Adverts

Feb 16, 2011

Hotuba ya Waziri Mkuu Bungeni Feb 15, 2011


Hotuba ya Waziri Mkuu Bungeni Feb 15, 2011

MAELEZO NA UFAFANUZI WA MHESHIMIWA MIZENGO P. PINDA(MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI WA KUHITIMISHA HOJA YA KUJADILI HOTUBA YA MHESHIMIWA DR. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, TEREHE 15 FEBRUARI 2011

Mheshimiwa Spika,
Awali ya yote, nami niungane tena na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Hotuba nzuri aliyoitoa wakati akizindua Bunge la kumi la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tarehe Novemba 2010. Sina shaka kuwa majadiliano ya hotuba hiyo hapa Bungeni yamedhihirisha umakini uliotumika katika utayarishaji na uwasilishwaji wake.

Nichukue nafasi hii kukupongeza wewe Mheshimiwa Spika na Naibu Spika kwa namna ambavyo mmesimamia kwa makini mjadala wa Hotuba ya Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Spika,
Nichukuwe nafasi hii pia, kuwapongeza sana Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia mjadala wa hotuba hiyo ya Mheshmiwa Rais kwa michango yao mizuri na ambayo imeisaidia Serikali kupima hatua ilizofikia katika utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi - mwaka 2005 hadi 2010 na mikakati mingine yote ya kuiletea Nchi yetu maendeleo. Jumla ya Waheshmiwa Wabunge 167 wamechangia mjadala huu. Kati ya hao, 108 wamechangia kwa kuzungumza hapa Bungeni na 59 kwa maandishi. Mjadala huu umetusaidia kujumejua maeneo tuliyofanya vizuri na yale ambayo hatukufanya vizuri. Ukweli ni kwamba, mjadala umeisaidia na kuirahisishia Serikali kazi ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi – mwaka 2010/ hadi 2015. Nawashukuruni sana!

Mheshmiwa Spika,
Katika kuhitimisha Hoja hii, si nia yangu kujadili hoja moja baada ya nyingine kama zilivyotolewa na Waheshimiwa Wabunge wakati wa kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Rais; bali nitajielekeza katika masuala makubwa mtambuka yaliyojitokeza katika michango hiyo.

1.0 SUALA LA MAREKEBISHO YA KUMI YA KATIBA YA ZANZIBAR NA HATMA YA MUUNGANO WETU

Mheshimiwa Spika,
Itakumbukwa kuwa, mwaka 2010 Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 ilifanyiwa marekebisho ya Kumi kwa lengo la kutekeleza Azimio la Baraza la Wawakilishi lililotolewa mwezi Januari mwaka 2010 kuhusiana na Muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Aidha, chini ya marekebisho hayo ya Kumi ya Katiba ya Zanzibar, yapo marekebisho mengine ambayo yalipendekezwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar yaliyolenga kukidhi hali halisi ya mabadiliko yaliyotokea Zanzibar tangu kupitishwa kwa marekebisho ya Tisa ya Katiba ya Zanzibar mwaka 2002.

Mheshmiwa Spika,
Katika mjadala wa kuchangia Hotuba ya Mheshimiwa Rais, wapo baadhi ya Wabunge ambao walichangia hoja hii. Wabunge waliochangia hoja hii waligawanyika katika makundi mawili.

Wapo Wabunge ambao hawaoni tatizo la kufanyika Marekebisho ya Kumi ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kwa kuona kuwa, Marekebisho hayo yanakidhi mustakabali wa Zanzibar; hususan marekebisho yaliyounda Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Kundi hili kimsingi pia hawaoni tishio la Muungano na wanaunga mkono Muungano uendelee kwa manufaa ya Watu wetu.

Aidha, wapo Wabunge wanaoona kuwa, Marekebisho haya ya Katiba ya Zanzibar yaliyofanywa katika mazingira haya, yamekwenda mbali na hivyo kutoa picha kwamba Muungano sasa unatetereka.

Baada ya kuwasikiliza wote, naungana na wale wanaosema kuwa, Muungano huu upo pamoja na Marekebisho ya Katiba kwa mustakabali wa Nchi ya Zanzibar na Watu wake. Bado Muungano wetu ni imara na utaendelea kuwa imara.

Bila kuingia kwa undani sana katika kutazama marekebisho haya Ibara moja baada ya nyingine, inatosha tu kusema kuwa, Marekebisho hayo ni mazuri; na yameboresha sana Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Aidha, mabadiliko hayo yameleta matumaini mapya kwa Wananchi wa Zanzibar, jambo ambalo ni la msingi sana katika maendeleo ya Nchi yeyote.

Marekebisho hayo ya Katiba pia yamesaidia kuamsha hisia sahihi kabisa za Umoja, Mshikamano, Upendo, Kuvumiliana na katika kuwaletea Wananchi wa Zanzibar maendeleo.

Mheshmiwa Spika,
Mabadiliko ya kumi ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, tunaweza kuyaweka katika makundi manne yafuatayo:

Kundi la kwanza ni masahihisho madogo madogo ya maneno na nafasi za madaraka ili kuendana na Mfumo mpya wa sasa wa Uongozi unaotokana na Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Chini ya kundi hili mpangilio mzima wa madaraka ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa umewekwa. Vilevile, kumekuwepo na marekebisho ya kuondoa baadhi ya nyadhifa za awali, kama vile, Wadhifa wa Waziri Kiongozi na kuwekwa Wadhifa mpya wa Makamu wa Pili wa Rais ambaye kimsingi kwa kiasi kikubwa ndiye aliyechukuwa majukumu yake.

Katika Kundi la Pili, Katiba imeweka Ibara mpya ambazo zinatambua uanzishwaji wa Mifumo mipya ambayo kabla ya marekebisho hayo ya Katiba hazikuwepo. Kwa mfano, baada ya marekebisho hayo, Katiba ya Zanzibar inatambua kuwepo kwa Tume ya Pamoja ya Fedha kama moja ya Chombo cha Muungano kama ilivyotambuliwa chini ya Ibara ya 134 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Taasisi nyingine muhimu zilizotambuliwa chini ya marekebisho hayo ni Tume ya Utumishi wa Mahakama na Kamisheni ya Utumishi wa Umma. Kwa mujibu wa marekebisho hayo, Kamisheni ya Utumishi wa Umma itakuwa ndicho Chombo cha juu kabisa kwa Tume zote za Utumishi chenye Mamlaka ya kusimamia na kuratibu mambo yote ya Utumishi wa Umma kwa Zanzibar. Vilevile, marekebisho haya yameanzisha Tume ya Utumishi Serikalini.

Maeneo yote haya, hayana sura yoyote inayoonyesha kwamba inapingana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977.

Kundi la Tatu ni Katiba kufanyiwa mabadiliko kwa kuwekewa Ibara ambazo baadhi ya Wabunge wamesema kuwa haziwiani na Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania. Maeneo haya ni pamoja na:
· Kueleza kuwa Zanzibar ni Nchi;
· Kuwekwa kwa Mamlaka ya Rais wa Zanzibar kugawa maeneo ya Kiutawala (Mikoa, Wilaya na maeneo mengineyo) badala ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama ilivyokuwa awali;
· Suala la ukomo wa Mamlaka ya Mahakama ya Rufani ya Tanzania katika kusikiliza baadhi ya Mashauri Tanzania Visiwani; na
· Rais wa Zanzibar kutambulika kuwa ndiye Mkuu wa Nchi ya Zanzibar.
Kundi la Nne ni Katiba hii kuwa na vipengele vinavyoendelea kuiweka Zanzibar kuwa Sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Maeneo haya ni pamoja na Ibara ya 2 inayoelekeza kuwa Zanzibar ni miongoni mwa Nchi mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshmiwa Spika,
Napenda niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wenzangu kwa ujumla kuwa, pamoja na marekebisho yaliyofanywa katika Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, marekebisho yote yaliyofanywa, kwa maoni yangu, yana utashi wa kuimarisha Muungano wetu. Hili linadhihirishwa na Ibara ya 2 ya Katiba hiyo kama nilivyoitaja hapo juu ambapo Zanzibar inajitambulisha kuwa iko ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha, endapo kuna sehemu yoyote chini ya Katiba hii inayoonekana kuwa na mgongano na masharti yaliyopo ndani ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, napenda kuwaeleza Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wenzangu kuwa, wakati wa kupitia Katiba yetu kwa lengo la kuwa na Katiba Mpya kama Serikali ilivyoelekeza, migongano yoyote inayojitokeza, itaangaliwa wakati huo kwa lengo la kuwianisha Katiba zetu hizi mbili ili kuendela kudumisha, kuimarisha na kukuza Muungano.

Nawaomba na kuwasihi Watanzania wote kuwa, tunapofanya majadiliano ya Marekebisho ya Kumi yaliyofanywa kwenye Katiba ya Zanzibar, majadiliano hayo yajikite kwenye kuimarisha, kukuza na kuendeleza MUUNGANO. Vivyo hivyo wakati wa mjadala wa kurekebisha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, dhamira yetu iwe hiyo hiyo.

Ningependa niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote kwa ujumla kwamba, Muungano wetu umeijengea Nchi yetu sifa kubwa, ni Muungano wa mfano, wa aina yake na wa kuigwa katika Bara la Afrika na duniani kwa ujumla.

Ni Muungano wa aina yake unaozingatia mazingira halisi ya eneo letu la Tanzania, kati ya Tanzania Bara na Tanzania Visiwani. Si kwamba hakuna matatizo katika kukuza Muungano, lakini ni lazima kuendeleza dhamira ya kweli katika kuimarisha Muungano wetu wa Nchi hizi mbili.

Mheshimiwa Spika,
Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wakati wa uhai wake na katika kipindi ambapo Muungano unazaliwa, aliwaasa Watanzania mambo mengi kuhusu Muungano huu. Mwalimu aliwaeleza Watanzania kuhusu
Muungano uliokuwa unapendekezwa kuanzishwa, kuwa ni Muungano ambao hauna budi kuzingatia hali halisi ya Nchi zinazoungana.

Mwalimu kupitia Hotuba yake ya tarehe 25 Aprili 1964 alisema maneno, ambao kwa maoni yangu, bado yana umuhimu mkubwa sana kwenye kuuendeleza na kuukuza Muungano wetu. Maneno hayo aliyasema kwa Kiingereza, lakini mimi naomba nitoe tafsri isiyokuwa rasmi ili Watanzania wengi zaidi waweze kujua Mwalimu alisema nini. Mwalimu alisema kwa tafsri isiyo rasmi kuwa:
“Tanganyika na Zanzibar ni majirani kwa kila hali. Kila mmoja wenu anajua ni kwa kiasi gani tuko karibu kijiografia. Naamini kwamba umbali kati ya Kisiwa cha Unguja na Kisiwa cha Pemba ni mrefu zaidi kuliko umbali kati ya Visiwa hivi na upande wa Bara wa Nchi za Afrika Mashariki. Vilevile Historia inatukumbusha kuwa wakati fulani eneo lote la Zanzibar na sehemu kubwa ya Tanganyika Bara lilikuwa likitawaliwa na Serikali moja, ambayo ni ya Sultani wa Zanzibar. Ilikuwa ni ajali ya kihistoria tu kwamba hatukuendelea kuwa Nchi moja. Wakati Wakoloni walipozitwaa Nchi za Afrika Mashariki, walikubaliana kuwa eneo lote la Visiwa vya Unguja na Pemba na ukanda wa Pwani wa Kenya liwe chini ya Himaya ya Uingereza na eneo la ukanda wa Pwani na sehemu ya eneo la Bara ya Tanganyika itawaliwe na Ujerumani. Hivi ndivyo Tanganyika na Zanzibar zilivyotenganishwa. Wakati Nchi zote za Afrika Mashariki zilipotwaliwa na Uingereza, baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, utengano huo uliendelea kuwepo. Uhuru umetupa nafasi ya kurekebisha kasoro hii.”

Katika Hotuba hiyo hiyo, Mwalimu aliendelea kusisitiza kwa maneno yafuatayo:
“Tanganyika na Zanzibar ni Nchi jirani kijiografia, kihistoria na hata kwa lugha; ni jirani kwa Desturi, Utamaduni na Siasa. Urafiki baina ya Chama cha Afro-Shiraz na TANU unafahamika vizuri kwenu nyote. Urafiki baina ya viongozi wa Vyama hivi viwili haukuanza jana. Tuna kila sababu ya kuungana; na zaidi ya yote tunazingatia shauku kubwa ya Waafrika kuungana. Na Nia tunayo pia. Mimi, kwa niaba yenu, na Rais Karume, kwa niaba ya ndugu zetu wa Unguja na Pemba, tulikutana Zanibar tarehe 22 mwezi Aprili nakutia saini Mkataba wa kuunganisha Nchi zetu mbili.”

Kwa maoni yangu, hali hiyo kwa Watanzania haina budi kuendelea kutambuliwa na kuimarishwa.
Aidha, Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere katika kitabu chake kiitwacho “Uongozi Wetu na Hatma ya Tanzania” alichokitunga katika miaka ya 1990 takriban miaka 26 tangu Muungano uanzishwe, aliendelea kuzidi kuwakumbusha Watanzania juu ya Muungano wetu ambao unazingatia mazingira halisi ya Nchi zetu mbili. Hapa alisema; Nanukuu:
Nchi mbili zinapoungana na kuwa Nchi moja, Mifumo ya kawaida ya Miundo ya Katiba ni miwili: Muungano wa Serikali moja, au Shirikisho la Serikali Tatu. Kwa Mfumo wa Kwanza, kila Nchi inafuta Serikali yake, na Nchi mpya inayozaliwa itakuwa ni Nchi moja yenye Serikali moja. Katika Mfumo wa Pili, kila Nchi itajivua madaraka fulani ambayo yatashikwa na Serikali ya Shirikisho, na itakuwa ni Serikali ambayo itakuwa na mamlaka ya juu ya mambo yaliyobaki. Mambo yatakayoshikwa na Serikali ya Shirikisho ni yale ambayo yakibaki katika mamlaka ya Nchi zilizoungana, basi kwa kweli Nchi hizo zitakuwa hazikuungana kuwa Nchi moja, bali zitaendelea kuwa Nchi mbili zenye ushirikiano mkubwa katika mambo fulani fulani.

Nchi za Afrika Mashariki zilikuwa katika hali kama hiyo kabla ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Zilikuwa Nchi tatu zenye ushirikiano mkubwa, lakini hazikuwa Nchi tatu zilizoungana kuwa Nchi moja yenye muundo wa Shirikisho. Shirikisho halisi la Nchi mbili litakuwa ni Nchi moja yenye Serikali tatu, Serikali ya Shirikisho, na Serikali mbili za awali zilizoungana kuzaa Nchi mpya moja.

Tanganyika na Zanzibar zilipoungana na kuwa Nchi Moja, tungeweza kufuata mojawapo ya mifumo hiyo ya kawaida. Lakini tulishindwa kufanya hivyo kwa sababu ya udogo wa Zanzibar na ukubwa wa Tanganyika. Zanzibar ilikuwa ina watu laki tatu (300,000) na Tanganyika watu milioni kumi na mbili (12,000,000). Muungano wa Serikali Moja ingefanya ionekane kama Tanganyika imeimeza Zanzibar. Tulikuwa tunapigania Uhuru na Umoja wa Afrika; hatukutaka tudhaniwe, hata kwa makosa, kwamba tunaanzisha ubeberu mpya! Kwa hiyo mimi nilipinga Mfumo wa Serikali Moja.

Shirikisho la Serikali Tatu lingekuwa ni gharama kubwa mno kwa Tanganyika. Zanzibar ingeendesha Serikali yake na kuchangia gharama za kuendesha Serikali ya Shirikisho; na Tanganyika ingefanya vivyo hivyo. Lakini ni dhahiri kwamba mchango wa Tanganyika ndio hasa ungeendesha Serikali ya Shirikisho. Kwa hiyo Tanganyika ingeendesha Serikali yake ya watu 12,000,000 na pia ndiyo ingetoa sehemu kubwa ya kuendesha Serikali ya Shirikisho la watu 12,300,000. Ni watu wanaofikiri kwa ndimi zao wanaodhani kuwa gharama ya Serikali yoyote kati ya hizo ingekuwa ndogo, (waulizeni Wazanzibari), na wala gharama ya Serikali ya Shirikisho isingekuwa ndogo, hata bila gharama za mambo yasiyo ya Shirikisho. Na gharama zote hizo kwa kweli zingebebwa na Tanganyika.

Kwa hiyo ilipaswa tujiulize kwa nini tunataka kuibebesha Tanganyika gharama zote hizo; na hasa kwa nini tunataka Serikali ya Tanganyika? Hivi tuna hofu ya kwamba Tanganyika bila ya kuwa na Serikali yake, itaonekana kuwa imemezwa na Zanzibar? Hofu yetu ni kwamba tukiwa na Serikali Moja, Tanganyika itaonekana kuwa imeimeza Zanzibar. Basi na tutafute Muundo ambao utaiondolea Zanzibar hofu hii ya kumezwa, bila ya kuibebesha Tanganyika mzigo wa kuendesha Serikali mbili zenye uzito unaolingana.

Hivyo ndivyo tulivyofanya, na hiyo ndiyo asili ya Muundo wa Serikali mbili. Badala ya kutungua Mfumo uliopo kama wapumbavu, tulitazama hali halisi yetu iliyokuwa, na tukabuni Mfumo utakaotufaa zaidi”. Mwisho wa kunukuu.

Katika Hotuba hiyo hiyo, Mwalimu aliwatahadharisha Watanzania kwa kusema yafuatayo:

“Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge, Muungano ambao naupendekeza katika Bunge hili ni suala la muhimu sana linalohitaji umakini wenu zaidi. Ni dhahiri kwamba Muungano huu utakabiliwa na changamoto mbalimbali. Wako watu wengi watakaoona kuwa kuendelea kwa Muungano huu ni hatua ya KUWAUNGANISHA Waafrika wote na hivyo watafanya kila njia kuuyumbisha Muungano wetu, watapanda mbegu za hofu na kusababisha chuki za kisiasa.

Inabidi tujihadhari na watu wa aina hii. Kwani mara tu baada ya kuanzishwa kwa Muungano huu, sote tutakuwa na jukumu la kuulinda na kuuendeleza. Tumwombe Mungu atusaidie sisi na ndugu zetu wa Unguja na Pemba katika kutimiza wajibu wetu.”

Mheshimiwa Spika,
Kwa kuzingatia haya yote, ninayo imani kubwa kabisa kwamba, Marekebisho haya ya Katiba ya Zanzibar, kamwe hayana nia ya kuua Muungano wetu; na ndiyo maana Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alieleza kwamba, hata kama jambo hili la Katiba Mpya lisingejitokeza kwa namna lilivyojitokeza, bado Serikali ilikuwa na wajibu mkubwa wa kuchukua mabadiliko haya ya Katiba ya Zanzibar na kufanya marekebisho stahiki katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 yatakayoweza kukidhi matakwa ya Zanzibar bila ya kuathiri Muungano wetu.

Kwa kuwa sasa tumeanza mchakato wa kuitazama upya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ninayo imani kubwa kabisa kwamba kazi hii itafanyika kwa dhamira njema na kwa kuzingatia uhalisia wa Muungano wetu.

2.0 UMOJA WA KITAIFA

Mheshimiwa Spika,
Waheshimiwa Wabunge wamezungumzia suala la amani na utulivu Nchini kwa kiasi kikubwa. Baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wameonyesha wasiwasi kuwa amani na utulivu Nchini vimeanza kutetereka kutokana na matukio mbalimbali yaliyojitokeza hivi karibuni. Kuna baadhi ya Wabunge waliosisitiza kuwa, kwa hali ilivyo, Watanzania wote kwa ujumla wetu huku tukiweka itikadi zetu za Kisiasa pembeni, hatuna budi kushikamana zaidi ili kudumisha amani na utulivu tuliokuwa nao siku zote.

Vyovyote vile itakavyokuwa, Watanzania wote kwa pamoja hatuna budi kuendelea kulinda na kuimarisha amani, mshikamano, upendo na utulivu wa Taifa letu.

Tumeweza kufanya hivyo kwa kipindi chote cha takriban miaka 50 ya uhuru tukiongozwa na Katiba ya Jamhuri ya Tanganyika na Katiba ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na baadaye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977.

Tumeweza kufika hapa tukiishi kwa amani, kwa maelewano na hivyo kuifanya Nchi yetu hii kuwa ni kimbilio la majirani zetu ambao wamekuwa wakipata misukosuko mbalimbali.Nchi yetu imekuwa kimbilio la Wakimbizi kutoka sehemu mbalimbali. Hakuna watu wanaokimbilia nchi zenye misukosuko, wanakimbilia nchi zenye amani na utulivu kama Tanzania. Sote tutambue hili, tulikubali na tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa hilo. Tumekuwa Nchi ya MFANO.

Tumeweza kufanya hivyo kwa sababu Wananchi chini ya Uongozi wa Vyama vyao vya Siasa vya TANU na AFRO SHIRAZ waliweza kila ilipobidi kufanya mabadiliko katika Katiba kwa lengo la kwenda na wakati katika maeneo muhimu waliyoyaona kwa wakati huo kwamba yaingizwe katika Katiba na Sheria za Nchi katika kuwaongoza Watanzania.

Hata baada ya Vyama hivi viwili kuungana mwaka 1977, Muungano uliotokana na ridhaa ya Vyama hivyo na Wananchi wakati huo, Tanzania imeendelea kuwa Nchi ya amani na utulivu chini ya Chama Cha Mapinduzi mpaka mwaka 1992, tulipoona kwamba ni wakati muafaka kwa Taifa letu kuwa na Mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa; ili kuruhusu Demokrasia zaidi, kupanua Uhuru wa Watu na Uhuru wa Vyombo vya Habari.

Mheshimiwa Spika,
Vyama vya Siasa kama ilivyokuwa wakati wa Mfumo wa Chama Kimoja, vinao wajibu mkubwa wa kuhakikisha vinaendeleza Amani, Utulivu, Mshikamano na Upendo miongoni mwa Wananchi wake; na visiwe Vyama vya Siasa vya kuleta mifarakano miongoni mwa Watanzania.

Sasa ni takriban miaka 20 tangu kuanzishwa kwa Mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa hapa Nchini. Kipindi hiki ni kipindi kifupi sana. Na ni kipindi ambapo Dunia inakabiliwa na misukosuko mingi ya Kiuchumi, Kijamii na Kisiasa. Tusipokuwa imara, Nchi inaweza kutetereka. Kwa hiyo, pamoja na tofauti zetu za itikadi za Kisiasa, za Dini, za Rangi na Jinsia, ni lazima tusimame wote kwa pamoja kujenga Nchi yetu.

Mheshimiwa Spika,
Nchi yetu inasifika ulimwenguni kote kwa kuendeleza amani, mshikamano na utulivu miongoni mwa Wananchi wake. Aidha, tumeishi bila ya kunyanyasana kutokana na imani zetu za Kisiasa, Dini na Kabila. Tumeishi tukiwa na itikadi tofauti za Vyama vya Siasa tangu mwaka 1992, tumeishi tukiwa na imani tofauti za Dini na Makabila tofauti zaidi ya 120 kabla na baada ya Uhuru mwaka 1961 hadi leo; lakini pamoja na tofauti hizo, wote tumeishi kwa uhuru, haki na usawa tukiheshimiana katika uhuru wa mawazo na imani. Aidha, Nchi yetu haina Kabila, bali Wananchi wake wana Makabila yenye mila na desturi tofauti.

Nchi yetu haina Dini, bali Wananchi wake wana Dini na imani tofauti; na kila mmoja anaheshimu Dini na imani ya mwenzake. Madhehebu ya Dini yana nafasi kubwa kupitia nyumba za ibada katika kuhamasisha amani na utulivu. Hivyo, nawaomba viongozi wa madhehebu yote ya dini kuunganisha nguvu zenu katika kutetea, kuhifadhi na kulinda amani na utulivu wa Nchi yetu.

Uko ukweli kwamba Nchi nyingi Duniani zenye mafanikio ya Uchumi imara ni matokeo ya juhudi za Wananchi kuwekeza katika Misingi bora ya amani na utulivu. Kwa maana hiyo, kama tunataka kujenga Uchumi imara ni lazima tulinde Nchi yetu idumu katika hali ya amani na utulivu.

Kwa maoni yangu, Bunge na Wabunge wake, linapaswa kuonyesha kwa vitendo dhamira yetu ya kujenga Taifa lenye amani na utulivu. Sisi kama Wabunge wa Bunge letu Tukufu sasa tuonyesha mfano.

3.0 DHANA YA KWAMBA KATIKA MIAKA 50 YA UHURU HAKUNA MAENDELEO YOYOTE YALIYOFANYIKA

Mheshimiwa Spika,
Katika kujadili Hotuba ya Mheshimiwa Rais, wapo baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wanaoona kwamba Taifa hili halijapata maendeleo yoyote katika kipindi cha miaka 50 ya Uhuru na kutupa lawama kwa Viongozi na Serikali zake hicho. Lakini wapo pia wanaouona ukweli kwamba Wananchi wa Taifa hili wamepiga hatua kubwa katika kujiletea maendeleo.

Naelewa wale wanaosema hakuna kilichofanyika, wanaweza kuwa wanasema hivyo wakidhani huko ndiyo kutekeleza dhana ya Vyama vya Upinzani au uwepo wa Mfumo wa Vyama vya Upinzani. Mimi siamini hivyo; na ninaamini kuwa wengi wenu mtaniunga mkono.

Mheshimiwa Spika,
Suala hili, niliwahi kulitolea maelezo nilipokuwa nahitimisha majadiliano ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, tarehe 18 Juni 2010. Nilisema; Ninanukuu:
“Mheshmiwa Spika,……naomba pia uniruhusu nitoe angalau dukuduku langu moja kwa Watanzania wenzangu. Wako baadhi yao na wengine wamo humu Bungeni ambao wamekuwa kwa muda mrefu hivi wanadiriki kubeza baadhi ya juhudi ambazo Serikali imefanya hadi hivi sasa na kuonyesha kana kwamba hapa tulipo, ni pabaya zaidi, duni zaidi, ni mahali panapotisha zaidi na panakatisha tama zaidi kuliko hata huko tulikotoka. Mimi binafsi siamini kuwa kauli hizi ni za dhati.

Naelewa kuwa, wapo Watanzania waliozaliwa kabla ya Uhuru, wako wa kipindi kati ya Uhuru na Muungano, wako pia waliozaliwa kati ya Muungano na miaka ya sabini, wako pia wa kizazi kipya. Inawezekana kabisa kwa wale wote ambao hawakuzaliwa katika vipindi vya nyuma, isiwe rahisi sana kuona tumetoka wapi na tunakwenda wapi; na kwa bahati mbaya baadhi ya kauli hizi zinatoka hapa Bungeni, kwa hiyo, ndio kusema wako katika makundi haya. Kwa wale waliozaliwa baadaye, ni dhahiri hawawezi kujua yaliyowasibu wa enzi hizo isipokuwa kwa kuelezwa au kusoma historia. Hali kadhalika, kwa waliozaliwa nyakati nyingine zilizofuata itakuwa hivyo hivyo. Ni dhahiri kuwa, kauli za namna hii kwa muono wangu, wakati mwingine zinavunja moyo, zinakatisha Watu tamaa na zinafanya ionekane kana kwamba hakuna matumaini ya kwenda mbele. Lakini ukweli uliopo ni kwamba Tanzania imepiga hatua kubwa ya maendeleo, na ninalisema hili kwa sababu hata wadau wetu wa maendeleo wanakubali kwamba Tanzania imefanya juhudi kubwa katika kuwasaidia Wananchi kujiletea maendeleo.

…Serikali chini ya Chama cha Mapinduzi, imeweza kuiongoza Nchi hii kwa kipindi chote hiki katika hali ya amani na utulivu mkubwa kabisa wa kisasa. Leo tupo hapa tunajivuna kwa kuwa na demokrasia iliyopanuka, Mfumo wa vyama vingi, uhuru mkubwa sana wa watu kwenda wanakotaka na kusema wanalotaka. Umepanua sana wigo wa Vyombo vya Habari na wakati mwingine watu wanafikiri kwamba pengine tumetoa uhuru kupita kiasi.” Mwisho wa kunukuu.
Mheshimiwa Spika.
Nimerejea kuyasema hayo kwa kuwa hata sasa katika mjadala huu wa hotuba ya Mheshimiwa Rais bado kuna Watu wenye mawazo ya kwamba katika muda wa miaka 50 ya Uhuru, Serikali haijafanya kitu chochote katika kuwaletea Wananchi wake maendeleo. Napenda tena kuwakumbusha kuwa, kuna mengi yaliyofanywa na Serikali chini ya TANU na ASP na hadi sasa chini ya Serikali ya CCM.

Mheshimiwa Spika,
Sina haja ya kulieleza Bunge hili kuonyesha Mkoloni alipoondoka katika Nchi zetu, Wananchi aliwaachia maendeleo ya namna gani katika masuala ya uzalishaji mali kama vile Kilimo, Ufugaji, Uvuvi, n.k. Sina haja ya kuwaeleza hali ya Elimu tuliyoachiwa ilikuwa ya aina gani. Kwa mfano, Shule za Msingi, Sekondari na Vyuo Vikuu vilivyokuwepo wakati huo.

Lakini pia hata kama ningefanya hivyo, kwenye Sekta ya Afya tungeulizana walituachia Zahanati ngapi? Vituo vya Afya vingapi? Hospitali za Wilaya ngapi? Hospitali za Mikoa na Hospitali za Rufaa ngapi? Hata Madaktari waliokuwepo wakati huo kwa kulinganisha na idadi ya Wakazi waliokuwepo walikuwa Wangapi?

Ni kweli kwamba leo tunalaumiwa kwa kutokusaidia kukuza Sekta ya Maji. Lakini yafaa tuulizane, Mkoloni wakati anaondoka aliiacha sekta ya maji katika hali gani? TUULIZANE! Tulirithi Visima vingapi vya Maji, tulirithi Miradi mingapi ya kupeleka Maji katika Miji yetu? TUULIZANE!

Taifa letu leo lina Watu takriban Milioni 42 kwa Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar Milioni 1.3. Mwaka 1964 wakati tunapata Muungano wa Nchi hizi mbili Tanganyika ilikuwa na Watu Milioni 12; na Zanzibar Watu Laki Tatu (300,000). Ni dhahiri kuwa tumeongezeka na hivyo matumizi yetu nayo yameongezeka.

Pamoja na ongezeko kubwa kiasi hicho, Serikali haijapuuza hata kidogo wajibu wake wa kuwapatia Wananchi maji safi na salama. Vijiji vingi sasa vinapata huduma hiyo kupitia visima vilivyochimbwa na kuwekewa pampu au njia nyingine kutoka kwenye Vyanzo vilivyo karibu. Tunaambiwa kwamba hali ya upatikanaji Maji hivi sasa Mijini ni Asilimia 80.3 na Vijijini ni Asilimia 58.3. Juhudi za Serikali kuhusu sekta ya maji zinaonekana sehemu mbalimbali ikiwemo kukamilisha mradi mkubwa wa Maji kutoka Ziwa Viktoria kwenda Shinyanga uliogharamiwa kwa fedha za ndani kiasi cha Shilingi Bilioni 260.

Kauli liyotolewa na Waziri wa Maji hapa Bungeni imeonyesha mikakati mingi mbalimbali inayochukuliwa na Serikali katika kuboresha sekta aya maji Nchini. Hivyo, Serikali imedhamiria kwa dhati kutekeleza ahadi zake kwa umakini mkubwa.

Mheshmiwa Spika,
Kwenye Sekta ya Elimu, hivi Wanafunzi waliokuwa wanakwenda Shule walikuwa wangapi? Je, kulikuwa na Sekondari ngapi? Na Vyuo Vikuu vingapi?

Leo tuna Shule za Msingi 15,816 hapa Nchini. Vijiji karibu vyote vipatavyo 11,812 vina shule za msingi. Wakati wa Uhuru kulikuwa na Wanafunzi 486,470 wa shule za msingi na kufikia mwaka 2010 kulikuwa na jumla ya Wananfunzi 8,419,305, sawa na ongezeko la asilimia 1,700. Aidha, kila mtoto mwenye umri wa kwenda Shule, leo anakwenda Shule. Umoja wa Mataifa umeona na kuridhika kabisa na jitihada za Serikali za kuandikisha watoto waliofikisha umri wa kwenda shule ya msingi. Hali hii ilipelekea mwaka jana Tanzania kupewa Tuzo kwa jitihada za kutekeleza Lengo la Pili la Malengo ya Milenia ya Umoja wa Mataifa. Hii ni heshima kubwa ya kujivunia.
Vilevile, tunazo Shule za Sekondari 4,237 katika Kata 3,338 hapa Nchini. Wakati wa Uhuru kulikuwa na Wanafunzi 11,832 wa Sekondari na hadi kufikia mwaka 2010 kulikuwa na Wanafunzi 1,638,699, sawa na ongezeko la asilimia 13,850.

Wakati wa Uhuru kilikuwepo Chuo Kikuu Kimoja. Leo tunajivuna tunavyo Vyuo Vikuu pamoja na Vyuo Vikuu Vishiriki 32.

Mheshimiwa Spika,
Kwa Upande wa sekta ya Afya, lengo ni kuwa na zahanati moja kila Kijiji, na zahanati zilizopo hivi sasa ni 4,717 Nchi nzima. Tunayo dhamira ya kweli ya kujenga Vituo vya Afya katika kila Kata. Hadi sasa tunavyo Vituo vya Afya 534. Aidha, kati ya Wilaya 114 zilizopo kwa sasa, tunazo hospitali za Wilaya 57. Kwa Wilaya ambazo hazina hospitali za Wilaya, Serikali imeweka utaratibu wa kuwa na Hospitali Teule ambazo hadi sasa zipo 18.
Mikoa karibu yote ina Hospitali za Mikoa isipokuwa katika Mikoa mipya. Sasa tunazo Hospitali za Rufaa Kanda ya Kaskazini KCMC, Kanda ya Ziwa Bugando na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Hospitali ya Rufaa ya Mbeya. Bado Kanda ya Kusini na Kanda ya Kati ambapo juhudi za kujenga zinaendelea.

Vilevile, tunayo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambayo ina Vitengo mbalimbali muhimu vinavyotoa huduma kwa Wananchi.

Mheshimiwa Spika,
Sijui Mkoloni alipoondoka hali yaumeme nchini ilikuwa je? Wale wenye umri mkubwa waliokuwepo wakati huo, wanaweza kujibu swali hili.

Kuhusu hali ya umeme pamoja na matatizo yake yote, Serikali imefanya jitihada kubwa za kuwezesha upatikanaji wa umeme angalau kwa kiwango tunachopata leo. Juhudi za kuongeza kasi ya upatikanaji wa umeme zipo na zimeelezwa vizuri na Waziri anayehusika. Serikali inatekeleza Miradi mbalimbali ya Muda Mfupi, wa Kati na Muda Mrefu ili kuimarisha uzalishaji wa umeme Nchini kwa kushirikiana na Sekta Binafsi.

Serikali pia inaendelea kupeleka na kusambaza umeme katika Makao Makuu ya Mikoa, Wilaya na Vijiji mbalimbali. Baadhi ya Miradi inayoendelea kutekelezwa hivi sasa ni ile inayogharimiwa na Mfuko wa Changamoto za Milenia (Millenium Challenge Account), JICA, Tanzania Energy Development and Expansion Project, Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika.

Aidha, kupitia Bajeti ya mwaka 2010/2011, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) unaendelea kutekeleza Miradi ya kupeleka umeme katika Makao Makuu ya Wilaya za Ngorongoro, Kibondo na Kasulu na maeneo mengine ya Vijiji katika Wilaya mbalimbali Nchini.
Vilevile, Serikali kupitia Wakala huo, inatayarisha Mkakati Kabambe wa kupeleka umeme Vijijini na kuimarisha Mfuko wa Nishati Vijijini. Lengo ni kukamilisha upelekaji wa Umeme kwenye Mikoa na Wilaya ambako Gridi ya Taifa haijafika na kujipanga vizuri katika kuongeza kasi ya kukuza uchumi wa Mwananchi mmoja mmoja na kuondoa umaskini, hasa katika maeneo ya Vijijini kwa kuwapelekea umeme hatua kwa hatua.

Mheshimiwa Spika,
Mwaka 1961, mimi nilikuwa na Miaka 13. Waliokuwa na umri mkubwa kuliko mimi, wanaweza kueleza vizuri zaidi. Kwa wakati huo nakumbuka, njia ya usafiri iliyokuwa na uhakika katika Nchi yetu ni Watu kutembea kwa miguu, tena kwa kupita katika barabara zisizo za uhakika. Hakukuwepo na barabara za lami, changarawe na hata za udongo tu.

Tumepiga hatua kubwa katika ujenzi wa barabara. Karibu Mikoa yote sasa imeshaunganishwa na barabara za lami isipokuwa Mikoa minne ambayo ni Rukwa, Kigoma, Tabora na Manyara. Utekelezaji wa miaradi ya ujenzi wa barabara za kuunganisha Mikoa hiyo ipo katika hatua mbalimbali za upembuzi yakinifu, usanifu wa kina ama ujenzi kwa kiwango cha lami. Hivi sasa, barabara zenye urefu wa Kilomita zipatazo 5,626 tayari zimejengwa kwa kiwango cha lami, kati ya barabara zenye urefu wa Kilometa 12,809 za Barabara Kuu Nchini.

Wapo baadhi ya Wabunge katika kuimarisha uono wao kuwa hakuna kilichofanyika hasa na Serikali ya Awamu ya Nne wamethubutu kusema kuwa Awamu hii haina Mradi wowote wa Barabara.

Mheshimiwa Spika,
Napenda kueleza kuwa katika Ilani za Uchaguzi za CCM zilizotangulia pamoja na ile ya 2005/2010 na hii ya mwaka 2010/2015, zimetilia mkazo kwa Serikali kuendelea kuweka kipaumbele cha juu cha uwekezaji katika Miundombinu, hususan ya Barabara. Serikali za Awamu ya Tatu na Awamu ya Nne zimeendelea kutambua umuhimu wa Barabara nzuri kama kichocheo cha Ukuaji wa Uchumi na Kupunguza Umaskini.

Hadi kufikia mwaka 2000, kati ya Barabara Kuu zenye urefu wa Jumla ya Kilometa 12,809, kulikuwa na Kilometa 3,904 tu za lami. Kutokana na Jitihada za Serikali katika Awamu ya Tatu na Nne, jumla ya Kilomita 1,722 za barabara mpya za lami (upgrading from gravel to bituminous roads) zimejengwa kati ya mwaka 2000 na mwezi Mwezi Desemba 2010 na kufanya Barabara Kuu ambazo zimejengwa kwa kiwango cha lami kufikia jumla ya Kilomita 5,626.

Katika Serikali ya Awamu ya Tatu, Miradi 14 yenye jumla ya Kilometa 1,226 ilianzishwa. Kati ya Miradi hiyo, iliyokamilika katika kipindi hicho ni saba (7) yenye jumla ya urefu wa Kilomita 403. Hivyo, Serikali ya Awamu ya Nne ilipoingia madarakani ilirithi Miradi saba (7) yenye urefu wa jumla ya Kilometa 823 ambayo yote imekamilika hivi sasa.

Katika Serikali ya Awamu ya Nne Miradi mipya 27 ya ujenzi wa Barabara yenye urefu wa Kilometa 1,745 ilianzishwa. Kati ya Miradi hiyo jumla ya Kilometa 392 zimekamilika kwa kiwango cha lami hadi kufikia mwezi Desemba 2010, na jumla ya Kilometa 1,353 zilizobaki zinaendelea kutekelezwa katika hatua mbalimbali. Aidha, sambamba na Miradi hiyo, Serikali imefanya ukarabati mkubwa wa Barabara za lami zenye jumla ya Kilometa 592 kati ya mwaka 2005 na mwaka 2010.

Mheshimiwa Spika,
Ni ukweli uliowazi kwamba maendeleo ya ujenzi wa barabara yamepunguza kwa kiasi kikubwa kero iliyokuwepo ya usafiri wa Barabara Nchini. Sambamba na hatua hizo za ujenzi wa barabara mpya kwa kiwango cha lami, Serikali ya Awamu ya Nne imeendelea kuzingatia umuhimu wa kuimarisha mtandao wa barabara zote Nchini kwa kufanya matengenezo kwa viwango vinavyotakiwa kwa kuongeza Bajeti ya Matengenezo ya Barabara kupitia Mfuko wa Barabara.

Mheshimiwa Spika,
Lengo la Serikali ni kuunganisha Miji Mikuu ya Mikoa kwa Barabara za lami na Makao Makuu ya Wilaya zote Nchini kwa Barabara za changarawe ifikapo mwaka 2018, kulingana na Mpango Kabambe wa Uwekezaji katika Sekta ya Usafiri na Usafirishaji wa mwaka 2007. Hatua hizo zitachochea sana uzalishaji wa mazao ya kilimo nchini na hivyo kukuza Uchumi wa Nchi yetu na kupunguza umaskini kwa kiwango kikubwa.

Mheshimiwa Spika,
Maendeleo ni HATUA moja kwenda nyingine. Sina haja ya kuendelea kutoa mlolongo wa mambo ambayo ninaweza kuyatolea ulinganisho. Lakini inatosha kusema Waheshimiwa Wabunge, Ndugu Watanzania, Taifa hili limejitahidi na ndiyo maana leo tupo hapa.

Tumepita katika hatua nyingi mbalimbali na ndefu. Niwakumbushe tu kwamba miaka ya 80 ilikuwa ni jambo la kawaida kwa Watanzania na hasa wa Mijini kupata bidhaa zao kwa mgao. Watu tulilazimika kupanga foleni kwa ajili ya kupata robo kilo ya sukari, kipande au mche wa sabuni; na mara nyingi Wananchi walipaswa kuwa na daftari la kutunza kumbukumbu za mgao anaopata. Ilifika mahali hata kupata Soda au Bia mpaka upate kibali maalumu. Leo hapa yote yamesahaulika.

Mheshimiwa Spika,
Tumeweza kufanya haya kama nilivyotangulia kusema kwa kuwa kipindi chote tumekuwa ni WAMOJA. Ndiyo maana Mataifa Rafiki nao wameendelea kuunga mkono juhudi zetu. Kama Taifa, tumejitahidi sana kujenga Uchumi Imara, licha ya mitikisiko mbalimbali ya Uchumi tuliyoipitia.

Kuimarika kwa Uchumi kumetuwezesha vilevile, kupata mapato ya kutosha. Rais wa Awamu ya Tatu, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa wakati anachukua Madaraka mwaka 1995, uwezo wa Serikali wa kukusanya Mapato yake ulikuwa hauzidi Shilingi Bilioni 25 kwa wastani wa kila mwezi.

Wakati Rais wa Awamu ya Tatu anakabidhi Madaraka kwa Rais wa Awamu ya Nne mwaka 2005, makusanyo yetu ya Mapato ya ndani kwa mwezi yalifikia wastani wa Shilingi Bilioni 150. Hii ni sawa na ongezeko la Shilingi Bilioni 125 kwa kipindi cha miaka 10. Leo Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Awamu ya Nne amewezesha Taifa hili kupata Mapato ya ndani ya wastani wa Shilingi Bilioni 400 kila mwezi. Hii ni sawa na ongezeko la Shilingi Bilioni 275 katika kipindi cha miaka mitano. Mwezi Desemba 2010, mapato yalifikia Shilingi Bilioni 587. Hiki ni kielelezo cha kutosha kwa Watanzania kujivuna kwamba juhudi zimefanyika.

Mheshimiwa Spika,

Kama alivyokwisheleza Waziri wa Fedha, tumepata mafanikio mengi katika kutekeleza Sera za Uchumi Jumla. Mafanikio hayo, ni pamoja na:

  • Uchumi wa Nchi yetu unaendelea kuimarika licha ya athari za msukosuko wa uchumi duniani, kupanda kwa bei ya mafuata katika soko la dunia na uhaba wa mvua katika baadhi ya maeneo nchini. Katika Kipindi cha mwaka 2005-2010 Pato la Taifa lilikua kwa wastani wa Asilimia 6.9 kwa mwaka ikilinganishwa na miaka ya nyuma ambapo ukuwaji ulikuwa chini ya asilimia tano;

  • Matarajio katika mwaka 2010 ni kwamba kiwango cha ukuaji wa Pato halisi la Taifa kiatafikia Asilimia 7. Changamoto kubwa tuliyonayo ni kuhakikisha kuwa ukuaji huo wa Uchumi unaboresha hali ya maisha ya Watanzania wengi pamoja na kuchangia kwa kiasi kikubwa kupunguza umaskini kwa Wananchi wettu ambao wengni huishi Vijijini;

  • Akiba ya fedha za kigeni imeimarika sana. Hadi Desemba 2010, Nchi yetu ilikuwa na Akiba ya Dola za Marakani Milioni 3,980 ambazo ni sawa na Miezi 6.5 ya kuagiza bidhaa na huduma kutoka Nje ya Nchi ikilinganishwa na miezi 4.8 mwaka 2005;

  • Wadau wetu wa Maendeleo wanaendelea kutuunga mkono katika kuongeza na kutimiza ahadi zao za Misaada na Mikopo kwa Tanzania. Jumla ya Misaada na Mikopo ya Kibajeti (General Budget Support-GBS), Mifuko ya Kisekta (Sector Baskets) na Miradi ya Maendeleo ilifikia Shilingi Trilioni 2.4 mwaka 2009/2010 kutoka Shilingi Trilioni 1.37 mwaka 2005/2006; sawa na ongezeko la Asilimia 57. Hii inatokana na usimamizi imara na utawala bora unaosimamiwa na Serikali ya CCM; na

Viashiria hivi vinaonyesha kuwa Watanzania kupitia Vyama vyao, Viongozi wake na Serikali yao, wamekuwa mstari wa mbele katika jitihada za kuwaletea Watanzania maendeleo.

Serikali itaendelea kuchukua hatua za makusudi za kuimarisha Uchumi na kutekeleza sera zinazochochea kuondoa Umaskini na kukua kwa uchumi. Serikali inatambua kuwa zaidi ya Asilimia 80 ya Watanzania wanaishi Vijijini wakitegemea Kilimo. Kwa kuwa kasi ya ukuaji wa kilimo imekuwa ndogo ikilinganishwa na ongezeko la Idadi ya Watu, Serikali ya Awamu ya nne imeweka mkazo kupitia Azma ya KILIMO KWANZA ili kuboresha sekta ya kilimo. Serikali imejipanga kuleta mabadiliko katika kilimo ikiwa ni pamoja na kuanzisha Benki ya Maendelea ya Kilimo, kuwekeza katika miundombinu ya Umwagiliaji na kuanzisha Kongano (Clusters) zenye lengo la kuleta msukumo wa ukuaji katika sekta ya kilimo (Kilimo Kwanza Growth Corridors);

Mheshimiwa Spika,
Kabla ya kuhitimisha napenda kueleza kuwa, Hotuba ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa wakati akizindua Bunge hili la Kumi, imezingatia na inaendana na ahadi za Serikali ya Awamu ya Nne ambazo zipo katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010, MKUKUTA II, Utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya hadi mwaka 2025.

Kwa mantiki hiyo, ushauri uliotolewa na Waheshimiwa Wabunge hapa utasaidia sana Serikali katika kutekeleza na kufikia malengo ya Mipango hiyo. Aidha, Michango hii ya Wabunge itatusaidia sana katika kupanga vizuri vipaumbele vya Bajeti ya Serikali ya mwaka ujao ili vitoe ufumbuzi wa changamoto zinazolikabili Taifa kwa sasa na pia kutatua kero mbalimbali za Wananchi.

Kwa hivyo tunawaomba Waheshimiwa Wabunge wote tumuunge mkono Mheshimiwa Rais katika kutekeleza mipango yetu ya maendeleo kwa maslahi na ustawi wa Wananchi wetu.

4.0 MIGOMO VYUONI NA MAANDAMANO

Mheshimiwa Spika,
Siku za hivi karibuni pamekuwepo na migomo na maandamano kwenye Vyuo Vikuu mbalimbali vya Umma na vile vya Binafsi Nchini. Migomo hii ambayo imehusisha Wanafunzi na katika Vyuo vingine Wahadhiri imetokea kwenye zaidi ya Vyuo 17 vya Elimu ya Juu hapa Nchini.

Sababu za Migomo

Mheshimiwa Spika,
Sababu za Wanafunzi kugoma zimeelezewa kuwa ni kutoridhika na utoaji mikopo kwa Wanafunzi; baadhi ya Programu kutokuwa na mafunzo kwa vitendo; Wanafunzi kuishi kwenye mazingira yasiyoridhisha ya kusomea na baadhi ya Vyuo kudahili Wanafunzi kwenye Programu ambazo hazijaidhinishwa na Tume ya Vyuo Vikuu na hivyo kukosa mikopo. Zipo pia sababu za Vyuo kutoza ada kubwa au kupandisha ada kwa kiasi kikubwa na katika baadhi ya Vyuo, Wanafunzi kutaka Serikali iongeze posho ya chakula na malazi kutoka Sh. 5,000/= ya sasa kwa siku na kufikia Sh. 10,000/=. Aidha, zipo sababu za kiutawala ambapo Wanafunzi wameonyesha kutoridhika na uongozi wa Menejimenti za baadhi ya Vyuo.

Migomo hii imesababisha vurugu Vyuoni na hivyo kuvuruga Ratiba za Masomo na amani kwa ujumla. Vilevile, kutokana na vurugu hizo, muda mwingi unapotea katika kushughulikia ufumbuzi wa migomo kwa upande wa Vyuo na Serikali.

Hatua Zilizochukuliwa
Mheshimiwa Spika,
Sababu ambayo inajitokeza katika kila mgomo ni kuhusu utoaji wa mikopo ya elimu ya juu. Hata hivyo, kumekuwa na juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali kutafuta ufumbuzi wa suala hili la mikopo.

Itakumbukwa kuwa Serikali iliweka sera ya uchangiaji katika elimu ya juu mwanzoni mwa miaka ya 1990. Ili kuwawezesha wanafunzi ambao wengi walikuwa hawana uwezo wa kuchangia kiasi kilichotakiwa kutokana na vyanzo vyao vya mapato, Serikali iliweka utaratibu wa kutoa mikopo kwa wanafunzi hao. Mikopo hiyo ilikuwa inatolewa na Serikali kupitia Wizara iliyokuwa na dhamana ya elimu na ilikuwa inatolewa kwa asilimia 100 katika maeneo ya chakula, malazi, vitabu, viandikwa, utafiti, ada ya mafunzo, mahitaji maalum ya vitivo na mafunzo kwa vitendo.

Mwaka 2004 ilianzishwa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ili kusimamia suala zima la utoaji na ukusanyaji wa mikopo. Bodi hiyo ilianza kazi rasmi mwezi Julai 2005. Kwa mwaka wa masomo 2005/2006, Bodi ilitoa mikopo kwa maeneo yote niliyoyataja hapo juu kwa asilimi 100. Mwaka uliofuata wa 2006/2007, Bodi ilitoa mikopo kwa asilimia 100 kwa maeneo ya chakula, malazi, utafiti, vitabu na viandikwa. Aidha, ilitoa mikopo ya asilimia 60 ya mahitaji ya gharama za ada ya mafunzo, mahitaji maalum ya vitivo na mafunzo kwa vitendo kwa kila mwanafunzi. Hivyo, mwanafunzi alichangia asilimia 40 katika kugharimia maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika,
Katika mwaka 2007/2008 na 2008/2009, utoaji wa mikopo kwa baadhi ya maeneo ya gharama ilitolewa kwa kuzingatia matokeo ya means testing ambapo wanafunzi walitengwa katika madaraja 6 ya A mpaka F ya asilimia 100 hadi 0. Aidha, kuanzia mwaka 2009/2010, madaraja hayo yaliongezeka kutoka sita hadi 11, (kutoka A mpaka K).
Maeneo yaliyozingatia matokeo ya Means Testing ni:
(i) Ada ya mafunzo;
(ii) Mahitaji Maalumu ya kitivo; na
(iii) Mafunzo kwa vitendo (Sh. 10,000 kwa siku kwa siku zisizozidi 56 kwa mwaka).
Madaraja hayo yalizingatia historia ya elimu ya mwombaji, kiwango cha elimu ya wazazi/mlezi, Shughuli za kiuchumi za mwombaji na mzazi/mlezi, mali za muombaji na mzazi/mlezi na mahali zilipo, hadhi ya maisha yake na ya wazazi/walezi wake kijamii, hali ya kijamii ya mwombaji (uyatima na ulemavu).
Wanafunzi waliopewa kipaumbele ni Wanafunzi waliofaulu vizuri zaidi kwa kiwango cha daraja I na II katika mitihani ya kidato cha sita. Aidha, Wanafunzi wote wanaosomea masomo ya Sayansi; (afya za binadamu na wanyama, kozi za Uhandisi, Kilimo n.k); Ualimu na wale waliopelekwa kusoma nje ya nchi chini ya makubaliano kati ya serikali yetu na serikali zingine wamekuwa wanapewa pia kipaumbele.

Hivyo, kutokana na sifa hizo, wanafunzi walichangia gharama za mahitaji hayo kwa viwango mbalimbali kati ya asilimia 0 hadi 100.

Maeneo ya ukopeshaji yafuatayo yaliendelea kupata mikopo kwa asilimia 100:
(i) Chakula na Malazi (kwa sasa ni kiasi cha Sh. 5,000 kwa mwanafunzi kwa siku, kwa idadi ya siku atakazokaa chuoni);
(ii) Vitabu na Viandikwa (kwa sasa ni Sh. 200,000 kwa mwanafunzi kwa mwaka); na
(iii) Utafiti (kwa sasa ni Sh. 100,000 kwa mwanafunzi kwa mwaka.

Takwimu za ongezeko la wanafunzi waliokopeshwa na kiasi cha fedha kwa kipindi cha 2004/2005na 2009/2010 zinaonyeshwa kama ifutavyo:

Jedwali Na. 1: Takwimu za Utoaji Mikopo kuanzia 2004/2005 hadi 2009/2010
Mwaka
Idadi ya Wanafunzi Walio-kopeshwa
Ongezeko
(%)
Kiasi kilichoko-peshwa
(Tshs Bilioni)
Ongezeko
(%)
2004/05 (Na Wizara)
16,345
-
9.9
-
2005/2006
42,729
161.4
56.1
467
2006/2007
47,554
11.3
76.1
35.7
2007/2008
55,687
17.1
110.8
45.6
2008/2009
58,798
5.6
139.0
25.5
2009/2010
72,035
22.5


2010/2011 (Matarajio)
85,319
18.4
237.8
28.7
Wastani wa Ongezeko
39.4
105.9


Kwa ujumla takwimu hizo zinaonyesha kwamba, katika kipindi cha miaka mitano cha 2005/2006 hadi 2009/2010 iliyopita, idadi ya waliokopeshwa imeongezeka kwa asilimia 100. Muhimu zaidi ni kuwa ongezeko hilo limekuwa linakua mwaka hadi mwaka kutoka mwaka 2006/2007 (asilimia 11) hadi mwaka 2009/2010 (asilimia 22). Hivyo, ni wazi kuwa kutoa mikopo kwa madaraja kumeongeza uwezo wa Serikali kutoa mikopo kwa wanafunzi wengi zaidi. Aidha, katika kipindi hicho, fedha zilizokopeshwa nazo zimeongezeka kutoka Shilingi bilioni 56.1 mwaka 2005/2006 hadi shilingi Bilioni 184.7 mwaka 2009/2010, sawa na ongezeko la asilimia 229.

Mheshimiwa Spika,
Kwa ujumla Serikali imekuwa ikijitahidi kuwawezesha wanafunzi wengi kupata mikopo kulingana na vigezo vilivyowekwa vya means testing. Hata hivyo, bado kuna mapungufu katika suala zima la viwango na mfumo wa utoaji mikopo yanayosababisha malalamiko mbalimbali kutoka kwa wadau na wakati mwingine kusababisha migomo.

Katika kutatua suala la migomo,kumekuwepo na Mikutano kadhaa iliyohusisha Serikali, Menejimenti za Vyuo na Viongozi wa Wanafunzi, Wahadhiri na hata wakati mwingine kuzungumza na Wanafunzi wote ili kutafuta suluhisho ya madai yao. Serikali pia imekuwa inatoa taarifa kwa Umma kupitia Vyombo vya Habari kuhusu kiini cha migomo hii na hatua mbalimbali zinazochukuliwa.

Hatua za hivi karibuni ni pamoja na Mheshimiwa Rais kuunda Tume ambayo itatoa mapendekezo ya viwango vya mikopo vinavyolingana na hali ya sasa ya uchumi na kushauri namna bora ya kutoa na kurejesha mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu. Tume hii imeshaanza kazi na inatarajia kutoa ripoti yake kabla ya tarehe 15 Aprili 2011. Aidha, Serikali imeiagiza Tume ya Vyuo Vikuu kuyashughulikia madai yanayohusu Taaluma ili Wanafunzi waweze kusoma bila matatizo. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ameanza kufanya Ukaguzi wa Hesabu za Vyuo ili kuishauri Serikali namna ya kuondoa malalamiko yanayohusu fedha.

Sheria za Migomo Vyuoni

Mheshimiwa Spika,
Napenda kurudia kuwakumbusha wanajumuiya wa Vyuo Vikuu kuwa, Chini ya Hati Idhini za Vyuo (Charters) na Sheria Ndogo za Wanafunzi, migomo hairuhusiwi Vyuoni. Sheria Ndogo za Wanafunzi pia zinatamka kuwa kama Wanafunzi watagoma kuingia Darasani kwa siku tatu mfululizo, Mkuu wa Chuo anaweza kuwafukuza au kufunga Chuo. Hivyo, migomo katika vyuo vikuu ni kinyume cha sheria.

Mheshimiwa Spika,
Wanafunzi pia, wakati mwingine hufanya maandamano katika kujaribu kwasilisha hoja zao kwa viongozi wa Vyuo na Serikali na pengine bila hata kuwa wamechukua hatua zozote za kuwasilisha malalamiko yao rasmi kwa ngazi zinazohusika.

Wakati suala zima la Migomo na maandamano linafanyiwa kazi, Wito wangu kwa Wanavyuo wote ni kwamba, kudai haki kwa njia ya migomo au maandamano bado sio utaratibu mzuri, kwani athari zake ni kubwa. Nawashauri Wanavyuo, Wahadhiri na Wafanyakazi wote kutumia njia ya majadiliano zaidi hadi kufikia muafaka.

Serikali wakati wote imekuwa sikivu na itaendelea kuwa sikivu ili kudumisha amani na umoja Nchini. Serikali iko tayari kupokea, kujadili, kuchambua na kufanyia kazi ushauri wowote unaotolewa kwake kwa maslahi ya Watanzania. Milango iko wazi na yeyote mwenye wazo, ushauri, hoja, na kero anakaribishwa.

5.0 HITIMISHO

Mheshimiwa Spika,
Nimeona nieleze haya kama njia ya kuwaomba Waheshimiwa Wabunge wenzangu, Vyama vyote vya Siasa na Wananchi wote kutambua kwamba si busara kubeza juhudi zenu ambazo zimesaidia kuwafikisha hapa. Nawaomba Tuungane. Naliomba Bunge lako Tukufu lisaidie kutuunganisha katika juhudi za kuwaletea Watanzania maendeleo.

Michango yenu chanya ya mawazo hapa Bungeni na nje ya Bunge ndiyo kielelezo cha Watanzania walio chini ya msingi muhimu wa Umoja wa Kitaifa.

Wote, tujiepushe na jambo lolote lenye lengo la kurudisha juhudi hizi nyuma kwa kudhani kwamba zitatuwezesha kushika Madaraka. Kwani kama kwa kufanya hivyo na ukaweza kweli kushika Madaraka kwa njia ambazo si za amani na utulivu, kazi ya kujenga amani na utulivu itawachukua miaka mingi ambayo ingeweza kutumika kusukuma mbele maendeleo.

Mheshimiwa Spika,
Nimalizie kwa kukupongeza kwa kuchaguliwa kwako kuwa Spika wa Bunge letu hili pamoja na Naibu Spika wako, Mheshimiwa Job Augustino Ndugai (Mb.),pamoja na Wenyeviti wa Kamati zote za Kudumu za Bunge.

Naomba niwapongeze kwa dhati Waheshimiwa Wabunge wenzangu wote kwa kuchaguliwa na kupewa dhamana kwa kuwakilisha katika Bunge letu hili.

Kwa namna ya pekee, niwapongeze Kambi ya Upinzani chini Kiongozi wake Mheshimiwa Freeman Mbowe kwa kuchaguliwa kwenu na Watanzania. Tukumbuke kwamba sisi ndiyo mboni ya jicho la Watanzania wetu waliotuchagua.
Tunayoyafanya Bungeni yawe kwa maslahi ya Wananchi wetu wote. Na hivyo katika kutekeleza jukumu hili, ninyi mliopo upande wa Upinzani, ninawasihi sana USHIRIKIANO, kwani ninyi wote mko katika Kambi moja ya Upinzani, na ni Watanzania.

Kwa upande mwingine, nawasihi sana Waheshimiwa Wabunge wenzangu wa Chama Cha Mapinduzi tufanye kazi kwa karibu sana. Tujitahidi kuondoa tofauti zetu zote kwa maslahi ya Watanzania. Na kwa kuwa sisi Wabunge wa Bunge hili wote ni Watanzania, basi hatuna budi kufanya juhudi za dhati za kupendana, kushirikiana na kusaidiana kwa maslahi ya Watu wetu.

Mheshimiwa Spika na
Waheshimiwa Wabunge,

Nawashukuru sana kwa kunisikiliza na naomba kutoa HOJA.