Adverts

Aug 20, 2011

MADIWANI MANISPAA YA SONGEA WAMWEKA PABAYA MKURUGENZI

Kushoto ni Katibu wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Faustine Mhagama akibadilishana mawazo na Mwenyekiti wa Mafunzo na Maadili ya Waandishi wa Habari Tanzania Juma Nyumayo (katika) kushoto Mwenyekiti wa Mtaa wa Namanyigu kata ya Mshangano Fidolin Malindisya baada ya kutoa tamko lake mbele ya waandishi wa habari la kumtaka Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Zakaria Nachoa kuheshimu maamuzi ya vikao halali vya Madiwani na vya kata hiyo kuhusu mgogoro wa Ardhi unaoendelea mjini humo
MADIWANI wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea wamemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Zakaria Nachoa kuacha mara moja kulumbana na wananchi wa kata ya Mshangano na Kampuni ya Ardhi Plan kwa maslahi yake binafsi

Mwandishi wa mtandao huu wa www.francisgodwin.blogspot.com Stephano Mango anaripoti kutoka Ruvuma kuwa akisoma tamko hilo kwenye ukumbi wa Better Life Tanzania mjini mbele ya waandishi wa habari Katibu wa Madiwani wa Halmashauri hiyo ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mshangano Faustine Mhagama alisema kuwa wanashangaa na tabia ya Mkurugenzi huyo kukaidi maagizo halali ya vikao na kuwasumbua wananchi kwa maslahi yake

Mhagama alisema kuwa idara ya ardhi ya Manispaa hiyo imekuwa kero kubwa sana katika upangaji wa mji na uendelezaji wa makazi kwa wananchi wake kutokana na urasimu mkubwa unaofanywa na viongozi wake

Alifafanua kuwa kila siku wananchi wanawalalamikia Madiwani kuhusu suala hilo hali ambayo inapelekea kuwa na adha kubwa kwa wananchi ambao wanataka kuendeleza maeneo yao

Alisema kuwa wananchi wa Kata ya Mshangano kwa ridhaa yao na kwa kushirikiana na viongozi wao wa Mitaa waliamua kuipa kazi Kampuni ya Ardhi Plan ili iweze kuwapimia maeneo yao kwa kuzingatia michoro ya Halmashauri

Alisema kuwa wananchi wa mitaa ya Namanyigu,Mshangano na Mitendewala waliamua kufanya mikutano ya hadhara na kuwaalika viongozi wa Kampuni hiyo ili waweze kukubaliana namna ya kufanikisha zoezi hilo

Alieleza kuwa baada ya wananchi kukubaliana na Kampuni walipeleka taarifa kwa Mkurugenzi wa Manispaa kwa taarifa na hatua zaidi lakini wanashangaa Mkurugenzi huyo ameshindwa kuwajibu wananchi na badala yake ameuzuia mchoro na kuinyima kibali Kampuni hiyo bila sababu za kimsingi

Alisema kuwa Manispaa imekithiri kwa vitendo vya kuwadhuluma wananchi ardhi katika maeneo yao jambo ambalo linasababisha wananchi wawe na maisha magumu kutokana na tama mbaya ya fedha ya viongozi wa idara ya ardhi ya Manispaa hiyo

Alibaisha kuwa Kampuni hiyo kwa kushirikiana na wananchi ambao ndio wenye ardhi pamoja na viongozi wa Serikali za Mitaa na Kata hiyo waliandaa mchoro mzuri na wa kisasa ambao maeneo muhimu kwa huduma za kijamii kama vile makanisa,misikiti,masoko,vituo vya mabasi,Zahanati na shule yametengwa

Alifafanua zaidi kuwa wananchi wamechoka na vitendo vya unyonyaji vinavyofanywa na Manispaa wananchi kwa umoja wao waliamua kwa dhati kuhihitaji Kampuni hiyo ili iweze kupima ardhi na maeneo yao ambayo yameendelezwa kiholela ili waweze kupata hatimiliki za maeneo hayo kwa lengo la kujikomboa kiuchumi kupitia ardhi yao kwa kupata mikopo kwenye taasisi za fedha

Alisema kuwa endapo Mkurugenzi ameshindwa kuheshimu matakwa ya wananchi wa Mshangano na maamuzi ya vikao halalibasi mkurugenzi huyo hatoshi na atakiwi kwa maslahi ya wananchi wa Manispaa hiyo

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mipango miji ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Matarawe akizungumza kwenye mkutano huo alisema kuwa Mkurugenzi huyo aliagizwa na Kamati yake katika kikao kilichoketi agosti 4 mwaka huu kuwa ifikapo tarehe 30 agosti mwaka huu kampuni hiyo iwe imeanza upimaji katika eneo la Mshangano

Makene alisema kuwa maagizo ya kikao chake ni halali kwa mujibu wa kanuni za Halmashauri hivyo yanapaswa yatekelezwa haraka kwa maslahi ya wananchi na sio ya mtu binafsi

Alieleza kuwa Halmashauri ya Manispaatangu ianzishwe mika 20 iliyopita imeweza kupima viwanja elfu 13 tu ambapo Kampuni ya Ardhi Plan ndani ya miezimitano imefanikiwa kupima viwanja elfu 16 na kwamba ina mpango wa kuchonga barabara katika maeneo yote ya kata ya Mshangano

Alisema kuwa kitendo cha Mkurugenzi kukaidi maagizo hayo kinaashiria kuwa kina mazingira ya ubabe na rushwa hivyo vikao vimemuagiza atoe haraka vibali ili Kampuni hiyo iweze kuwapimia wananchi maeneo yao vinginevyo Baraza la Madiwani la dharura litaitishwa kwa hatua zaidi dhidi ya Mkurugenzi huyo

Gazeti hili lilimtafuta Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Zakaria Nachoa ili kuweza kupata lolote kutoka kwake kuhusiana na tamko hilo alisema kuwa amelisikia tu lakini hajalipata kwa maandishi na kwamba yupo safarini kuelekea Dodoma kikazi