Meli ya Korea Kusini iliyokuwa imetekwa na maharamia. Ilikuwa ni chereko shangwe na vifijo katika bandari ya Mombasa baada ya ndugu za raia wa Kenya waliokuwa mateka kuwaona ndugu zao baada ya miezi mitano waliokaa huko Somalia.
Meli ya uvuvi ya Korea Kusini iliwasili katika bandari ya Mombasa Kenya jumanne ikiwa na wafanyakazi 39 raia wa Kenya na wawili wa Korea Kusini na wengine wawili wa China.
Ilikuwa ni chereko shangwe na vifijo katika bandari hiyo ya Mombasa baada ya ndugu za raia hao waliokuwa mateka kuwaona ndugu zao baada ya miezi mitano waliokaa huko Somalia.
Meli hiyo ya uvuvi inayomilikiwa na Korea Kusini iitwayo Keummi ilitekwa nyara mapema Oktoba ya 2010.
Kwa mujibu wa Sauti ya Amerika (VOA) Kabla ya kutoka kwenye meli hiyo walifanyiwa uchunguzi wa afya zao na walionekana kuchoka sana lakini hawakuonyesha ishara yeyote ya magonjwa mengine.
Maafisa wa Korea Kusini wanasema hakuna fidia yeyote iliyolipwa lakini ili waachiwe mmoja wa mabaharia hao Daniel Odea anaeleza kuwa kapteni wa meli yao aliingia mkataba na maharamia wawasaidie kwenye kazi za kiharamia ambapo walijikuta bila kupenda wakishiriki katika zoezi la kuteka nyara meli nyingine kama vile York LPG iliyokuwa ikitoka Mombasa, na nyinginezo ambapo walifikishwa mpaka sheli sheli na kuteka meli ya Iran na nyingine iitwayo Belunga ambapo wafanyakazi wawili wa meli hiyo waliuwawa katika tukio hilo na hivi sasa ameendelea kusema kuwa wameacha meli nyingine 15 katika ngome ya maharamia hao wa Somalia.
Meli iliyotekwa kwa mujibu wa mratibu wa mpango wa ubaharia Afrika Mashariki Andrew Mwangura “imezeeka mno na hivyo ilikuwa haifai kuelea baharini”.
"