Maandamano yalilengwa kuunga mkono hotuba hii ya JK.
Polisi wazuia maandamano ya kumuunga mkono JK
Imeandikwa na Hellen Mlacky
Tarehe: 16th March 2011
POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imesitisha maandamano ya Kamati ya Vijana ya Watanzania na Wapenda Amani (KVT) ya kuunga mkono hotuba ya Rais Jakaya Kikwete baada ya taarifa za uchunguzi kuonesha yatasababisha uvunjifu wa amani.
Badala yake, vijana hao wameruhusiwa kufanya mkutano wao wa hadhara leo kuanzia saa 9 alasiri katika viwanja vya Bakhresa ambako mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mwenyekiti wa TLP Taifa na Mbunge wa Vunjo, Augustino Mrema.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Kaimu Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Kamishna Msaidizi Fulgence Ngonyani alisema, walipokea barua ya maombi ya maandamano hayo Machi 11 kutoka KVT na lengo lao ni kuunga mkono hotuba ya Rais Kikwete.
Barua hiyo kwa mujibu wa Kamanda Ngonyani, ilieleza kwamba kaulimbiu ya maandamano hayo ni ‘Amani yetu bado tunaipenda’ na yalikuwa yaanze saa 4 asubuhi kutoka Mnazi Mmoja kupitia Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) na barabara ya Morogoro mpaka Manzese ambako mkutano huo utafanyika.
Kutokana na uchunguzi uliofanywa Jeshi hilo, imebainika kuwa maandamano hayo yana muitikio mkubwa wa watu hivyo yanaweza kusababisha msongamano mkubwa na kusababisha uvunjifu wa amani.
“Baada ya Polisi kupata taarifa ya maandamano hayo, tulifanya tathmini na kuamua kusitisha maandamano haya ...yanaweza kusababisha msongamano ambao ungetokana na kufungwa kwa barabara kwa muda mrefu na kusababisha kero kwa watumiaji wengi wa barabara hiyo,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu hatua hiyo kama ni ya kuwanyima vijana hao haki yao ya kimsingi ya kuandamana, Ngonyani alisema: “Uhuru wa Mtanzania usifikie mahali ukaingilia uhuru wa watu wengine na Polisi imeahidi kutoa ulinzi wa kutosha ili mkutano huo ufanyike kwa amani na utulivu.
Katibu Mwenezi wa KVT, Omari Genzeli aliyekuwepo katika mkutano huo, alisema maandamano hayo yalilenga kuunga mkono hotuba ya Rais na kupinga kauli za uchochezi zinazotolewa na Chadema na kwamba kusitishwa kwake wameona ni sawa kwa sababu lengo lao ni kutafuta amani na si vurugu.
Chanzo: Habari Leo