Adverts

Jun 21, 2011

MBOWE AWAPANDISHA PRESHA WABUNGE WENZAKE- AANZA KWA KUKABIDHI SHANGINGI LAKE


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI:
KUHUSU BAJETI YA SERIKALI YA MWAKA 2011/2012:
Utangulizi.
Mnamo tarehe 21/06/2011 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha bajeti ya Makadirio na Matumizi ya Serikali kwa mwaka 2011/2012 .


Pamoja na Bajeti ya Serikali kukubali na kuzingatia baadhi ya hoja zilizotolewa na wabunge wa Kambi ya Upinzani na hususani CHADEMA kama vile ;
a) Kupunguza kodi na tozo mbalimbali kwenye mafuta ya petrol na dizeli.


b) Kupunguza kiwango cha faini za makosa ya barabarani kutoka shilingi 300,000/50,000 hadi kufikia ukomo wa shilingi 30,000.


c) Kufuta leseni za biashara kwenye Majiji,Halimashauri za Wilaya na Vijiji.
d) Kufuta misamaha ya kodi kwenye makampuni yanayotafuta mafuta na gesi Nchini.
e) Kuongeza pesa kwenye bodi ya Mikopo ya Elimu ya juu kwa kuhakikisha kuwa kodi ya skills development levy 2/3 inapelekwa kwenye bodi kwa ajili ya Mikopo.


Katika kupitisha bajeti hiyo wabunge wa Kambi ya Upinzani na hususani wa CHADEMA tuliamua kupiga kura za HAPANA kwenye mapendekezo hayo ya Serikali kutokana na sababu mbalimbali na haswa hizi zifuatazo;
1. Serikali haikukubaliana na hoja yetu ya kuondoa posho za vikao (sitting allowances) kwenye mfumo wa malipo ndani ya serikali.
2. Serikali haikukubaliana na hoja yetu ya kuhakikisha kuwa magari yote aina ya “Mashangingi” yanayotumiwa na viongozi na watumishi wa umma yauzwe kwa mnada ndani ya miezi sita na viongozi hao wakopeshwe magari kwa ajili ya kufanya majukumu yao mbalimbali.
3. Serikali haikukubaliana na hoja yetu ya kufuta/kupunguza misamaha mikubwa ya kodi ambayo Makampuni ya Madini yanapata ili kuhakikisha kuwa serikali inapata mapato kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo.
4. Serikali imekataa kuingiza pensheni kwa ajili ya wazee wote nchini ya shilingi 20,000 kila mwezi ili kuweza kuwapunguzia ukali wa maisha wazee wetu .
5. Serikali imekataa Kufuta/kuondoa misamaha ya kodi kwa kipindi cha miaka 10 kwenye maeneo maalum ya uwekezaji (EPZ).
6. Serikali haikukubaliana na hoja yetu ya kuhakikisha kuwa tunapunguza gharama za safari na haswa kuhakikisha kuwa ni viongozi wakuu na wenzi wao tuu ndio waruhusiwe kusafiri kwa kutumia daraja la kwanza (first class) ambao ni ;
· Rais
· Makamu wa Rais
· Waziri Mkuu
· Spika
· Jaji Mkuu
Mawaziri wasafiri kwa kutumia daraja la pili (bussines class) na viongozi wengine wote wa umma na watumishi wa umma wakiwemo wabunge wasafiri kwa kutumia daraja la kawaida (economy class) .
Pia misafara ya viongozi wakuu ipunguzwe ili kupunguza gharama za kuhudumia misafara hiyo pindi wanaposafiri nje ya Nchi.

MH FREE MAN MBOWE-KIONGOZI WA KAMBI YA UPINZANI BUNGENI
 
 
Hitimisho.
  1. Tumeamua kumwandikia katibu wa Bunge barua ili aweze kutenganisha fomu kwa ajili ya mahudhurio na kwa ajili ya posho na wabunge wa CHADEMA hawatasaini fomu za posho.
  2. Kuhusu magari, kiongozi wa Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni (KUB) Mhe. Freeman Mbowe ameamua kurejesha gari yake aina ya “Shangingi” alilopewa na Bunge ili liwe la kwanza kupigwa mnada.
Tunawataka wabunge wengine waunge mkono hoja hizi kwa masilahi ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
Imetolewa na ;
………………………
Mhe. Freeman A. Mbowe (Mb),
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.
21 Juni 2011.
Kwa hisani ya Francis Godwin