Adverts

Feb 9, 2011

Rais Kikwete akutana na Bwana Johnnie Carson, Naibu Waziri wa Nchi Marekani anayeshugulikia Masuala ya Afrika

Rais Kikwete akutana na Bwana Johnnie Carson, Naibu Waziri wa Nchi Marekani anayeshugulikia Masuala ya Afrika: "
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akiwa katika mazungumzo na Naibu Waziri wa Nchi wa Marekani anyeshughulikia masuala ya Afrika Bwana Johnnie Carson, Ikulu jijini
Dar es Salaam leo mchana.

Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akimkaribisha ikulu Naibu Waziri wa nchi wa Marekani anayeshughulikia masuala ya Afrika Bwana Johnnie Carson ambapo walifanya mazungumzo.
Tanzania ni moja ya nchi nne (4) za kwanza duniani zinazotarajia kunufaika na uhusiano wake mzuri na Marekani.
Naibu Waziri wa Nchi wa Marekani anayeshughulikia Masuala ya Afrika, Bw. Johnie Carson amemweleza Rais Kikwete alipofika Ikulu leo mchana ambapo ameleta salaam za Rais Obama na kueleza mpango mpya wa Marekani wa kuongeza kasi ya ushirikiano baina ya Marekani na nchi mbalimbali duniani.
“Marekani inataka kuongeza mazungumzo na uhusiano na nchi mbalimbali duniani, na Tanzania ni moja ya wenza wetu katika maendeleo, na tunaiona Tanzania kuwa ni moja ya wenza madhubuti katika mazungumzo na tunataka kushirikiana zaidi na Tanzania” Bw. Carson amesema.
Katika ushirikiano huo mpya nchi za Ufilipino, El Salvador, Tanzania na Ghana zitashirikiana na Marekani ambapo uhusiano huo mpya una lengo la kufanya mazungumzo ya pamoja ambayo yataharakisha maendeleo na kuleta maendeleo katika nchi hizi.
“Marekani inajivunia uhusiano huu kwa sababu Tanzania imetekeleza na kutumia misaada ya Marekani vizuri na hivyo tunataka tushirikiane zaidi”Amesema.
Bwana Carson yuko nchini na ujumbe wa wataalamu ambao watakaa na wataalamu na viongozi wa Serikali ya Tanzania na kwa pamoja watabainisha maeneo ambayo yatafanyiwa kazi na hatimaye kuongeza kasi ya maendeleo.
Mazungumzo hayo yataangalia sekta mbalimbali za kilimo, biashara, miundo mbinu na maeneo mengine ya maendeleo.
Rais Kikwete amemhakikishia Naibu Waziri huyo wa Marekani kuwa Tanzania imepania kuleta maendeleo kwa wananchi wake na misaada yote ya Serikali ya Marekani imekuwa ya manufaa na yenye kugusa maslahi ya wananchi.
“Tanzania imefaidika sana na uhusiano huu, misaada ya Mrekani kwenye malaria, HIV, barabara, maji, kilimo na sasa uhusiano huu mpya, yote haya ni mambo mazuri na yenye manufaa kwa wananchi wake” amesisitiza na kuongeza kuwa uhusiano huo mpya, umeongeza matumaini mapya katika juhudi za Serikali ya Awamu ya Nne kuleta maendeleo na kukuza uchumi.
Mwisho.
Imetolewa na Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
Ikulu.
Dar es Salaam.
8 Februari, 2011
"