Adverts

Apr 16, 2011

WANANCHI LINDI WAASWA WASIUZE ARDHI

Na Anna Nkinda – Maelezo,

Wenyeji wa mikoa ya Lindi na Mtwara wametakiwa kutouza ardhi yao kiholela kwa wageni badala yake waitumie ardhi hiyo kwa kilimo na shughuli zingine za maendeleo.

Wito huo umetolewa jana na mke wa Rais Mama Salma Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) wakati akiongea na viongozi pamoja na watendaji wa mikoa hiyo.

Mama Kikwete alisema kuwa mikoa hiyo imejaliwa kuwa na ardhi nzuri na yenye rutuba jambo ambalo linawafanya wageni wengi kukimbilia katika mikoa hiyo kwa nia ya kutaka kununua ardhi.

“Katika maeneo mengine watu wanagombania ardhi na kupata kipande kidogo cha ardhi ni kazi kubwa lakini ninyi mmejaliwa kuwa na ardhi nzuri, kubwa na yenye rutuba hivyo basi muitumie ardhi hii kuzalisha chakula”, alisema Mama Kikwete.

Aliendelea kusema kuwa mikoa ya Lindi na Mtwara imejaliwa kuwa na Gesi ya asili jambo ambalo si la kawaida katika maeneo mengine hivyo basi kama watauza ardhi wajue kuwa wageni watakuja na kunufaika na gesi hiyo kuliko wenyeji wa eneo husika.

Pia aliwataka viongozi hao kabla ya kusaini mikataba au kuingia katika makubaliano yoyote yale wasome kwa umakini mkubwa nyaraka wanazopewa ili mikataba hiyo isije ikaleta matatizo siku za usoni.
Kwa upande wa madiwani alisema kuwa madiwani wananguvu sana katika maeneo yao ya kazi kwani bila Diwani kusema mambo hayaendi. Alitoa mfano kama kuna mradi wa kuchimba kisima wao madiwani wajiulize je thamani ya kisima ni sahihi?
Alimalizia kwa kuwasihi madiwani hao kutokubali kukosa vikao vya kazi labda wawe wagonjwa kwani kuwepo kwao katika vikao hivyo kuna umuhimu mkubwa.