Na Lulu Mussa
Katika jitihada za kukuza weledi wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Idara ya Mazingira imefanya warsha kwa maafisa mazingira juu ya mikakati ya kuhimili mabadiliko ya Tabianchi.
Akifungua warsha hiyo ya siku tatu, Katibu Tawala wa Mkoa wa Songea Dk. A.H. Tarimo amewataka wataalamu hao kusimamia vizuri sheria ya mazingira na kuwaasa watoe elimu kwa jamii juu ya hifadhi ya mazingira kuanzia ngazi ya kaya.
Amesema katika kukabiliana na changamoto za mazingira Serikali imeendelea kutekeleza Sera, Sheria, Kanuni na mikakati inayolenga kuwa na matumizi endelevu ya rasilimali na maliasili kwa lengo la kufikia maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii.
“Uharibifu wa mazingira ndio kiini cha kuenea kwa hali ya jangwa na ukame, kukauka kwa vyanzo vya maji, wingi wa mifugo unaozidi uwezo wa malisho, na migongano ya ardhi” alisisitiza Dk. Tarimo.
Aidha, majadiliano kuhusu mpango wa muda mrefu wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi yalianza baada ya kuanzishwa kwa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi mwaka 1992 na Mkataba mdogo wa Kyoto wa mwaka 1997 ambao Tanzania imeridhia.
Warsha hii ya kukuza uelewa imeratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais na inafanyika Mkoani Ruvuma inahusisha Maafisa Mazingira kutoka mikoa ya Iringa, Mbeya na Songea.