Na Danny Tweve
Mbozi.
Madereva wa magari makubwa yanayotumia mpaka wa Tunduma na Zambia jana waliamua kuchukua hatua za kukomesha matukio ya ubakaji, mauaji na uporaji hadharani yaliyodumu wiki mbili sasa pasipo hatua za jeshi la polisi.
Hatua ya madereva hao inafuatia dereva mwenzao Omary Juma anayeendesha magari ya kampuni ya Akon Co Ltd kujeruhiwa nusura ya kutolewa roho juzi usiku wakati akitoka kwenye bar moja katikati ya mji huo kuelekea mahala alipopangisha kulala.
Inaelezwa kuwa dereva huyo akiwa na wenzake alivamiwa na kikundi cha vijana waliojitwalia mamlaka ya kukaba watu hadharani hata bila hofu na kutumbukizwa kwenye matope nyuma ya roli moja ambapo wenzake walishtukia mwenzao akiwa katika hatua ya kuelekea kukata roho baada ya kukandamizwa na kujeruhiwa vibaya.
Kufuatia tukio hilo ambalo sasa linaelezwa kuwa ni la tatu kuwakuta madereva hao na kwa wanawake kubakwa na kujeruhiwa kuwa la 8 ililazimu madreva hao kuweka mkakati wa kukisaka kikosi hicho baada ya kuripoti awali polisi lakini hakuna kilichofanyika.
Kutokana na hali hiyo madereva hao leo mchana wameendesha msako ambapo walianza mtaa kwa mtaa baada ya kumwaga dau kwa vijana wa vijiweni watoe data kundi hilo linaongozwa na nani? ambapo haikuwachukua muda mrefu walipotajiwa kinara wa mradi huo kuwa ni kijana aliyetajwa kwa jina la Mustapha!.
Kufuatia hatua hiyo walimsaka hadi kumkamata ambapo alipewa chai ya kutosha, ambapo polisi waliingilia kati kumwokoa na kumpakiza kwenye gari lao PT 1426 na kukimbizwa polisi yeye pamoja na majeruhi wa kukabwa jana usiku bwana Omary Juma ambaye alimtambua kijana huyo kuwa miongoni mwa waliomkaba.
Akizungumzia hali hiyo dereva mwingine Ramadhan Mangushi amesema matukio ya kuwashambulia madereva wa magari makubwa na kwamba hatua hiyo imeambatana na ubakaji wa hadharani kwa wanawake katika eneo la katikati ya mji wa Tunduma na kwamba hakuna hatua zilizochukuliwa licha ya kuripotiwa.
wamesema ili kukomesha halo hiyo bado madereva wataendelea kuwasaka watuhumiwa wengine katika tukio hilo na kwamba itafikia mahala wageni watajenga hofu juu ya mji huo hali ambayo itaathiri mwelekeo wa uwekezaji uliofanywa kwenye eneo hilo hasa katika sekta za biashara za hoteli, bar na maduka.