Mar 1, 2011
Daraja FC Yaisambaratisha CRDB Njombe
Yaifunga 3-1
· Zatoa changamoto kwa mashirika mengine
Na Anither Kitteni
Timu ya shirika la Daraja kutoka Njombe imeisambaratisha timu ya CRDB tawi la Njombe kwa kichapo cha mabao 3 kwa moja katika mchezo mkali wa kirafiki uliofanyika katika uwanja wa Magereza mjini Njombe.
Mchezo huo ulianza kwa kasi sana ambapo watunza fedha kutoka benki ya CRDB tawi la Njombe walijipatia bao la kuongoza mapema mnamo dakika ya saba kupitia mshambuliaji wao machachari, Frank. Baada ya muda mfupi, vijana wa Daraja waliweza kusawazisha kwa bao la ufundi wa hali ya juu kupitia kwa winga wao anayekulikana maarufu kama Meneja.
Kabla ya kipindi cha kwanza kumalizika, vijana wa Daraja FC waliongeza bao la pili lililopatikana baada ya mchezaji wa CRDB FC, Robert, kujifunga alipojaribu kuokoa mpira wa shuti kali lililopigwa na mchezaji wa Daraja FC.
Kipindi cha pili kilianza kwa makeke sana kwa timu zote kukosakosa lango la mwenzie. Ngome za timu zote mbili zilifanya kazi ya ziada kuzuia mashambulizi kutoka kwa maadui wao ambapo timu ya CRDB ilikosa bao kwa shuti iliyopigwa na mshambuliaji wao lakini hatimaye kuokolewa na kipa wa Daraja.
Mashambulizi ya timu ya Daraja yalizaa matunda mnamo dakika ya 65 ambapo mshambuliaji wa Daraja FC, Robert Zephania maarufu kama ‘Chacharito’ alifunga bao la tatu kwa ustadi mkubwa sana baada ya kupata basi maridadi kutoka kwa Winga, Meneja. Vijana wa Daraja sasa walikuwa mbele kwa mabao 3 kwa moja la CRDB Njombe.
Timu ya Daraja ilizidi kufanya mashambulizi ambapo mshambuliaji wao, Longino almaarufu kama Babu bao la wazi baada ya kupiga nje akiwa yeye na kipa. Beki mahili wa Daraja FC, Juma Idd maarufu kama Zungu alifunga bao lakini refa alilikataa akidai kuwa kipa wa CRDB alifanyiwa madhambi. Hadi mwisho wa mchezo, timu ya Daraja waliibuka kidedea kwa kuichabanga CRDB FC kwa goli 3-1.
“Pamoja na kufurahia ushindi, pia tumepata wasaa wa kujijenga kimahusiano na tunaamini tutakuwa tumefungua ukurasa mpya kwa ajili ya mashirika mengine kuiga mfano huu. Tunakaribisha maombi ya mechi za kirafiki kutoka kwa timu mbalimbali maana sasa tumeiva vilivyo”, alisema Fred Kihwele ambaye ni Kocha wa timu ya Daraja FC baada ya mchezo huo.
Naye Kapteni wa timu ya Daraja, Longino alisema “mchezo ulikuwa mzuri licha ya kuwepo kwa mvua, tumeonyesha uwezo mkubwa wa kuhimili mchezo na tunataka kuendeleza viwango vyetu. Mchezo sio magoli kikubwa ni mahusiano”.
“Mchezo ulikuwa mzuri, tumecheza vizuri pamoja na kwamba tumefungwa na Daraja. Imekuwa ni nafasi nzuri ya kupata kufahamiana vizuri ili kuleta mahusiano mazuri baina yetu kama vijana”, alisema Frank, Kapteni wa timu ya CRDB tawi la Njombe."