Adverts

Feb 6, 2011

MUME ADAI KUPANGIWA KAZI YA KUPIKA NA MKEWE.

MUME ADAI KUPANGIWA KAZI YA KUPIKA NA MKEWE.: "Robert Kipanga (29),mkazi wa Buguruni Madenge, amekana kuiba sh.1,000 ya mkewe na kudai kuwa alichukua fedha hiyo kwa ajili ya kununulia mahitaji ya jikoni kwa kuwa mkewe alimuachia kazi ya kupika chakula kwa siku hiyo. Mshitakiwa aliyadai hayo mbele ya Hakimu Jamilah Ramadhani wa Mahakama ya Mwanzo Buguruni. Amedai kuwa, siku ya tukio mkewe alichoka kupika na kumuomba yeye amsaidie kupika chakula cha mchana naye alikubali. Amedai alipokuwa akipika ugali mkewe aliondoka nyumbani naye akagundua kupungukiwa na baadhi ya mahitaji ya jikoni hivyo alichukua fedha hiyo kwa ajili ya kununua kile alichokihitaji.Amedai kabla hajaenda dukani,mkewe aligundua kutoweka kwa fedha hiyo, hivyo alianza kumdai naye akamrudishia kisha akamuomba fedha hiyo mkewe ili akanunue kitu alichokuwa na shida nacho. Baada ya kuomba kwa muda mrefu mkewe alimwambia amsubiri akamchukulie alipotoka nje alirudi na Polisi akamkamata. Kwa upande wake mlalamikaji amedai kuwa yeye ni mfanyabiashara wa mitumba ya kutembeza majumbani, pesa huwa anaipata kwa shida na kwamba mumewe amezoea tabia hiyo. Hati ya mashtaka iliyosomwa na karani Karim Wenge imedai kuwa, Januari 12 mwaka huu, saa 6 mchana, Buguruni Madenge, mshitakiwa aliiba sh. 42,000 zilizokuwa chumbani mali ya mkewe Sara Goshoka. Mshitakiwa amekana mashtaka na kesi hiyo itatajwa tena Februari 2, mwaka huu.
"