Adverts

Feb 7, 2011

JK Aunda Tume Kutayarisha Mfumo Mpya Wa Mikopo Elimu Ya Juu

JK Aunda Tume Kutayarisha Mfumo Mpya Wa Mikopo Elimu Ya Juu: " TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU UTEUZI WA TUME YA KUTAYARISHA MFUMO MPYA WA KUGHARIMIA/KUTOA MIKOPO KWA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU Katika hotuba yake ya kukizindua rasmi Chuo Kikuu cha Dodoma Novemba 25, 2010, Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete aliahidi mambo makubwa mawili kama ifuatavyo, nanukuu: Moja: “Kuhusu mikopo ya elimu ya juu napenda kuwahakikishia wazazi na wanafunzi kuwa tutaendelea kuongeza fedha katika mfuko huo ili wanafunzi wengi zaidi wanufaike. Tumefanya hivyo katika miaka mitano iliyopita na tutafanya hivyo siku za usoni. Serikali iliongeza fedha za mikopo kutoka shilingi bilioni 56.1 mwaka 2005/06 hadi kuwa shilingi 237 bilioni mwaka 2010/11 na wanafunzi waliopatiwa mikopo hiyo wameongezeka kutoka 16,345 hadi 69,921. Haya ni mafanikio makubwa na naahidi kuwa tutafanya vizuri zaidi ili tuwafikie wanafunzi wengi zaidi; na Pili: Pia tutautazama upya mfumo mzima wa utoaji wa mikopo ikiwepo na utendaji kazi wa Bodi ya Mikopo kwa nia ya kuuboresha na kuleta ufanisi zaidi. Mawazo ya wadau wakiwemo wamiliki wa vyuo, wahadhiri na wanafunzi, yatasaidia sana”. Ili kutekeleza ahadi hiyo ya Pili, Mheshimiwa Rais ameteua Tume ya wataalam 11 kufanya mapitio ya mfumo na uendeshaji wa Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu nchini kwa lengo la kuimarisha utoaji wa mikopo hiyo. Tume inatakiwa kufanyakazi kwa siku 60, kuanzia tarehe 14 Februari 2011 na kuwasilisha ripoti yake kwa Katibu Mkuu Kiongozi tarehe 15 Aprili 2011. Tume hiyo itaongozwa na Makamu Mkuu wa Chuo (Taaluma) Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Makenya Abraham Maboko. Wajumbe wengine wa Tume hiyo ni Bw. Masoud Mohamed Haji, Ofisa Uhusiano wa Kimataifa, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Zanzibar; na Dkt. Eliawony Kristosia Meena, Mhadhiri Mwandamizi (Elimu), Chuo Kikuu cha Tumaini Arusha. Wengine ni Bw. Daniel Paul Magwiza, Naibu Katibu, Tume ya Vyuo Vikuu; Bibi Sarah K. Baharamoka, Mkurugenzi Msaidizi (Uandishi Sheria), Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Profesa Penina M. Mlama, Mkurugenzi Mtendaji wa Tawi la Tanzania la Taasisi inayopigania Elimu kwa Wanawake (Campign for Female Education Tanzania Chapter). Katika Tume hiyo pia yumo Bw. Deo Mbasa Daudi, Ofisa Taaluma, Chuo cha Usimamizi wa Fedha, ambaye ni Rais Mstaafu wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam-DARUSO (2007/2008), na Katibu Mkuu Mstaafu wa DARUSO (2006/2007); Bw. Kassim Almasi Umba, Makamu Mkuu wa Chuo (Utawala na Fedha), Chuo Kikuu cha Kiislamu, Morogoro; Bw. Anderson Y. Mlambwa, Mkurugenzi wa Mikopo, Benki ya CRDB; Prof. Wilbert Abel, Mkurugenzi wa Elimu ya Juu, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Bibi Rosemary Rulabuka, Mkurugenzi Mkuu, Mamlaka ya Elimu Tanzania. Tume itateua Makamu Mwenyekiti kutoka miongoni mwa Wajumbe. Sekretarieti ya Tume hiyo itatokana na Wajumbe kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi; Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; na Ikulu. Hadidu za Rejea za Tume hiyo ni pamoja na kuchambua kwa kina Sheria Na. 9 ya mwaka 2004, iliyounda Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu, na Kanuni zake na kubainisha vifungu vinavyohitaji marekebisho kulingana na hali halisi ya utoaji mkopo na kuangalia upya vigezo na sifa zinazozingatiwa katika utoaji wa Mkopo endapo vinakidhi haja na mahitaji halisi ya waombaji na taifa kulingana na makusudio ya kuundwa kwa Bodi ya Mikopo. Nyingine ni kuangalia kwa kina muundo wa Bodi na ufanisi wake katika utoaji na urejeshwaji wa mikopo na kutoa mapendekezo na kuchunguza kiini cha malalamiko na mahusiano yasiyoridhisha kati ya Bodi na Wanafunzi, Bodi na Taasisi ya Elimu ya Juu na kati ya Bodi na Wizara ya Elimu na kutoa mapendekezo ya namna ya kurejesha mahusiano mazuri. Hadidu nyingine za rejea ni kuchambua mfumo mzima wa namna ya kubaini wanafunzi wanaohitaji mikopo (Means Testing) ili kuibua mapungufu yake na kupendekeza taratibu za kuuboresha au kuwa na mfumo mbadala na kuangalia mambo yanayosababisha mifuko mingine kama vile “Resource Endowment Fund” wa Maliasili unafanikiwa na Nchi nyingine zenye mazingira kama ya Tanzania zinavyofanikiwa kugharimia Elimu ya Juu kwa mfumo wa Mikopo. Nyingine ni kutoa ushauri na mapendekezo yatakayowezesha Mkopo utolewe kwa wanafunzi wengi wahitaji wa Elimu ya Juu ili kuondoa lawama zilizopo na kushughulikia mambo mengine yoyote yatakayoweza kuboresha mfumo huo kwa kadri inavyoonekana inafaa. Ni matumaini ya Serikali kwamba baada ya Tume hiyo kukamilisha kazi yake, itatoa ushauri utakaosaidia kujibu malalamiko mbalimbali kuhusu utendaji kazi wa Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu. Mizengo P. Pinda (Mb) WAZIRI MKUU 6 Februari 2011
"