YUSUF Manji, mfanyabiashara wa Dar es Salaam, ni miongoni mwa walionufaika na mabilioni ya shilingi ambayo yalikwapuliwa na kampuni ya kitapeli ya Kagoda Agriculture Limited kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), MwanaHALISI limegundua.
Taarifa zinasema Manji, kupitia kampuni yake – Quality Finance Corporation Limited (QFCL) – ambayo anamiliki na baba yake, Mehboob Manji, “anakabwa koo na serikali” ili arudishe dola za Marekani 28 milioni (Sh. 31 bilioni) zikiwa sehemu ya fedha zote zilizoibwa na Kagoda.
Nyaraka zilizopo zinaonyesha kuwa Manji na kampuni yake walikopa kiasi hicho cha fedha kutoka kampuni ya Kagoda chini ya mkataba wao wa tarehe 12 Septemba 2005.
Kampuni ya Kagoda ilikwapua jumla ya dola za Kimarekani 30,732,658.82 (Sh. 40 bilioni) katika Akanuti ya Madeni ya Nje (EPA), ndani ya BoT. Fedha hizi na nyingine zipatazo Sh. 73 zilichotwa katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.
Manji anadaiwa chini ya kinachoitwa urejeshaji kiasi fulani cha madeni ya EPA kwa mpango wa Rais Jakaya Kikwete wa msamaha kwa wezi au washirika wao watakaokubali kurejesha sehemu ya fedha zilizoibwa.
Barua ya aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa serikali, Johnson Mwanyika, Kumb. Na. JC/B.20/29/16 ya 20 Mei 2008 iliyotumwa kwa Manji, inamtaka Manji alipe fedha hizo katika kipindi alichokubaliana katika mkataba wake na serikali.
Mwanyika alikuwa akijibu ombi la Manji la 28 Agosti 2008 la kutaka kusogeza mbele muda wa kurejesha mabilioni hayo kadri ya makubaliano.
Manji alikuwa akimkumbusha Mwanyika kuwa makampuni yake yalitoa dhamana ya mali isiyohamishika na vilevile kutoa hundi nane zenye tarehe za mbele.
“Bahati mbaya tumeshindwa kufanya malipo ambayo yalikuwa yafanywe tarehe 1 na 15 Aprili 2008 kutokana na upatikanaji kwa viwango vidogo wa fedha za kukulipa…Tunaona pia kuwa hatutaweza kukamilisha wajibu wetu hata kwa tarehe 1 Mei 2008,” anaandika Manji.
Katika barua hiyo, Manji anaomba kusogeza mbele muda wa kulipa na kwamba warejeshewe hundi zao ili waweke tarehe mpya. Kagoda inaeleza katika mkataba wake na Manji kuwa mkopo huo ulipaswa kulipwa katika muda wa miaka mitatu (3), kwa riba ya asilimia 11 kwa mwaka. Haijafahamika Kagoda walipata wapi mamlaka ya kukopesha fedha iliyodaiwa kukusanywa kutoka kwa wadai wa serikali wa nje ya nchi.
Manji na baba yake Mehboob, ndio wanaonyeshwa kuwa walisaini mkataba huo kwa niaba ya QFCL, huku waliosaini kwa niaba ya Kagoda, wakitajwa kuwa ni Francis William na John Kyomuhendo ambaye tangu sakata la Kagoda ametajwa kuwa mfanyakazi wa Rostam Aziz.
Mbali na Manji na baba yake kuwa wakurugenzi wa QFCL, ni haohao ambao pia ni wadhamini binafsi wa mkopo ili kuhakikisha fedha hizo zinarejeshwa.
Taarifa zinaonyesha pia kuwa ni Yusuf Manji aliyedhamini Kagoda kufungua akaunti katika tawi la CRDB Benki la Holland jijini Dar es Salaam ambako mabilioni ya shilingi yalipitia.
Mkataba wa makampuni hayo mawili ulisimamiwa na mwanasheria Nasir Rattansi na mkopo wenyewe ulitakiwa kuwa umemalizwa kulipwa ifikapo 28 Desemba 2008.
Kufumuka kwa taarifa hizi za Kagoda kunaiweka serikali ya Kikwete katika mazingira magumu. Serikali imekuwa ikikana kufahamu wamiliki wa Kagoda na kwa zaidi ya miaka mitano sasa imekaa kimya juu ya wizi wa kampuni hiyo.
Aidha, serikali imekuwa ikijikanyaga kuhusu wizi huu. Aliyekuwa waziri wa fedha, Zakia Meghji aliwaandikia maodita wa kampuni ya Deloitte & Touche ya Afrika Kusini akisema, fedha za Kagoda zilitumika kwa “kazi za usalama wa taifa.”
Katika barua yake ya 15 Septemba 2006, Meghji anasema, “Kama unavyofahamu vema, mamlaka ya serikali huwa na siri, vilevile haja ya kugharamia matumizi ya busara.
“Kwa hiyo... malipo ya dola 30,732,658.82 za Marekani yaliyofanywa na BoT kwa Kagoda Agriculture Limited, yaliidhinishwa na serikali kugharamia matumizi yake nyeti na ilikuwa lazima kuchukua hatua hii ya kudumisha usiri huu.” Hatua hii inaleta maswali mengi kuliko majibu; yakiwa ni pamoja na iwapo Manji na wakwapuaji wa Kagoda ndio hasa wanaitwa “Usalama wa taaifa.”
Hata hivyo, kwa mujibu wa nyaraka zilizopo, 12 Septemba 2005, siku ambayo kampuni ya Manji na baba yake wanadai kufunga mkataba wa kukopa mabilioni ya shilingi, Kagoda yenyewe ilikuwa haijasajiliwa.
Cheti cha usajili wa Kagoda Na. 54040 kilichotolewa na ofisi ya Wakala wa Usajili wa Leseni za Biashara na Makampuni (BRELA), kinaonyesha Kagoda ilisajiliwa 29 Septemba 2005, siku 17 baada ya Manji kufunga mkataba na kampuni ya kitapeli.
Watu muhimu katika siri ya Rais Kikwete kuhusu wezi wa fedha za BoT ni Inspekta Jenerali wa Polisi (IJP), Said Mwema, Mkurugezi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Edward Hoseah na Mwanyika, ambao walikuwa wajumbe wa Kamati Maalum ya rais ya kufuatilia walioiba benki.
Kazi za kamati hii zimebaki siri ya watu hao wanne; hata idadi ya watu waliogundulika, walioahidi kulipa na kiasi watakacholipa imebaki siri yao.
MwanaHALISI lina taarifa, tangu miaka mitatu iliyopita, kuwa mwenye kampuni ya Kagoda au anayejua shughuli zake ni Rostam Aziz.
Wakili Bhyidinka Sanze wa kampuni ya mawakili ya Malegesi – Malegesi Law Chambers – ya Dar es Salaam, katika andishi rasmi kwa Kamati ya rais ya kushughulikia wizi kwenye akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), anakiri kuwa ni yeye alishuhudia “…mikataba ya Kagoda na makampuni mengine ya nje.”
Anasema alishuhudia mkataba wa Kagoda ndani ya ofisi za kampuni ya Caspian Construction Limited ambayo inamilikiwa na Rostam iliyoko Mtaa wa Milambo Na. 50 katikati ya jiji la Dar es Salaam.
Sanze anasema, “Niliitwa na Bw. Malegesi ofisini kwa Bw. Rostam Aziz…Nilipofika…niliwakuta Bw. Rostam Aziz, Peter Noni (Mkurugenzi Mtendaji wa sasa wa benki ya raslimali) na Bw. Malegesi; wakaniambia fedha hizo zinahitajika kwa ajili ya kugharamia uchaguzi wa CCM na rais wake.”
Andishi la wakili linaeleza kuwa Rostan Aziz, Peter Noni na Bered Malegesi walimthibitishia Sanze kuwa Rostam alikuwa kwenye kikao ambako rais mstaafu Benjamin Mkapa alitoa maelekezo kwa Gavana Ballali kutoa fedha hizo kwa Rostam kwa ajili ya uchaguzi.
Bali taarifa zilizoenea Dar es Salaam zinasema Rostam aliamua “kumuuzia kesi Manji ili kujinusuru na kashfa ya Kagoda.” MwanaHALISI lilipowasiliana na Manji kutaka kufahamu iwapo madai hayo ni kweli alijibu, “Hivi sasa ni vita.” Hata hivyo, Manji hakufafanua vita hivyo vinalenga kuangamiza nani.
Nyaraka zilizo mikononi mwa gazeti hili zinaonyesha risiti kadhaa za serikali zinazodaiwa na wa ndani wake kuwa ndizo zilizotolewa na serikali kuthibitisha Manji kurejesha fedha za Kagoda.
Miongoni mwa risiti hizo ni Na. 31494282 yenye thamani ya Sh. 4.5 bilioni; 31494264 ya Sh. 4.5 bilioni na 31494283 ya Sh. 4.5 bilioni. Bali tarehe za risiti hizo zinagongana na zile ambazo Manji alielekeza katika mawasiliano yake na Mwanyika ya tarehe 28 Aprili 2008.
Juhudi za kuthibitisha uhalali wa risiti hizo na malipo yanayodaiwa kufanyika hazikufanikiwa. Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk. Servacius Likwelile hakupatikana kwa maelezo ya Katibu Muhtasi wake kuwa alikuwa katika mkutano akijiandaa kwenda bungeni Dodoma.
Baada ya mwandishi kusisitiza ni lazima aonane na Likwelile kwa sababu kuna jambo la dharula, katibu huyo alisema Likwelile hawezi kuwa na muda huo.
“Kwanza umepitia mapokezi? Huwezi tu kuja ofisini kwa mtu kwa vile wewe ni mwandishi na ukapewa nafasi ya kuzungumza naye. Ukitaka labda nikupangie miadi uje siku nyingine,” alisema mwanamama huyo.
Mwandishi aligoma kuondoka kutoka katika ofisi hiyo na ndipo katibu huyo aliposema kuwa bosi wake (Likwelile) ameagiza kama kuna maswali yapelekwe katika ofisi ya uhusiano ya wizara.
Risiti hizo zilipelekwa kwenye ofisi ya uhusiano ambayo nayo ilizipeleka kwenye ofisi inayohusika na hundi zilizolipwa na hazina, lakini majibu hayakuweza kupatikana kwa madai kwamba jambo linalozungumziwa ni la miaka mitatu.
Source: Mwanahalisi
"