Nilijiona nipo sehemu yenye ubaridi, na kumetulia kimya, nikajiona nimezungukwa na watu warefu waliovalia majoho meupe na usoni wamejifunika kuficha sura zao, na kuachia sehemu ya macho tu, na wote walinizunguka mimi. Kwa hisia zangu walikuwa wakigombea nyama yangu, au kugawana mwili wangu. Mmoja wao alikuwa akiagiza visu na vifaa vingine ambavyo vilionekana kama mapanga yenye ncha kali, na kila mara alikuwa akikirudisha kifaa au kukisogeza pembeni kifaa alichotumia kikiwa kimejaa damu. Hakuna hata mmoja aliyeonyesha dalili ya huruma machoni mwao, hasa huyu aliyekuwa akiagiza mapanga na visu vya aina yake.
Nilijaribu kuinua kichwa kuwaomba wanihurumie na kuniacha huru, lakini sikuweza kuinua hata sehemu ya mdomo wangu, nilikuwa nimelegea mwili mzima, na hata akili ilikuwa ikiwaza tu kuwa huenda wanafanya kitu kibaya kwenye mwili wangu. Niliwaona kama wachawi wanaokula mwili wangu, na walianzia kunitoa matumbo yangu, maini, na sehemu za ndani, na…au sijui nini wanakitafuta ndani ya tumbo langu, kwani uwezo wa kuinua kichwa na kutizama nini wanachokifanya kwenye maeneo yangu ya kuanzia tumboni kwenda miguuni haukuwepo, bali kuwatizama wakibadilishana vifaa! Niliwatizama kwa hisia na wala sio macho…macho yalikuwa yamefunguka kwa hisia!
Kwa muda waliochukua nilihisi kuwa watakuwa wameshamaliza, na sijui kutakuwa kumebakia kitu gani. Kwa kweli nilisha kata tamaa kabisa kuwa mimi sina kiwiliwili na sasa wataanza kunikatakata kifuani na pengine watanimalizia kichwani! Wakati wanaendela, nikaoana jambo la ajabu, walitoa kiumbe cha ajabu mwilini mwangu, kilionekana kama mtu, lakini mtu huyo alikuwa amejaa damu, niliogopa hata kumtizama yule mtu kwani kama ni mwanga huenda akakilamba zile damu zilizomganda yule mtu. Alikuwa mtu kwa uwoni wangu, lakini sura ilikuwa kama ya kitoto –kitoto…ila kubwaa.
Alikishika kile kitoto-jitu akawa anakata vitu fulani, sijui ni nyama zilizomzunguka yule mtu-kitoto au nini, halafu akamkabidhi mtu-jitu mwingine, ambaye alikuwa kashika mavitambaa makubwa, kwa mtizamo ni mwanamke, ingawaje kajifunika uso, huyu mtu-jitu akakizungushia kile kitoto-mtu na kukiweka kwenye chombo kikubwa kama beseni kubwa, halafu wakaendelea kufanya wanalolifanya kwenye mwili wangu. Nilitamani kuwaambi wanirudishie hicho walichokitoa tumboni mwangu, ingawaje sikujua ni namna gani mtoto-mtu aliweza kukaa tumboni mwangu na ukubwa wote ule. Nikataka kusema `nipeni mtoto –mtu wangu’ lakini mdomo haukuweza kufunguka!
Baadaye wale watu-mijitu wakawa `wameshiba’ moyoni nilijua hivyo,walikuwa wakila nyama yangu na sasa walikuwa wametosheka, na kuniacha nikiwa gofu la mtu. Nikamuomba mungu wasiniache pale nikabebwa na mwewe au midege yenye uchu, au fisi…nikawa najaribu kulia , lakini machozi yakawa hayatoki, nikajua kwa vile damu imeshakauka hata machozi yamekauka pia.
Niliona ajabu pale walipochukua kitu kama kamba…zilikuwa nene , na zinametameta na kama vile kamba hizo zina maji yanapita ndani yake, wakanifunga mkononi…na nilihisi kamba hiyo ikizamishwa kwenye mishipa ya damu…nilihisi kabisa, kamba hiyo ikipenya hadi kwenye moyo, …ina maana wanataka kunimalizia damu iliyobakia…nikawaza, na kwanini kamba ya kunifungia izamishwe ndani ya mishipa ya damu kama sio kuninyonya damu?
Baadaye kabisa, nikahisi nabebwa hewani hewani au kitu kama gari linanibeba…wananipeleka wapi hawa watu-mijitu, au ndio wanaenda kunitupa, kwani nimebakia mifupa, au gofu la mtu? Nikawaza na kuwazua, kwani kinachoonekana ni kuwaza tu, hakuna kauli. Na baadaye nikahisi nahamishwa kwenye eneo jingine, na zile kamba zikawa zimefungwa kwenye michuma mikubwa iliyotokea huko juu, nisipopaona vyema. Nipo wapi hapa…ubaridi, utulivu kama huko nilipotoka…nipo wapi hapa jamani, nikajaribu kufunua mdomo lakini, ilikuwa kama vile sina mdomo …!
Baadaye wakaondoka , …nakahisi nipo peke yangu, nikajiuliza hapo nilipo ni porini au ni wapi, na mbona kamba niliyofungiwa imefungwa kwenye chuma, ni pori gani hili lina vyuma. Nikajaribu kugeuza macho, yakawa hayageuziki, ina maana hata macho sina, ikawa kuhisi hisi tu! Nikawaza kuwa kama damu imekauka, maji yamekwisha mwili mpaka machozi hayatoki, macho yatageukaje?
Mara nikaona mtu-jitu akinikaribia,…aaah, yule yule mwanamke aliyemchukua mtoto-jitu toka tumboni mwangu, alikuwa kavaa kitu usoni, akanisogeza usoni mwangu na kusema kitu, sikuelewa ni, nini, …lakini nilisikia neno kama radi…tototo…halafu akaondoka . Nilitamani nipige kelele kuwa anirudishie mtoto wangu, lakini sikuweza, akaondoka na baadaye akarudi akiwa hana kitu, nikataka kutoa kauli , kumuulizia kuwa kampelekea wapi mtoto wangu, lakini sikuweza. Baadaye akakiondoa kile kitambaa usoni, …..mungu wangu, nilitamani niinuke nikimbie, macho ya huyu mtu-jitu yalikuwa makubwa kama mpira wa miguu,meno yalikuwa makubwa kama majembe ya trekta kubwa sana, na aliptabasamu kuyaonyesha yalitisha sana! Au ndio kaja kunimalizia, …baada ya kummaliza mwanangu…akili iliwaza hivyo, kuwa ni `mwanangu waliyemtoa tumbaoni…lazima nifanye kitu…lazima nijitetee…lakini kwa vipi?
Alionekana ni mtu-jitu-mwanamke. Alishika ile kamba nene iliyotoka mkononi mwangu na kufanya kitu nisichokielewa, akawa amashika kitu kama gunia , yeye kwake kwasababu ni jitu kashika kama kapaketi ka….sijui hata kuelezea, kwani akili hukumbuka itakavyo…lakini kile kitu, ambacho mimi nilikiona kama gunia la plastiki, lilikuwa limejaa maji ndani yake, akalitundika kwenye chuma na …sijui alikuwa analitoboa ili mai yanimwagikiea u vipi, lakini maji niliyoyaona mle ndani hayakumwagika!
Yule mtu-jitu mwanamke akasogeza kiti na kukaa karibu na nilipolazwa, akawa ameshika karatasi kubwa kama shuka linalojaa eneo lote nililoweza kuliona, kama vile limejaa chumba kizima,kulikuwa na maandishi makubwa ajabu nafikiri alikuwa akisoma kitu! Nikajiuliza. Huenda anasoma, kwa vile ni mijitu mikubwa lazima hata vitabu vyao vitakuwa vikubwa. Muda ukawa unapita name huku nawaza, wanasubiri nini hawanimalizii kunila sehemu iliyobakia nini!
Masaa yakawa yanakwenda na subira ikawa inanishinda, niliomba mungu wangu wasinimalizie sehemu iliyobakia, angalau yabakie mabaki ili ndugu zangu waweze kunizika. Nikaomba sana, na kila mara nikitulia na kumwangalia yule mtu-jitu mwanamke , namuona habandui macho yake kunitizama, anatizama ile karatasi halafu ananitizama mimi. Ina maana kaamurishwa asiondoe macho yake kunitizama ili nisitoroke nini?
Akili ikiwa imechoka kufikiri na kitu kama usingizi kikawa kinaninyemelea na hatimaye nikahisi kulala na kuona kichwa hakifikiri tena. Na kwa mbali nilimuoana yule mtu-jitu –mwanamke akishika ile kamba nene na kufanya kitu fulani, halafu akainuka na kunitizama machoni, alileta kidole chake kwenye jicho langu akawa ananifunua, kilikuwa kama mchi wa kutwangia. Halafu akasogea mbele nikahisi anaondoka. Au ndio anakwenda kuwaita wenzake waje kunimalizia? Ni akili ikawa imechoka kuwaza…
‘Hapa, hapa, ndipo pakutorokea, hapa hapa, jitahidi mwanamke, jitahidi utoroke, kabla hawajarudi tena….’ Nikahisi sauti ikitoka sijui akilini au wapi, sauti hiyo ilikuwa ikiniambia hivyo. Na kweli baada ya ile sauti kusikika akilini,nikahisi nguvu za ajabu zikinijia, nikaweza kuinua mabaki ya mwili wangu na nikajitutumua na kujikokota , nilitumia nguvu kutoa ule mnyororo au kamba niliyofungwa mwilini mwangu, ulikuwa kama umezamishwa ndani ya mwili wangu, kwani kila ulipokuwa ukitoka nilihisi mwili mzima ulikuwa ukisikia maumivu yake, na nahisi ulikuwa umeanzia moyoni , lakini sikujali hatimaye ukatoka…nikajitutumua nikaweza kuamuka pale nilipokuwa nimelala, nilijaribu kutizama mabaki ya mwili wangu yaliyobakia kwa chini, lakini kichwa kilikuwa hakiwezi kuinama, nilikuwa kama roboti. Kichwa kinaangalia mbele tu…!
Nikatoka pale nilipolala nikajikongoja na niliona sehemu kama upenyo wenye mwanga, ni kama upenyo mkubwa kama mlango, lakini ni mkubwa sana…cha ajabu hata mimi nikajiona kama `jitu’ maana hata kupita kwenye ule upenyo mkubwa nilikuwa najipenyeza…oooh, ina maana hata mimi ni jitu –mtu…nikacheka, kumbe naweza kupambana na hawa-watu –mijitu…nikatoka mle nilipokuwa na kuingia sehemu yenye mwanga mkali, ulioenea kote…mwili wangu ulikuwa kama umetoka kwenye barafu na kuingia kwenye moto…
‘Bora nikafie kwenye huu moto kuliko kuliwa na haya majitu-watu…bora…bora…lakini nakumbuka walitoa kitu mwilini mwangu kama mtoto-jitu…wamekiweka wapi! Nikawaza, nikaanza kusogea huku naangaza macho huku na kule mithili ya roboti, linageuka mzima-mzima…
Baadaye nikawa najiona kama napaa, au natembea, lakini mwendo wa kiroboti. Hadi nikafika mahala kuna nguo zimeanikwa, nguo ni kubwa ajabu…nani anavaa nguo kama hizi, lazima ni hii mijitu watu. Nikaona kitu kama kitambaa, kimeshonwa nikakisogelea na kuona kinaweza kunisaidia kuficha macho uso wangu usiungue na mwanga huu mkali na kujikinga na joto. Nikakivaa, bahati nzuri, kilifunika kichwa chote na kuweza kuacha sehemu ya macho tu…
‘Safii kabisa, haya majitu-watu hayataniona kamwe, nikaingiwa na nguvu nakuanza kutembea kwenye eneo lilojaa mwanga mkali unao-unguza. Nilihisi kuona watu-mijitu wakitemebea, lakini walikuwa hawaji ninapotembea mimi, ilikuwa kama kila mtu-jitu ana njia yake. Nikaongeza mwendo, nikawa naondoka nisipopajua….joto, ..joto…likawa kero, lakini nashukuru usoni pamefunikwa!
Sijui ilikuwaje kwani wakati natembea nihisi kitu kimenigonga na kujikuta nikielea hewani juu kwa juu kama mtu anayepaa juu kwa juu..na mwisho nilijikuta nikidondokea kwenye vitu kama matakataka, kunatoa harufu mbaya…!
‘Umeua, umeua…’ nikasikia sauti kama mwangwi ikisema hivyo…Nilijaribu kuinuka pale nilipodondokea, sikuweza. Ina maana nimekufa…? Nikawaza kama nimekufa, mtu anakufa mara ngapi! Mara kelele zikasikika toka mbali zikisema `hajafa bado mzima, …’ Ina maana mimi sijafa, haiwezekani, nikajitutumua na kujiinua na nilipogeuka kama roboti, niliona mijitu watu imejaa kwa mbele, lakini ilikuwa kama kilima, mimi nipo chini wao wapo juu. Kila walipofunua meno ya ilikuwa inatisha, nikaona hapo hakuna heri nikimbie tu..
Nilikimbia, nilikimbia….na baadaye nikawa kama mtu amezama ndani ya giza nene, sikuweza kufikiri tena!
Ilikuwa kama vile nililala, nilipoamuka, nikajikuta nimetokea sehemu ya dunia nyingine. Sikumbuki nilipotoka, au imekuwaje. Niliwaona watoto, wamenizunguka, nikahisi kitu cha ajabu, nilikuwa wapi na nahisi kama nimetokea sehemu ya hatari na nilikuwa nikifukuzwa na kitu, lakini sikumbuki kilikuwa kitu gani, au…akili ikawa haikumbuki kabisaaa…! Nilihisi kupitia sehemu mbalimbali, kuimba maneno kama `nataka mtoto wangu…’ nikahisi kuishi kwa watu, na baadaye nikapewa mtoto…ooh, alikuwa mtoto wangu, nikahisi hivyo.
Siku moja nikawa nimelala, mara wakaja watu, wameshika mapanga…wakaniamusha na kuniambia `wewe ni mwanga, unatulogea watoto wetu…’ nikashangaa, mimi ni mwanga, kwani umwanga ni nini…kabla sijawajibu wakaanza kunikatakata na mapanga…wakanikata mikono yote, wakanikata miguu yote, wakawa wananikata usoni, kukipasua kichwa, na baadaye wakanichoma moto…nikawa naungua kama nyama ya kubanikwa…nikasema sasa nikizubaa nitakuwa majivu, bora niinuke….nikahisi mtu ananisaidia kuinuka, nikajua ni wenzao wanataka kunimalizia…nikapiga ukulele…nisaidieni nakufaaa…lakini sauti haitoki, nikapiga kelele…kelele…kelele..
‘Wewe tulia …tulia….’ Ni sauti iliyonizindua….nikainuka haraka kitandani, kumbe nilikuwa nimelala kitandani lakini hata hivyo nikataka kukimbia, wakanidaka madakitari, na kunilazimisha kulala na nilipunua macho vizuri, nikastaajabu kumbe nilikuwa….oh, na huyu dada si ndiye yule niliyemuona kuleee…oh, ndani ya ndoto…ndiyo yeye aliyemchukua mtoto wangu…ndiyo yeye, nikaanza kupiga ukulele huku namnyoshea kidole yule nesi; `Nataka mtoto wangu, nasema nataka mtoto wangu, wewe dada ulimchukua mtoto wangu , yupo wapi….’
Nashindwa kuachia kuandika, lakini inabidi...muda umekwisha, tutaonana kwenye sehemu inayofuata, je nesi atasema nini?
Ni mimi: emu-three
http://miram3.blogspot.com/feeds/posts/default?alt=rss
"