Serikali imeombwa kurahisisha mawasiliano ya mtandao (inteneti) kwa wananchi wengi zaidi hasa vijijini kusaidia maendeleo nchini.
Akizungumza nami jana kabla ya kurejea nyumbani baada ya kukutana na kuhutubia mamia ya Watanzania wakazi wa Uingereza, mwanahabari na mwanablogu mashuhuri, Issa Michuzi, alisisitiza hakuna wakati ambapo suala la mawasiliano ya habari duniani limekuwa kiungo cha maendeleo kama sasa.
Michuzi akihutubia kadamnasi, London (Picha toka Blogu ya Haki Ngowi)
Akitoa mfano wa Marekani ambako ndipo penye chimbuko la fani hii ya kublogu Mtanzania huyu alisema karibuni serikali hiyo imepitisha sera ya kufanya mawasiliano ya mtandao bure kwa jumuiya za vijijini. “Mtandao Bongo bado ni mgumu na aghali sana kwa wengi,” alikiri Michuzi.
Mwanahabari na mpiga picha huyu alikaribishwa kuhudhuria mkutano wa Watanzania ughaibuni (Diaspora) uliotayarishwa na Ubalozi wetu na Jumuiya ya Watanzania Uingereza. Wadhifa huo wa kuja kuhutubia kikao umetokana na utambuzi wa mchango wake Michuzi katika suala la mawasiliano na habari katika kipindi cha miaka minne tu. Alijiunga na wataalamu mbalimbali wengine wakiwemo maofisa wa uhamiaji, wanasheria na wafanya biashara waliohutubia na kujibu maswali wakati wa mkutano huu uliofanyika siku mbili karibu na uwanja maarufu wa Wembley.
Mkutano ulifunguliwa rasmi na Waziri wa Mambo ya nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Balozi wetu Uingereza, Mwanaidi Maajar. Barua iliyoandikwa na kutiwa saini toka Rais wa Jamhuri, Jakaya Kikwete ilisomwa kwa washiriki wa mkutano, ikiahidi kuunga mkono umoja ulioonyeshwa na Watanzania ugenini.
Blogu lake Michuzi liitwalo “Libeneke la Jamii” karibuni imetokea kuwa moja ya viungo vikuu vinavyotegemewa kihabari mbalimbali bila kuficha, hasa kwa Watanzania ughaibuni, likiwa bega kwa bega na vyombo vingine mahsusi vya habari na redio nchini.
Akipigiwa makofi na takribani washiriki mia tatu, Issa Michuzi alikumbusha kwamba suala la habari lina nguvu na uwezo sana kuhamasisha na kuendeleza majadiliano baina ya watu, serikali na maendeleo ya kijamii. Alikumbusha kwamba hata hivyo blogu tatu kuu mashuhuri: Michuzi, Haki Ngowi na Maggid Mjengwa (Kwanza Jamii); magazeti na Redio vimekwama kwa kutoa habari zile zile zinazorudiwa rudiwa.
“Habari hizi zilizoshazoewa na wananchi zimeanza kuchosha yaani starehe, siasa na udaku. Iko haja kuchukua maoni na habari kutoka vijijini kuanzia Ukerewe, Moshi, Muheza na Tukuyu. Ila haiwezekani kama mtandao haupatikani kirahisi mashambani.”
Majuma mawili yaliyopita BBC ilikutanisha Wanablogu na Waandishi wa habari kutathmini mawasiliano kati ya vyombo hivi. Toka kushoto, Freddy Mtoi (Mwandishi wa kujitegemea), Salim Kikeke (BBC Swahili), Zuhura Yunus (BBC Swahili) na mdau wa Kitoto.Haya ndiyo baadhi ya mambo anayoongelea Michuzi. (Picha na Hassan Mhelela wa BBC Swahili)
Akitoa takwimu Michuzi alisema toka mawasiliano ya mablogu yalipoanza mwaka 1995 kupitia Mmarekani Jorn Barger, zimeanzishwa blogu milioni 112.
Tanzania inao wanablogu 200 na kila juma blogu zaidi ya kumi zinaanzishwa. “Umefika wakati kutambua nafasi ya mawasiliano ya mtandao kama chombo mahsusi cha majadiliano na ujenzi wa jamii kati ya serikali na wananchi,” alisisitiza.
Akamalizia kusema yuko tayari kuwa kiungo cha ushirikiano wa wanahabari (kama vile Jamii Forums) kati ya wananchi Bongo na wale waishio nchi za nje.
Waandishi na wanablogu mbalimbali toka kila pembe za dunia walipokutanishwa na idhaa mashuhuri ya BBC mwezi jana katika ukumbi wa Shoreditch Hall, mjini London (Picha na Narama Terima toka Kenya)
Wanahabari Zuhura Yunus (BBC Swahili) mwanzo kushoto, Freddy Mtoi ( wa pili toka Tanzania), na Tarama Nerima (toka Kenya) katika warsha hiyo. (Picha na Salim Kikeke)
Swali moja kuu lililoulizwa wakati wa kongamano lilochukua siku nzima,( Alhamisi tarehe 18 Machi) ni je, wananchi wa nchi zetu changa na maskini watawezaje kusaidiwa kuyafikia zaidi haya mawasiliano ya mtandao ndani ya dunia ya sasa inayotegemea sana technolojia hii muhimu?
Mahojiano kuhusu Blogging na Alice Muthengi mtangazaji wa BBC toka Kenya. (Picha na Hassan Mhelela)
Mazungumzo na maswali kuhusu Blogging na Charlotte Attwood wa idhaa ya BBC -Kiingereza (Picha na Hassan Mhelela)
" new post