Feb 24, 2011
YALIYONENWA NA MAGUFULI YAMEANZA KUTIMIA........
"Wakati waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, akiendelea kusisitiza msimamo wake wa kuvunja majengo na kuondoa mabango yaliyo kwenye hifadhi ya barabara bila kulipa fidia, jijini Mwanza shughuli imeanza ....Katika utekelezaji wa hilo, tayari mabango kadhaa jijini Mwanza yameanza kupigwa x ikiwa ni utekelezaji wa sheria iliyopo tangu mwaka 1938, kabla ya mabango.
Kwenye kikao cha Kamati ya Miundombinu kilichowashirikisha wadau wa usafirishaji mjini Dar es Salaam. Waziri alisikika akisema “Wakati nakabidhiwa wadhifa huu niliapa kusimamia sheria, nikaongeza na neno ‘Mungu nisaidie’ hivyo kulipa fidia watu waliovunja sheria ni kukiuka sheria ambayo ilikuwepo kabla yao. “Majengo yaliyojengwa kwenye hifadhi ya barabara yapo mengi, yakiwemo ya TANESCO na Wizara ya Maji, eneo la Ubungo. Yote yatavunjwa bila kulipwa fidia, ndiyo maana nikamwambia Meneja wa TANROADS mkoa wa Dar es Salaam aanze kubomoa ofisi zake ili asimamie vizuri kazi hiyo,”
Hata kama kuna kampuni inayotaka kuweka mabango, iingie mkataba na Mfuko wa Barabara na si vinginevyo ili fedha ziingie kwenye mfuko na zitumike kujenga barabara nyingine. Waziri Dk. Magufuli alisema halmashauri zinakusanya fedha na kwenda kuzitumia kulipana posho kwenye vikao vya madiwani, na si kujenga barabara kwa maendeleo ya wananchi.
Kwa mujibu wa Dk. Magufuli, kuyaacha mabango na majengo ndani ya hifadhi ya barabara ni kutowatendea haki Watanzania, ambao kodi zao zilitumika kutengeneza barabara kwa gharama kubwa.
Alisema endapo halmashauri zinataka kuingia mikataba ya kuweka mabango, zifanye hivyo katika barabara zinazozisimamia na si zinazosimamiwa na TANROADS.
Magufuli tayari ameziwekea ‘mgumu’ Halmashauri za Jiji na manispaa nchini akisema, “mabango yote yaliyomo kwenye barabara zetu tutayang’oa. Haiwezekani nyumba ajenge mwingine halafu aje mtu apangishe bila kukuarifu.”"