka nchini Rwanda,” amesema Msama.
Aida Msama amesema kwamba kutafanyika mchujo mkubwa kati ya waimbaji hao 15 kutoka Rwanda na Kenya ili kuwapata wawili wakali watakaotumbuiza katika tamasha la Pasaka.
“Pamoja kwamba wamethibitisha waimbaji 15 mpaka sasa kutoka nchi mbili za Kenya na Rwanda, lakini tutafanya mchujo kwa ajili ya kuwapata waimbaji wawili kwa ajili ya tamasha hilo,” alisema Msama.
Msama amesisitiza kwamba tamasha la mwaka huu litakuwa na utofauti mkubwa ikilinganishwa na matamasha mengine yaliyopita, kwani limeboresha zaidi.
Msama amesema kwamba tamasha la mwaka huu limekuwa na maboresha makubwa mno kwa ajili ya kukidhi matakwa ya wapendwa wengi.
Aidha Msama amesema kwamba baada ya tamasha hilo pia litafanyika katika mikoa ya Shinyanga Jumatatu ya Pasaka Aprili 25 na Mwanza Aprili 26 ambayo itakuwa ni sikukuu ya Muungano.
"