Na Anna Nkinda
– Maelezo
7/6/2011
Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) kwa kushirikiana na mradi wa FHI PAMOJA
TUWALEE wamedhamiria kufanya kazi kwa pamoja kwa ajili ya
kuwakomboa watoto yatima wa Tanzania.
Hayo yamesemwa
hivi karibuni na Mke wa Rais ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya WAMA Mama
Salma Kikwete wakati akipokea taarifa ya kuutambulisha
mradi wa FHI PAMOJA TUWALEE katika ofisi za WAMA zilizopo jijini Dar es Salaam.
Mama Kikwete alisema kuwa kwa kuwa malengo
ya kazi ya taasisi zote mbili yanashahabiana ya kuwasaidia watoto yatima hivyo
basi watafanya kazi kwa pamoja ili kuhakikisha kuwa watoto hao wanasaidia na
kuishi katika mazingira mazuri.
“Lengo kubwa la
Taasisi zetu ni kuhakikisha kuwa mtoto yatima hanyanyaswi wala kubaguliwa na
jamii inayomzunguka bali anaishi maisha mazuri, anapata elimu bora ambayo
itamsaidia katika maisha yake”, alisema Mama Kikwete.
Akisoma
taarifa ya mradi huo Priskila Gobba ambaye ni Mkurugenzi wa mradi alisema kuwa
lengo kubwa walilo nalo ni kuboresha hali ya maisha ya watoto walio katika
mazingira hatarishi na kaya zao kwa kuwajengea uwezo wana kaya na jamii ili
watoe huduma kamilifu, bora na endelevu.
Gobba anasema,
“Tumeamua kufanya kazi ya uhamasishaji na utetezi wa haki za watoto na WAMA
kwani taasisi hii imekuwa ikiwasaidia watoto wenye mahitaji mbalimbali hapa
nchini.”
Aliendelea
kusema kuwa wamekuwa wakiwajengea uwezo watoto hasa wasichana ili wawe na
ujasiri wa kujimudu kwa kuimarisha uwezo wao wa kuhimili athari za matukio
mabaya yaliyowakuta, kujitunza, kujilinda na kujitosheleza kimaisha.
PAMOJA TUWALEE
ni mradi ambao unafadhiliwa na Serikali ya Marekani kupitia ofisi
ya Shirika lao la Maendeleo la hapa nchini (USAID
Mission/Tanzania) na unafanya kazi zake katika wilaya 25 zilizoko
kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro na
Zanzibar.
Mwisho.