MAZISHI ya Diwani wa Kata ya Majengo halmashauri ya Jiji la Mbeya,Francis Shayo(CCM) yameonyesha kugeuka kama uwanja wa siasa baada ya vyama kuanza kampeni za wazi wazi katika mazishi hayo .
Mtandao huu wa www.francisgodwin.blogspot.com umepata kushuhudia mwenendo mzima wa mazishi hayo ambapo baada ya taarifa za kifo hicho kutangazwa rasmi februari 13 kuwa,Diwani huyo amefariki alipokuwa amelazwa katika hospitali ya Rufaa ya Mbeya, kuliamsha upya kampeni za kisiasa kutoka kwenye vyama vitatu, huku kukiwa na vikao visivyokuwa rasmi vikielezea mikakati ya vyama hivyo kuziba pengo lililoachwa na Diwani Shayo(54).
Jana hali ndipo ilipokuwa tete zaidi katika msiba wa Diwani huyo aliyewahi kuwa diwani wa TLP kabla ya kujiunga na CCM mwaka 2005 akiiongoza kata hiyo kwa kipindi cha tatu pale vyama vyote vitatu vilipojitokeza kwa mbwembwe kuhani msiba huo kulikoashiria kampeni za wazi.
Umati mkubwa uliokuwa umehudhuria msiba huo ukiwa umetawaliwa kwa sare za CCM na Chadema na vyama vyote vikipeperusha bendera zao hawakuweza kuishia hapo isipokuwa dalili zilionyesha kila chama kikitafakari jinsi ya kuanza kampeni hizo baada ya msafara wa diwani huyo kwenda Kilimanjaro kwa mazishi.
Msafara wa magari zaidi ya 10 waliyopanda madiwani wa Chadema wapatao 18 huku wakipeperusha bendera za chama chao, ulipoingia nyumbani kwa marehemu ,Shayo majira ya Saa 5.30 hali iliyoonyesha wazi kuwakera wana CCM ambao wengi walilalama kichinichini kuwa wamefuata nini hapo.
Hali ikiwa hivyo ,dakika chache baadae liliingia gari dogo aina ya Hiece likiwa limetundikwa bendera kubwa za chama cha CUF na kujiunga nay ale yaliyokuwa yakipeperusha bendera za CCM na Chadema kitendo kilichoashiria wazi kuwa msiba huo tayari uligeuzwa ulingo wa kisiasa na kampeni za kuziba pengo hilo kabla mwili haujazikwa.
Dosari ya msiba huo ilianza kujitokeza pale mrusha matangazo ya CCM alipotamba kuwa msiba huo ni wao na kuvitaka vyama vingine vya siasa kuwa na adabu ,kauli ambayo ilionyesha wazi kuwakera madiwani wa Chadema waliofika kwa ajili ya kumuaga diwani mwenzao bila kujali itikadi ya vyama wanavyotoka.
Kauli hiyo ilimsukuma ,Mstahiki Meya wa Jiji hili,Athanas Kapunga(CCM) aeleze wazi kuwa huo msiba ni wa kiserikali japokuwa marehemu ni kada wa CCM na kuagiza madiwani wote waende wakavae magauni yao na kufuata taratibu za mazishi yasiyokuwa na itikadi ya vyama.
“Waheshimiwa madiwani wote mliopo hapa naona huu msiba umegeuzwa uwanja wa siasa,sasa kama mstahiki meya wa jiji nawaagiza wote mkavae magauni yenu,mjemjipange pembeni ya jeneza lililobeba mwili wa Mheshimiwa Shayo” alisema Kapunga.
Agizo hilo lilitelekezwa haraka na katika muda mfupi madiwani wa CCM na Chadema wote walivaa magauni yao ,CUF wao waliokuwa katika msiba huo hawana diwani katika halmashauri ya jiji hilo wao waliendelea kushuhudia kampeni za chini chini zilizokuwa zikiendelea.
Katika msiba huo,Mwenyekiti wa Chadema wilaya ya Mbeya mjini,John Mwambigija alitoa ubani wa Sh 100,000 kwa familia ya marehemu Shayo na kudai kuwa kama chama kinachojali uhai wa binadamu yoyote bila kuguswa na itikadi za kisiasa wameshtushwa mno na kifo cha Shayo kuwa alikuwa Diwani wa watu na mpambanaji.
Mwambigija alisema kuwa ,Chadema wanaungana na jamii nzima ya Kata ya Majengo katika msiba huo mzito na kudai kuwa wamepoteza mtu muhimu na makini na kuwataka wale wanaodhani kuwa huo ulikuwa ni msiba wa kampeni wasubiri wakati wake kwa mujibu wa taratibu za uchaguzi.
Diwani Shayo alisafirishwa jana kuelekea kijijini kwao Mengeni Chini ,wilaya ya Rombo mkoa wa Kilimanjaro huku akiwa amemwacha mjane Joyce na watoto wake watatu,msafara ulioongozwa na Mstahiki Meya wa jiji hilo,Kapunga.
Bofya hapa