Wakazi wa Kijiji cha Ihanda wilayani Mbozi wameendelea kuonyesha hasira zao dhidi ya serikali kwa kushindwa kujenga matuta kwenye kijiji hicho na kusababisha ajali za mara kwa mara.
Katika hatua ya jana wananchi hao wamefunga maduka baada ya kudaiwa mmoja wa viongozi kueleza kuwa sababu za ajali eneo hilo ni wafanyabiashara kujenga maduka pande zote mbili za barabara.
Kutokana na hali hiyo maduka yamefungwa kwa siku nzima na kusbabaisha wananchi kukosa huduma za kila siku na kwamba hali ikiendelea kuwa hivyo kuna uwezekano wa kuzunsha matatizo mengine ya kijamii.
Ili kujiweka sawa mkuu wa wilaya ya MBOZI Gabriel Kimolo kesho asubuhi atafanya mkutano wa hadhara na wananchi hao kwa lengo la kujadili njia bora ya kutatua tatizo hilo, ingawa tayari wameshasema hawataki Siasa zaidi ya kuona matuta yakijengwa.
Mwezi Decemba mkuu wa wilaya ambaye alishuhudia moja ya ajali zilizotokea kijijini hapo aliahidi kujengwa matuta kabla ya wiki tatu kupita hata hivyo zoezi hilo halijatekelezwa hadi juzi lilipotokea tukioo jingine lililosababisha basi aina ya coaster kuchomwa moto na kuharibiwa kwa magari mawili likiwemo basi la Hood.
Katika songombingo hiyo ililazimu mkuu wa wilaya kujificha na kuvaa kilemba kama msomali ili kujificha wakati akifuatilia tukio la vurugu kijijini hapo ambapo vijana wadogo walipandisha mori na kuanza kushambulia magari yanayopita kijijini hapo.
Watu walioruhusiwa kupita eneo hilo waliambiwa wapite kwa miguu bila pikipiki wala magari, hali ambayo ililazimu watu kushuka kutoka gari upande mmoja na kutembea umbali wa kilometa moja hadi upande mwingine na kupanda magari yaliyopo upande wa pili kwa staili ya kufaulishana.