Send to a friend |
Ramadhan Semtawa MBUNGE wa Maswa Mashariki (Chadema), John Shibuda, ameibuka na kutetea maandamano yanayofanywa na chama chake, huku akionya CCM kuacha kufanya kile alichokiita mchezo wa kugeuza polisi kuwa ‘ICU ya kutibu maradhi yake ya siasa za ufisadi. ICU ni chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum. Shibuda ambaye alijiunga na Chadema akitokea CCM ambako alitemwa kwenye mchakato wa kura za maoni mwaka jana, alitoa kauli hiyo baada ya kuwa kimya kwa muda, huku akikosekana katika maandamano ya chama chake yaliyofanyika mikoa ya Kanda ya Ziwa. Kukosekana kwa Shibuda katika maandamano na mikutano ya Chadema hata yalipotua mkoani kwake Shinyanga, kuliibua mguno wa chini chini miongoni mwa wapenzi na washabiki wa chama hicho. Akizungumza na Mwananchi juzi kuhusu hali ya siasa nchini ikiwamo maandamano hayo, Shibuda alisema licha ya kutoshiriki kutokana na matatizo ya kifamilia, anaona hatari kubwa inayokabili nchi kwa sasa ni ufisadi uliojikita ndani ya CCM unaochochea maisha magumu, dhuluma na wanyonge kupoteza haki. Akirejea historia ya msingi wa maandamano nchini tangu enzi za kudai uhuru wakati wa Baba wa Taifa, marehemu Mwalimu Julius Nyerere, Shibuda alisema ulilenga kuondoa dhuluma, ubwanyenye, wizi, unyonyaji na kila aina ya uporaji haki na rasilimali za nchi. Shinikizo kwa dola Shibuda alionya akisema: Mashinikizo ya CCM kwa vyombo vya dola ni ujenzi kwa jamii kuasi polisi. Polisi lisiwe barafu la kugandisha fikra za wananchi kudai utawala bora ili tu CCM iendelee kubaki na watu wabaki na fikra chakavu na mawazo mgando. Polisi liepushwe kuwa ICU ya wahanga CCM kutokana na uzembe na siasa zake za kifisadi." Mwanasiasa huyo mwenye kutumia tamathali za semi, alisema CCM wasigeuze polisi kuwa kama makaburu kwa kulivua sura yake ya uzalendo wa kusimamia usalama wa mali na raia. Mwishoni mwa wiki iliyopita, CCM kupitia kwa Katibu wake wa Itikadi na Uenezi, mwanajeshi mstaafu John Chiligati, ilitoa kauli inayovitaka vyombo vya dola kukibana Chadema kutokana na kile alichokiita ni mikutano na maandamano yanahatarisha amani nchini. Kauli ya Chiligati ilitanguliwa na onyo la Amiri Jeshi Mkuu, Rais Jakaya Kikwete, ambaye katika hotuba yake ya mwisho wa Februari mwaka huu alishutumu Chadema kwa kuhatarisha amani ya nchi kutokana na mpango wao ovu wa kutaka kumuondoa yeye (Rais) madarakani kwa njia zisizo halali. Mbali ya onyo hilo la Rais na Chilligati, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano wa Jamii), Steven Wasira na Mbunge wa Same Mashariki (CCM), Anne Killango Malecela nao wamejitosa kwa kutoa kauli za kuwalaani Chadema kwamba kinachochea vurugu nchini. Hata hivyo, Shibuda anayejifafanisha na gogo la udi katika duru za kisiasa, alisema kinachofanyika sasa ni kujenga mapinduzi ya kisiasa kwa kuleta mabadiliko ya kifikra yenye shabaha ya kujenga uongozi bora na siasa safi, kama ilivyosisitizwa wakati wa Mwalimu Nyerere na Tanu. "Naonya CCM, polisi lisivuliwe uzalendo wake wa kuwa nyenzo ya usalama wa raia na kuivisha ukaburu kwa kuziba ombwe na kukosekana nguvu za hoja kama mapigo ya kisiasa kupiku vyama vya upinzani," alisisitiza. Alisema ni dhahiri sasa CCM iliyopo inajitia kitanzi kutokana na kuegemea ubavuni mwa vyombo vya dola, vikisahau kufanyakazi ya siasa kwa kujisafisha. "CCM wanajitia kitanzi kwa kujiweka ubavuni mwa vyombo vya dola...hili ndio jeneza lao, kwani mwisho wa siku misumari ya jeneza lao ni kura za wananchi katika uchaguzi ujao," aliionya CCM. Kitendo hicho Shibuda alikiita sawa na fikra mgando na mawazo mpauko, huku akitoa mfano: "Kama ukiwa na nguvu kubwa ya dola halafu unataka usishindwe, basi ni dhahiri Marekani ingeweza kushinda kombe la dunia kila mwaka kwa sababu ina nguvu kubwa za kijeshi." |