WANANCHI  wenye hasira kali wakazi wa eneo la Meta jijini Mbeya jana  nusuru  wamtoe  roho aliyekuwa mfanyabiashara  wa nyama katika eneo hilo aliyetambuliwa kwa jina moja la Stanley baada ya  kijana  huyo  kuigeuza siku ya wapendanao  kuwa siku ya wachukianao kwa kuwajeruhi  watu zaidi ya wanne kwa mapanga na kuharibu mali mbali mbali  baada ya kudaiwa kutumia dawa za kulevya aina ya  bangi.
Tukio  hilo ambalo  lilikuwa kama sinema katika  eneo hilo la Meta na kupelekea  umati mkubwa wa wananchi kufurika katika eneo hilo lilitokea majira ya saa 8 mchana  muda mfupi bada ya kijana huyo kuwajeruhi watu  watatu kwa mapanga na kuharibu mali mbali mbali  likiwemo lori lenye namba za usajili SU 37740 mali ya shirika la umeme jijini Mbeya.
Wakielezea tukio hilo kwa mwandishi wa habari  hizi baadhi ya mashuhuda  walidai kuwa kijana huyo alikuwa akifanya kazi ya kuuza bucha katika  eneo hilo alipata kusimama  kuendelea na kazi hiyo kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa kabla ya jana  kuibukia katika eneo hilo la bucha  huku akiwa na kisu aina ya sime mfukono.
Walisema kuwa  baada ya kufika eneo hilo alimtishia mfafanyabiashara wa matunda katika eneo hilo kuwa amekuja kwa ajili ya kumuua hali  iliyopelekea mwanamke huyo kuacha biashara yake na kukimbilia kituo cha  polisi kilichopo jirani na  eneo hilo.
Hata  hivyo  walisema baada ya mwanamke huyo  kwenda polisi  kuripoti juu ya uvamizi  huo  kijana  huyo aliendelea kuharibu matunda yake pamoja  na meza na baada ya hapo aliligeukia lori   la Tanesco  na kuanza  kulikata mapanga kabla ya wafanyakazi wake  wawili kujitosa kupambana na kijana huyo ambaye alipata  kuwajeruhi wa panga .
Waliwataja  watumishi hao wa Tanesco ambao  walijeruhiwa  kuwa ni Geofrey Bukuli na  Peter Mwasantaja  na kupelekea  wafanyakazi  wenzao kutimua mbio na kuliacha  lori  hilo kabla ya wananchi  kuamua kuanza kupambana na kijana  huyo kwa mawe ,marungu na mapanga .
Hata   hivyo wakati mapambano hayo yakiendelea kijana  huyo alikimbilia dukani kwa Bi Irene Mpoki na  kumjeruhi kwa panga  mkono wake wa kulia wakati akimzuia kuingia dukani  kujificha  hali iliyozidisha jazba za wananchi hao na  kupelekea  kijana  huyo kutoka nje ya  duka hilo na kwenda kumjeruhi mwananchi mwingine kwa panga mgongoni.
Katika  kile kilichoonyesha  kuwa kijana huyo alikuwa amechanganyikiwa vibaya ni pale alipokimbia na  kwenda  kujificha katika baiskeli ya mtu mwenye  ulemavu akiamini kuwa ni  kificho  kizuri ama kichaka hali iliyopelekea  wananchi  kumzingira na  kutaka  kumchoma moto kabla  ya kijana  huyo kumnyanyua juu mlemavu huyo na kumgeuza ngao yake kwa wananchi hao ambao  tayari  walikuwa  wamemzingira na tayari kwa kumchoma moto.
Kifo cha kijana  huyo kiliepushwa na askari  polisi waliofika katika eneo hilo na kumchukua na  kumpeleka kituo cha  polisi huku tayari wananchi  wakiwa  wamemjeruhi kwa mapanga kichwani na mgongoni pamoja na  kumpiga mawe  kiasi cha kutosha hali ambayo ilionyesha wazi kijana  huyo  kuwa hoi kwa kipigo hicho.
Kamanda wa  polisi wa mkoa wa Mbeya Advocate Nyombi alithibitisha  kutokea kwa tukio  hilo la  kudai kuwa  ushirikiano mzuri wa wananachi na jeshi la polisi ndio uliookoa maisha ya  wananchi zaidi  kujeruhiwa kwa panga na kijana  huyo na kuwa vinginevyo kijana huyo angeweza  kusababisha maafa makubwa zaidi.
 
