DUA za watanzania zimeelekezwa kwa timu ya wanawake Tanzania 'Twiga Stars' ambayo inataraji kushambulia uwanjani kesho (Julai 7) kuwakabili wenyeji
Zimbabwe 'Mighty Warriors' katika mechi ya pili ya nusu fainali ya michuano ya
Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Kusini mwa Afrika (COSAFA) itakayochezwa
Uwanja wa Rufaro, jijini hapa.
Mechi ya Twiga Stars itachezwa saa 9.15 kwa saa za hapa (saa 10.15 kwa saa za
Tanzania), wakati nusu fainali ya kwanza kati ya Afrika Kusini 'Banyana Banyana'
dhidi ya Malawi itaanza saa 6.30 mchana kwa saa za hapa.
Twiga Stars inayoongozwa na nahodha wake Sophia Mwasikili imefanya mazoezi
mepesi leo asubuhi kwenye Uwanja wa Rufaro kujiweka tayari kwa ajili ya pambano
hilo ambalo tayari limekuwa gumzo kwa mashabiki wa hapa.
Akizungumza baada ya mazoezi , Kocha Mkuu wa Twiga, Charles Mkwasa amesema
Zimbabwe ni
timu nzuri lakini amekiandaa kikosi chake kwa ajili ya kuibuka na ushindi ili
kiweze kucheza nusu fainali na hatimaye kunyakua kombe hilo.
'Zimbabwe watakuwa na faida ya kucheza mbele ya mashabiki wao. Kwa kawaida
wanamtegemea yule mshambuliaji wao mrefu wa kati (Rufaro Mutyavaviri) huku
wakitumia sana wingi ya kulia. Nimewaandaa wachezaji wangu kwa hilo.
'Kikosi hakitakuwa na mabadiliko ambapo Ettoe Mlenzi aliyekuwa na kadi mbili za
njano atarejea uwanjani. Mabadiliko yatakuwa kwa beki wa kushoto ambapo kwenye
mechi ya Zimbabwe ataanza Fatuma Khatibu,' amesema Mkwasa ambaye timu yake
imeingia katika michuano hiyo ikiwa mwalikwa kwa vile si mwanachama wa COSAFA.
Mutyavaviri ndiye anayeongoza katika ufungaji katika michuano hiyo ambapo kwenye
mechi kati ya timu yake na Malawi alifunga mabao matano. Mighty Warriors
ilishinda mabao 8-2 na mshambuliaji huyo amekuwa akifunga katika kila mechi.
Twiga Stars ni miongoni mwa timu ambazo tangu awali zilikuwa zikipewa nafasi ya
kutwaa ubingwa kutokana na kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika
zilizofanyika mwishoni mwa mwaka jana nchini Afrika Kusini. Nyingine ni wenyeji
Mighty Warriors na Banyana Banyana ambazo zote zimefuzu kwa hatua ya nusu
fainali.
Wachezaji watakaonza kwa Twiga Stars katika mechi ya kesho ni Fatuma Omary,
Fatuma Makusanya, Fatuma Khatibu, Sophia Mwasikili, Mwanaidi Tamba, Mwajuma
Abdallah, Mwanahamisi Omary, Ettoe Mlenzi, Fatuma Mustafa, Asha Rashid na
Fadhila Kigalawa.
Twiga Stars imekuwa ikishangiliwa kwa nguvu na Watanzania wanaoishi hapa
wakiongozwa na Balozi Adadi Rajab ambaye ameshuhudia mechi zote za timu hiyo.
Mechi kati ya Twiga Stars na Mighty Warriors itaoneshwa moja kwa moja (live)
kupitia SuperSport 4 na Shirika la Utanganzaji la Zimbabwe (ZBC). Fainali na
mechi ya kutafuta mshindi wa tatu (classification) zitachezwa Julai 9 mwaka huu
kwenye Uwanja wa Rufaro.
Timu ambazo zimeaga mashindano baada ya kushindwa kufuzu kwa hatua ya nusu
fainali jana ni Botswana, Zambia, Lesotho na Msumbiji.
Boniface Wambura
Ofisa Habari TFF
Harare
"