Adverts

Mar 10, 2011

Rais Kikwete awasili Mauritania kushiriki kikao cha Suluhu ya Ivory Coast

Rais Mohamed Ould Abdel Aziz wa Mauritania akimkaribisha Rais Jakaya Mrisho Kikwete muda mfupi baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Nouakchott tayari kushiriki katika kikao maalumu kinachojadili mchakato wa amani ya Ivory Coast. Rais Kikwete yupo katika kamati maalum ya marais wa nchi za Umoja wa Afrika (A.U) yenye lengo la kuleta suluhu ya mgogoro wa kisiasa nchini Ivory Coast.Marais wengine waliopo katika kamati hiyo ni Rais Jackob Zuma wa Afrika ya Kusini,Rais Blaise Compaore wa Burkina Fasso, Rais Idriss Deby wa Chad na Rais Mohamed Ould Abdel Aziz wa Mauritania ambaye ndiye mwenyekiti wa kamati hiyo.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete, Rais Jackob Zuma wa Afrika ya Kusini na Rais Balise Compaore wa Burkina Fasso wakiingia katika kikao maalum cha kamati ya Umoja wa Afrika (AU) yenye lengo la kutafuta suluhu ya mgogoro wa kisiasa wa Ivory Coast.Kikao hicho kilifanyika katika mji mkuu wa Mauritania Nouakchott
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Jopo la Marais waliopewa jukumu la kutafuta suluhu kwa mgogoro wa Ivory Coast, wanatarajia kufanya mkutano wao wa mwisho ambao utawajumuisha viongozi wawili wanaohasimiana katika mgogoro huo.
Hayo yameamuliwa katika kikao kilichojumuisha Marais kutoka Afrika Kusini, Burkina Faso, Chad, Mauritania, Tanzania na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) waliokutana Nouakchott, Mauritania jana tarehe 4 Machi, 2011.
Viongozi hao Jacob Zuma wa Afrika ya Kusini, Blaise Compaore wa Bukina Faso, Idris Deby wa Chad, Mohamed Ould Abdel Aziz wa Mauritania na Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania na Jean Ping, Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU, wameamua katika kikao chao kuwa watawaalika Bw. Laurent Gbagbo, Bw. Alassane Dramane Ouattara na Mwenyekiti wa Baraza la Katiba la Ivory Coast ili kuweza kuwakutanisha kwa mara ya kwanza na kujadiliana nao kuhusu mustakabali wa nchi yao.
Viongozi pia wanatarajia katika kikao kijacho kukabidhi ripoti yao kwenye Baraza la Ulinzi na Usalama la Umoja wa Afrika, iliyowapa kazi ya kutafuta suluhu katika kikao kilichofanyika mwishoni mwa Januari, mwaka huu.
Katika majukumu yao viongozi wa Afrika walikutana mara ya kwanza mjini Nouakchott tarehe 20 Februari kabla ya kuelekea Abidjan tarehe 21 na 22 Februari ambapo walikutana na viongozi hao wawili na kupata kusikiliza pande zote mbili zinazopingana, walifanya mazungumzo pia na Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo na Baraza la Katiba ili kupata hali halisi ya jinsi uchaguzi ulivyoendeshwa hadi matokeo ambayo yalipingwa na kusababisha viongozi wote wawili kujitangazia ushindi.
Akielezea zaidi makubaliano yaliyofikiwa katika kikao cha viongozi hao Rais Kikwete amesema wamezitaka pande zote mbili ziache kuhamasisha maandamano ambayo yanazidi kujenga chuki baina ya wananchi wake na pia kuvitaka vyombo vya habari vya Ivory Coast viache kupandikiza mbegu ya chuki katika jamii.
Katika taarifa yao ya pamoja, pamoja na wito huo kwa pande zote mbili kuacha kuhamasisha vurugu, viongozi wamesema wanasikitishwa sana na hali ya uvunjwaji wa amani na upotevu wa maisha ya watu na uharibifu wa mali unaondelea hivi sasa.
Rais Kikwete anatarajiwa kurejea nyumbani leo tarehe 5 Machi, jioni.
Mwisho.
Imetolewa na Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
Mauritania.
4 Machi, 2011
"