Mei 2009 niliendesha warsha kadhaa Dar es Salaam, zilizoongelea mada mbalimbali; mosi ilikuwa hii pale British Council.
SEMINA 1- Ughaibuni
“HAITOSHI WEWE KULIELEWA, BALI NA WEWE KULIELEZEA NA MTU MWINGINE AKAELEWA…” -Profesa Chachage S. L. Chachage, “Makuadi wa Soko Huria” , 2002.
Usafiri usiotegemea magari unazidi kutakiwa Majuu; upandaji baiskeli unapewa kipaumbele kwa kuwa hauchafui mazingira kwa uchafu wa moshi na petroli. Picha ya mtaa wa Tottenham Court Road, mjini London na F. Macha Vijana na baadhi ya wazalendo leo wanataka kwenda nje kusoma, kufanya kazi au kutembea. Kinachotusukuma kwenda nje ni mseto wa uchumi mbaya, umaskini na kutaka tu kufahamu mambo. Lakini je, hili ni jambo geni? Kutaka kwenda Ulaya, Marekani, Afrika Kusini au Australia hakukuanza leo.
Ari ya kuhama hama ni moja ya nguzo kuu za uhai wetu wanadamu.
• UHAMIAJI UGENINI NI JAMBO LA KAWAIDA
1-Migogoro na Tafrani husababisha uhamiaji: Hakuna kipindi katika historia ya maisha ya wanadamu ambapo wananchi wowote katika nchi yeyote ile duniani hawakuhama ama kwa sababu za kivita, migongano ya mali (ardhi, biashara, nk) au kutafuta tu kazi na maisha bora. Umri wa ulimwengu ni miaka 6,000. Katika kipindi hicho vita mbalimbali zimefanywa na kusababisha watu kuhama. Asilimia 70 ya vita zimetokana na sababu za Kidini, Mbari na Ukabila (1). Mfano mzuri ni jamii ya Marekani yenye wananchi wa aina mbalimbali waliohamia pale ama kwa maguvu (ukoloni), utumwa (watu weusi) kukimbia vita kwao (Wayahudi) au kujaribu tu maisha mapya na ujasiriamali. Mseto huo ndiyo unaoifanya Marekani kuwa jamii ya aina hiyo. Kutokana na hilo Marekani leo inaye Rais chotara : nusu Mwafrika, (Kenya) nusu Mzungu (mama mzawa wa Kansas). Barrack Obama anakiri katika maandishi yake kwamba akiwa kijana ilimbidi aishi katika dunia mbili za weusi na weupe (2). Rais Barack Obama alilelewa na babu na bibi yake upande wa mama mzungu ; wakiishi Hawaii. Akiwa kijana alitembelea Kenya akagundua nini babu na babake walifanya na walikotoka na kuwaona ndugu wengine ndipo akafikia kilele cha mshawasha zaidi wa kujijua. Obama anatufundisha kuwa jambo baya laweza kugeuzwa kuwa zuri. Sio Marekani au Obama pekee. Tanzania yetu inatokana na maingiliano ( mazuri na mabaya) baina ya makabila na watu wa aina mbalimbali. Lugha ya Kiswahili ilizaliwa kutokana na kuhama hama baada ya maingiliano kati ya Waarabu na Waafrika ukiwemo utumwa, vita, dini na biashara (3). 2-Kwenda nje kusoma huchangia uhamaji: Miaka mingi nimeelezea ama maisha ya wanafunzi kama Masudi Pashamoto (aliyehamia Uingereza mwaka 2004). Bwana Masudi alipofika kusoma alikuwa na nidhamu. Alikuwa pia mcheza mpira. Alifanya vizuri. Alipata sifa sana chuoni na kupendwa. Hakuitia aibu familia wala nchi yake. Wanafunzi waliozingirwa na askari, wakiandamana (kwa kukaa chini ) kupinga kuongezeka kwa karo za vyuo vikuu (mara tatu toka Paundi 3,000 kwa mwaka kwenda 9,000) nchini Uingereza, mwaka 2010. Picha ya Reuters 3-Ukitoka nje jua unalotafuta: Masudi alisomeshwa na babu na mama yake. Mamake alipata mimba akiwa shuleni. Babu wa Masudi hakumkana binti wala kumdhihaki alipofukuzwa shule. Alimsaidia; akamlea; akamtunza mjukuu. Binti akapelekwa Nairobi kusoma; akawa sasa mtaalamu wa michezo. Masudi alipoletwa baadaye kusoma Ulaya hakusahau alikotoka. Siri ya kusafiri kwenda nje, kusoma au kutembea ni kujua unakotoka na nini unatafuta. Wanaojisahau hupotea.
4-Sababu zetu za kwenda nje tofauti na za wenzetu: Mara nyingi watu nchi zilizoendelea huenda nje kutembea; kutalii au kufanya tu utafiti. Baadhi huchoshwa na maisha ya kwao; hali ya hewa (baridi ya Majuu) au hata kutokana na mgogoro wa mapenzi. Mfano mzuri ni kisa kilichoelezewa na mwandishi toka Australia, Peter Moore aliyekuja Afrika (ikiwemo Tanzania) baada ya kugombana na mpenzi wake. Hakupoteza muda akaandika kitabu “Swahili for the Broken Hearted” (4).
• KUJA NJE Je kwanini unataka kwenda nje? Je, unajiendea tu kwa kuwa wenzako wameondoka au kwa kuwa umechoka na maisha? Na je baada ya hayo itakuwaje? 1-Fanya utafiti kwanza. Je unataka kwenda nchi gani? Je, ile nchi ikoje? Nenda Maktaba za nchi zao hapa nyumbani. Mathalan kama unataka kwenda Ujerumani nenda Goethe Institute. Soma mambo yao. Kama ni Marekani nenda USIS Library. Kama ni Uingereza nenda British Council. Kama ni Ufaransa nenda Alliance Francaise. Pale mwombe mkutubi yeyote akupe habari za ile nchi. Vijana wengi wanataka kuja nje lakini hawajui wapi wanakwenda; ile nchi inaongea lugha gani; ina utamaduni wa aina gani, nk. 2-Nenda Ubalozi wa ile nchi unayotaka kwenda. Omba habari au chukua tu mafaili na vijarida vinavyoihusu. Waambie unataka tu habari; si kwamba unataka kusafiri huko. 3-Balozi mbalimbali duniani zina tovuti zao. Tumia mtandao kusoma habari za ubalozi. Watakueleza sheria na kanuni za upataji Viza. Haitoshi kutaka tu kuja kama hujajisomea mwenyewe sheria za Viza, utaratibu unaotakiwa nk. Habari zote za Balozi mbalimbali nchini zipo katika tovuti au webu zao. Zisome kwa makini; ikiwezekana chapa hizo habari kabla hujakwenda kuwasumbua. Maofisa mbalimbali wa balozi za nje huwadharau na kuwasakama waomba viza kwakuwa huwa wanachoshwa na maswali na tabia zao; ilhali zile habari zimeshaandikwa katika tovuti. Mwanamuziki mkongwe Dave Marama ( wa pili mwenye gitaa) akipiga mjini Arusha miaka ya 1970. Siku hizi kahamia Australia ambapo anawika na bendi kali yenye mseto wa Waafrika na Waustralia, Public Opinion Afro Orchestra. Ukitaka kuhamia nje lazima uwe na ujuzi na msimamo unaoeleweka kama wa bwana Marama. 4-Soma magazeti ya ile nchi. Katika maktaba mbalimbali za hizo nchi kuna majarida na magazeti. Pia unaweza kupata hizo habari katika mitandao.
2-Watanzania hatuna tabia ya maingiliano na kujuana na wageni (Networking):
Tabia ya kutaka tu kujuana na wale wanaoongea lugha moja na yako, wenye mambo na chakula chako si mbaya. Ila katika dunia ya leo yenye uwezekano mkubwa wa habari na mawasiliano si rahisi kuendelea kama utajikunyata na kutopanua bongo na mikono yako. 1-Fanya urafiki na maingiliano na wageni wanaokuja nchini. Waulize wanatoka wapi, wamekuja kufanya nini, je, unaweza kuwasaidiaje? USIWAOMBE FEDHA. Hakuna kitu kinachowaudhi wageni kama kuwaomba fedha, kuwaambia unawapenda baada ya mazungumzo ya dakika tano. Watanzania tunasifiwa dunia nzima kwa kutopenda kufanya mawasiliano na maingiliano na watu wa mataifa mengine. Tunataka tu kukaa na watu wa kwetu; kula vyakula vya kwetu, kutochanganyikana (networking). Hii tabia imejijenga nje na ndani ya nchi. 2- Tatizo hili la kutopenda (au kutozoea) maingiliano linatokana na kutokuwa na fikra na tabia za kijasiriamali, dhana za kutaka kujiendeleza kutokana na kuongea na usiowajua au usichokijua. Mtaalamu na mhadhiri anaefundisha Uingereza, Dk. Imani Kyaruzi ameyaita maingiliano haya, ushirika wa nguvu na mbinu za biashara. Kitabu cha Dk. Kyaruzi “Mbinu za Ujasiriamali” si tu cha wafanya biashara, bali chakuhusu wewe Mtanzania unayetaka kujiendeleza. Mtanzania huyu anasisitiza kuwa ujasiriamali hujengwa kwa ushirikiano na siyo kwa “vyangu-vyangu.” Wazungu huendelea siku zote kwa hulka hiyo. Anatoa mfano wa milionea waliojenga himaya mathalani Bill Gates na Paul Allen (Microsoft) au Larry Page na Sergey Brin (Google). “Hapa yawezekana kuna masuala y watu kutoaminiana lakini uaminifu hujengwa.” (5). Hakuna kitu kinachothaminiwa nchi tajiri kama elimu. Hapa mdau wa Kitoto naendesha semina ya fasihi na muziki kwa familia na watoto katika maktaba ya Kentish Town, London, Oktoba 2010. Picha na Dianne Smith
3-Nilipitia ya kutojua mambo haya sawasawa pia:
Nakumbuka miaka ya Sabini tulivyokuwa tunapenda Ubaharia. Kazi ya ubaharia ambayo ni ngumu na ya hatari tuliiona mali sana kwa kuwa ilikuwa njia ya kusafiri, ya kupata fedha na kuhamia ughaibuni. Nakumbuka mimi mwenyewe nilivyokuwa tu nas’kia mambo. Nikajaribu hata kujipenyeza katika meli (stoaway) yakanipata makubwa. 1-Nimejaribu kueleza njozi za mchana katika vitabu viwili : “Twenzetu Ulaya” na “Mpe Maneno Yake.” Katika “Mpe Maneno Yake” kipo kisa cha baharia Yusufu Pigalaza akimwandikia barua rafiki yake Bongo, Johnny Nyau. (6) 2-Moja ya sababu zinazotufanya tushindwe kuwa na maingiliano au kutokujua mambo sawasawa ni kutokusoma. Maarifa yetu yanapatikana tu kwa uzushi, njozi na fikra za hapa na pale. 3- Kujifunza lugha mbalimbali ni muhimu. Leo kumezuka kizazi cha watu wasiojua Kiswahili au Kiingereza sawasawa. Kama hufahamu lugha sawasawa utapata shida sana ugenini. Baada ya kujifunza Kiswahili na Kiingereza hasa nikifanya kazi ya uandishi wa habari (Uhuru) nilianza kujifunza Kifaransa mwaka 1978. Kujua Kifaransa kulifungua milango mingi. Niliona sinema za aina nyingine, muziki wa aina nyingine na vitabu tofauti na vya Wamarekani na Waingereza. Nilijenga urafiki na maingiliano na Waafrika toka nchi zinazoongea Ufaransa mathalan Algeria, Congo na Senegal. Ilinisaidia nilipokwenda Marekani ya Kusini zinapoongewa Kispanyola na Kireno. Ujuzi wa Kifaransa ulisaidia kuzijua lugha hizo mbili upesi maana zina mizizi ya aina moja (Kilatino). 4- Lugha hukusaidia kujua nchi, jamii, tamaduni mbalimbali za nchi nyingine. Nikiwa Paraguay na nchi nyingine zisizoongea Kiingereza niliona wageni wengi wakiteseka (kuibiwa, kudanganywa au kudharauliwa) kwa kutojua lugha ya jamii ile. Nimeeleza haya katika Mpe Maneno Yake(7).
“JAMBO LA KWANZA KUZINGATIA KATIKA ELIMU YA KWELI YA MTOTO NI KUANZA KUMPA ELIMU YA KUJITAMBUA YEYE NANI, DUNIA YAKE, UTAMADUNI WAKE, JUMUIYA YAKE…HUO NDIYO MWANZO WA MCHAKATO WOWOTE WA ELIMU…” -Kutoka Dreams of My Father, Barack Obama.
Bango la tangazo la biashara kuhamasisha watalii kuja Kenya, mjini London. Ingawa Wakenya husema Wabongo tunaongea Kiswahili kuwazidi; wao wamekuwa mstari wa mbele miaka mingi kujenga lugha hii kwa mavazi, muziki nk. Picha na F Macha • KWENDA NJE KUSOMA
1-Vijana wengi wanataka kuja kusoma nje wangali sekondari. Kipimo cha masomo kwetu na nchi nyingine hasa za Ulaya na Marekani ni tofauti. Mathalan kama wewe uko kidato cha nne; Uingereza itakuwa inaitwa “O levels.” Ukiwa kidato cha sita huku Uingereza ni A levels. Umri pia unatofautiana. Wazungu huanza shule mapema kutuzidi. Shule za vidudu (chekechea) huisha miaka minne ; ilhali sisi huanzia miaka 6. Wao darasa la kwanza huanzia miaka 5/6. Wastani wao kuingia Sekondari ni miaka 11. 2-Watanzania wengi wanataka kuja kusomea shahada ya kwanza au diploma. Kiserikali ni bora na rahisi zaidi kuomba masomo ya kulipiwa au bure (“scholarship”) baada ya shahada ya kwanza nyumbani. Ubalozi wa Tanzania, Uingereza unashauri ni bora Vijana kuja kusoma Stashahada (masters) badala ya shahada ya kwanza. Unaasa kuangalia vyuo nyumbani zaidi; na kama unazo pesa zako tafuta nyuo vya nchi changa zinazoendelea vyenye unafuu wa bei mathalan, India, Malaysia, Indonesia, Afrika Kusini, Brazil, nk.
3- Kama una pesa zako unaweza kuja kusoma chochote utakacho. Kama huna pesa yakubidi umalizie kwanza shahada au diploma ya kwanza kabla ya kuhangaika na Masters au shahada nyingine. Ukiwa na pesa kuna wakala mbalimbali nyumbani wanaodai fedha kusoma nje. Wakala hawa hujitangaza kwa njia mbalimbali. Wanafunzi wengi wanajua. 4-Kuhusu vyuo na shule kadhaa za kusoma nje. Vijana tumieni Google. Kila chuo siku hizi hujitangaza katika mtandao. Ikiwa unajua unachotaka kuja kusoma tumia Google kutafiti. Mathalan unataka kuja kusoma IT na Computer. Weka maneno hayo katika Google, mji na nchi; kisha bofya; mathalan London International Colleges, India International Colleges, nk Vijana leo mna urahisi wa kupata habari kuliko sisi wa miaka 30 iliyopita. Kila kitu kimo mitandaoni. Unachotakiwa kuwa nacho ni maarifa, kufanya utafiti (kujua unachotaka) na fedha. Ndiyo tunayo matatizo ya umeme, Ndiyo migahawa ya mitandao ni aghali, lakini ukitaka cha mvunguni sharti uiname… Si kama zamani hata pa kuinamia au kuchutama hapakuwepo!!! 5- Fanya utafiti kadhaa wa vyuo mbalimbali halafu amua itakuwaje. Ukishapata chuo unachohitaji wasiliana nacho; linganisha bei na habari. 6-Mara nyingi huwezi kuwa na habari zote katika mtandao. Kwa hiyo ukishajua unataka kwenda wapi sasa ndiyo waandikie au waulize Wabongo wanaoishi nje wakufafanulie. Je mji ninaotaka kwenda (mathalan Washington, USA au Leicester, UK) ikoje? Je, kuna nini pale? Kama hujui watu unaweza kupata hizi habari katika mitandao maana miji yote mikubwa duniani siku hizi ina tovuti. Matumizi ya Google Earth kupata picha kamili ya miji na nchi duniani ni kitu cha kawaida siku hizi.
• HABARI MPYA ZA MASOMO NJE, 2009.
1-Ada za masomo zimepanda juu sana mwaka huu Uingereza. Ada hiyo inaathiri wanafunzi nchini na pia wanaotoka nje. Hii ina maana maisha ya kusoma ni aghali. 2-Kazi na mishahara Majuu hulipwa kwa saa si kwa juma au mwezi kama kwetu. Mara nyingi siku za kusoma ni chache kwa hiyo muda mwingi wanafunzi hufanya kazi kulipia maisha na masomo. 3-Miaka mingi wanafunzi toka ugenini wamekuwa wakitegemea ajira kadhaa kulipia masomo yao. Zamani ilikuwa rahisi hivyo lakini kuna tatizo jipya. Serikali ya Uingereza imepunguza saa za kufanya kazi hadi kuwa 20 kwa wiki. Hicho ni kiasi kidogo sana. 4-Ilikuwa kawaida wanafunzi kufanya kazi kujilipia masomo; ila kutokana na kukatwa saa hizo ina maana wanafunzi wanategemea wazazi wao Bongo kwa asilimia 75 kifedha. 5- Awali utumaji fedha wa Western Union haukuwa na masharti magumu. Aliyetakiwa kutoa kitambulisho alikuwa mtumiwaji fedha kabla ya kupokea. Leo mtumiwaji anapaswa kutuma dondoo kadhaa kwa anayemtumia Bongo ikiwepo nakala ya pasipoti, viza na habari za chuo alipo. 6-Karibuni wanafunzi wengi wamepatwa na matatizo mawili. Kwa wanawake wanabidi kukaa na jamaa wenye kipato matokeo wanapata mimba. Pili, wanaume kwa wanawake wanakaa hata miaka minane kumaliza masomo. Hii ni kwa sababu wanapoteza muda mwingi wakifanya kazi. Sam Wetengere Kitojo (fulana nyekundu) na wenzake wanaotengeneza sinema nchini Uingereza. Toka kushoto Andrew Fernandez Omari, Linda Kapinga, Ahmed Makame na mkewe. Ingawa Kitojo bado hajafahamika wala kutengeza filamu kubwa, mpangilio, nidhamu na malengo yake na wenzake yanaonyesha wanafunzi wa Kibongo wanaokuja huku kuchapa kazi badala ya kucheza cheza, kulewa na kupoteza muda. Picha ilipigwa mjini Reading wakati bwana Kitojo na wenzake walipoonyesha sinema ndogo ya “Coctum” mbele ya wadau wengine wa kimataifa na wawakilishi wa CCM Uingereza, Septemba 2010. Picha na F Macha.
7- Inaimanisha kabla ya kuja nje hakikisha una fedha, kama wazazi wako wanakuleta wawe tayari kukusaidia kifedha hata ukishakuwa nchi za nje. Si kama zamani ambapo wanafunzi wengi walijilipia wenyewe kwa kufanya kazi ugenini. Sababu kuu muhimu ni matokeo ya hali ngumu ya uchumi (credit crunch). 8- Ubalozi wa Tanzania (hasa London) unawashauri vijana wanaosoma kujiandikisha mara wanapowasili. Bila shaka kuna baadhi ya wananchi hawana hamu na idara mbalimbali za kiserikali. Ujue kwamba ukiwa nje ubalozi ni kama mzazi wa pili. Si vibaya kujiandikisha ukapata ushauri au msaada wowote wa kimawazo (au vingine) pale inapotakiwa. Wengi hungojea likitokea tatizo ndipo wakatafuta Ubalozi. Uandikishaji siku hizi si kama zamani kwenda ubalozini; unaweza kufanywa katika tovuti ya Ubalozi.
“MAJASIRI HUFAULU KULIKO WALE WANAOSITA SITA…” -Niccolo Machiavelli , karne ya 15.
• NAMNA MBALIMBALI ZA KAZI MAJUU
Kwa kuwa Wabongo wengi hawajui maisha ughaibuni yalivyo hukosa mkate. 1-Kazi zinazofanywa mara nyingi huwa za sulubu : kazi hizi zina mishahara ya kima cha chini sana lakini ndizo za kwanza na rahisi kupatikana, kama kusafisha vyoo, kupiga deki masupamaketi, kuhudumia ajuza na wazee, nk. 2-Kitaaluma kuna kazi ambazo Watanzania huwa hawazifikirii. Zinazotokana na utamaduni wetu. Kazi za kufundisha Kiswahili; kucheza ngoma (densi kwa wasichana); kueleza hadithi watoto shule za vidudu na msingi, uyaya, nk. 3-Je, utajitangazaje? Unachofanya ni kuweka matangazo katika maduka ya kitongoji unachoishi; (maduka hutoza kiasi kidogo kwa juma) au katika sehemu za matangazo ya vyuo. Je utajuaje? Kila mji una gazeti maalum la kutangaza mambo ya kila aina : mauzo, nyumba za kupanga, magari, muziki, nk. Ukilinunua unaweza kukuta kazi za kila aina. Ulizia wenyeji watakueleza. Ngoma ni ajira kubwa Majuu. Hapa natumbuiza na mwanamuziki toka Algeria, Farid Adjazairi, London Julai 2010. Picha na Louisa Le Marchand 4-Kama wewe dereva; kazi hiyo ina maslahi sana. Waweza kuajiriwa kama dereva wa teksi hasa miji kama London; na kama una leseni unaweza kufanya kozi ndogo ukawa dereva wa mabasi, kazi yenye mshahara mzuri sana. Huajiri wanaume kwa wanawake. Udereva wa mabasi Majuu si kama kwetu ambapo huendeshwa kwa kasi. Mabasi yanakabiliwa na sheria kali zinazoangalia maslahi ya abiria; hayaendi kasi kabisa. Ni moja ya kazi nzuri ingawa kwa kuwa zina shifti zaweza kuathiri wale wanaosoma. 5-Kama huna aibu unaweza kufanya kazi ya kuchorwa, kupigwa picha kutangaza miili, uzuri na sura kwa ajili ya wanafunzi wanaojifunza kuchora, wanafunzi wafanya biashara wanaotafuta watu wa kutangaza biashara zao. Kazi hii hulipwa kwa saa. 6-Waweza pia kusomea kazi nyingine kama upishi, doria au kutembeza mbwa ( maana Wazungu wanathamini sana wanyama hasa mbwa na paka) na kila siku mbwa hupelekwa kufanya mazoezi katika mapaki. Kazi hiyo ya kutembeza mbwa (dog walking) ni muhimu kwa kuwa wenye wanyama hawa wanakua kazini na hawana muda…
• YAHUSU WAKALA (MAAJENTI ) BONGO
Nimeelezwa kuwa miji mikubwa hasa Dar es Salaam kuna wakala wanaojitangaza katika vyombo vya habari. Wakala hawa wanatoza fedha kushauri vijana, kuwachagulia vyuo na kuwashauri namna ya kuja. Itabidi uangalie mwenyewe. Suala muhimu hapa ni fedha.
• VIJANA WALIOSHAKUJA AU WALIOKO HAPO Njia nyingine ya kupata habari kamili ni kuwasiliana na vijana walioko huku, wanaosoma, walioshasoma wakarudi ama likizo au wanafanya kazi wakueleze jinsi mambo yalivyo. Miti, magari mtaa wa Maida Vale, Magharibi ya London, mwaka 2008. Picha na F Macha
• MAISHA YA NJE SI RAHISI
Lazima kujitayarisha sana kimawazo na kimwili kabla ya kuondoka. 1-Hali ya hewa, utamaduni, watu wako tofauti sana. Wengi hatujui namna maisha yalivyo tofauti. Ulaya kwa mfano baridi miezi 6-8 kila mwaka. Watu hawaongei kama sisi; majirani hawasalimiani; kila mtu na lwake. Upweke. 2-Tatizo la kutojua utaishi je. Je pesa utapata wapi. Nchi tajiri zina utamaduni wa kuchapa kazi, kifedha na kibiashara. Kwahiyo jitayarishe kufanya kazi huku unasoma. Kazi nyingine mbaya sana. Kuna watu wanaosomea PHD zao huku wanafagia barabara, vyoo au kusafisha magari. Kila nukta fedha hudaiwa Majuu. Jitayarishe kuchapa kazi. Muda hauchezewi. Ukichelewa mahali dakika kumi tu unaweza kufukuzwa kazi kama huna sababu maalum au kama unarudia rudia makosa. Si kama Bongo mambo ya kuchekeana chekeana na kuzembea. 3-Siri kubwa ya maisha ya shida ni kufanya mazoezi na kula vyema. Mathalani wengi wakija nje kwa kuwa baridi sana wanajifungia ndani wakila, wakisononeka na kutazama runinga (tv). Siri ni kufanya aina fulani ya mchezo mara moja mbili kwa wiki (kuogelea, kukimbia, mpira nk) . Michezo inakupa raha fulani inayokuwezesha kupambana na maisha magumu. Mazoezi hutoa dawa inayoitwa “happy chemical” kwa jina la kitaalamu : SARATONIN. Saratonin ni utamu unaopatikana ukicheka, ukifanya mapenzi, ukila sukari, asali au kitu kitamu. Mazoezi hutoa dawa hiyo katika ubongo unaokufanya umudu maisha na kujisikia vizuri katika kila kitu. 4- Jambo jingine ni ulaji chakula. Kula matunda kwa wingi, mboga za majani mabichi (salad) na usisahau kunywa maji. Kifupi kutovuta sigara, kunywa pombe kuzidi, kula nyama kila siku (badala ya mara chache kwa wiki) huzorotesha mwili na akili.
“MOTO WA DAIMA KUFUKUZA JEHANAM KUELEKEA SEHEMU NYINGINE; MOTO MKALI WA DAIMA KUITUMIA JEHANAM MBALI NA HAPA…” -kutoka “Palco” wimbo wa mwanamuziki wa Kibrazili, Gilberto Gil (8)
MAREJEO- PATA HABARI ZAIDI
1-Blogu la James Miller kuhusu Uhamiaji – www.jamesdmiller.blospot.com 2-Barack Obama –“Dreams from My Father”, Canongate, 1995. Obama kaandika vitabu vingi ambavyo huwa na hotuba na maoni yake kisiasa na kifalsafa. Hiki kipo hivyo ila bora zaidi. Kinaeleza kwa undani maisha yake binafsi toka utotoni hadi alipoanza kupigania Urais. 3-Issa Bin Nasser Al-Ismaily-“Zanzibar : Kinyang’anyiro na Utumwa”, Oman, 1999. Kitabu hiki cha takribani kurasa 300 kigumu kupatikana Bongo au visiwani, kimechapwa Uarabuni lakini kwa Kiswahili. 4-Peter Moore – “Swahili for the Broken Hearted”, 2003, Bantam. Kitabu kimeandikwa kwa ucheshi na utani utani. Kwa mfano akiwa Tanzania anaeleza jinsi jamaa wanavyopigania kuuzia Watalii wa Kizungu vitu pale Arusha. 5-Dk. Imani Silver Kyaruzi- “Mbinu za Ujarisiamali”, 2008, Mkuki Na Nyota, Dar es Salaam. Kitabu kinapatikana Bongo. Soma mahojiano yangu na Kyaruzi hapa : www.kitoto.wordpress.com au www.bongocelebrity.com 6-Freddy Macha- “Mpe Maneno Yake”, 2006, E & D Limited, Dar es Salaam. Kitabu kina mkusanyiko wa hadithi fupi fupi nilizoandika kati ya 1976-2003. 7-Freddy Macha – “Mpe Maneno Yake” …Soma kisa cha “Mturuki, Waparaguay na Mimi.” Kinapatikana TPH na Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam au kwangu mwenyewe, nakiuza. 8- Mwanamuziki Gilberto Gil ni kati ya wasanii wanaonisisimua sana ughaibuni. Huchanganya mitindo mbalimbali katika nyimbo zake zenye pia ujumbe mzuri wa mseto kuhusu jamii na mahusiano. Huimba katika lugha kadhaa kikiwemo Kiyoruba, Kiingereza, Kifaransa na Kispanyola. Kawahi kutoa albam na bendi maarufu ya Wailers iliyopiga na hayati Bob Marley, Jamaika. Kawahi kuwa meya wa jiji la Bahia, jimbo kaskazini ya Brazili lenye weusi wengi kushinda yote nchini humo na nje ya Afrika. Kawahi kuwa Waziri wa Utamaduni katika serikali ya sasa ya Rais Lula. Gil alifungwa na kukimbilia kizuizini,London, enzi zile Brazil ikiwa chini ya utawala wa Kijeshi (1964-86). Hebu mtafute katika Google ukitaka zaidi.
Angalia habari zaidi kuhusu Freddy Macha
1-Soma mahojiano na Bongo Celebrity mwaka 2008:
http://www.bongocelebrity.com/2008/01/07/kwa-kina-na-freddy-macha/#axzz1EYuZAZpk
2-Tovuti:
http://www.freddymacha.com
3-Sikiliza na tazama moja ya nyimbo zake :
"