HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA
TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE,
KWA WANANCHI KUHUSU HALI YA UCHUMI NCHINI NA MCHAKATO WA KATIBA MPYA, TAREHE
17 NOVEMBA, 2011
Mheshimiwa
Mkuu wa Mkoa,
Mstahiki
Meya,
Viongozi
wa Serikali,
Wazee
wangu,
Ndugu
Wananchi,
Nakushukuru
Mkuu wa Mkoa na viongozi wenzako wa Jiji la Dar es Salaam kwa kuniandalia fursa
hii ya kukutana na Wazee wa Dar es Salaam.
Nawashukuru sana wazee wangu kwa kuitikia wito wangu huu wa kukutana
nanyi. Nimefarijika sana kwa mahudhurio
yenu makubwa pamoja na taarifa kuwa ya muda mfupi.
Nimewaiteni wazee wangu nizungumze
nanyi na kupitia kwenu nizungumze na wananchi wote wa Tanzania. Mwisho wa mwezi uliopita sikuweza kufanya
hivyo kupitia utaratibu wetu wa kawaida kwa sababu nilikuwa kwenye Mkutano wa
Jumuiya ya Madola nchini Australia. Mwisho
wa Mwezi huu nitakuwa Bujumbura kuhudhuria Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika
ya Mashariki, hivyo sitaweza kuongea na wananchi wakati huo. Lakini, yapo
masuala kadhaa ambayo ni muhimu watu kupata ufafanuzi kutoka kwangu. Kwa ajili hiyo nimeona nitumie fursa hii
kuzungumza nanyi siku ya leo. Leo
nataka kuzungumzia hali ya uchumi na mchakato wa kupata Katiba Mpya.
Hali ya Uchumi
Ndugu
Wananchi;
Katika kuelezea hali uchumi nchini,
naomba nianze kwa kuelezea hali ya uchumi duniani kwani yanayotokea nchini yana
uhusiano mkubwa na yanayotokea duniani. Hali
ya uchumi duniani siyo shwari. Ukweli ni
kwamba hali katika uchumi wa mataifa ya Marekani, Ulaya Magharibi na Japan
haijatengemaa kufuatia machafuko ya masoko ya fedha na mdororo wa uchumi wa
miaka miwili iliyopita. Hivi sasa uchumi
wa mataifa tajiri ya Ulaya , wanachama wa Umoja wa Ulaya na hasa wanachama wa
Umoja wa Sarafu ya Euro unapita katika kipindi kigumu na mashaka. Thamani ya sarafu hiyo inashuka na hata
kuaminika kwake ni kwa mashaka. Mfumuko wa bei umepanda, ukosefu wa ajira
umeongezeka na ipo hofu kubwa ya uchumi wa nchi hizo kudorora tena. Lakini nchi hizi ndiyo masoko makubwa ya
bidhaa zetu, watalii na bidhaa za viwandani.
Hivyo, athari zao zinatugusa na sisi.
Kuongezeka kwa mfumuko wa bei kunaongeza bei ya bidhaa tunazonunua
kutoka kwao. Aidha, kutetereka kwa
uchumi wao nako kumepunguza masoko ya bidhaa zetu.
Lakini
kulegalega kwa sarafu ya Euro kumesaidia kuimarika kwa sarafu ya dola ambayo
kabla ya hapo ilikuwa imepungua nguvu.
Kwa sababu hiyo thamani ya sarafu ya dola imepanda duniani
ikilinganishwa karibu na sarafu nyingine zote pamoja na yetu. Wakati huo huo bei ya mafuta imeendelea
kupanda duniani kutoka dola 76.1 kwa pipa Septemba,, 2010 hadi dola 100.5
Septemba, 2011. Jumla ya yote haya ni
kuongezeka kwa mfumuko wa bei kutoka asilimia 4.2 Oktoba, 2010 hadi asilimia
17.9 Oktoba, 2011.
Ndugu
Wananchi;
Serikali
na vyombo husika vimekuwa vinachukua hatua mbalimbali kukabiliana na matatizo
ya kushuka kwa thamani ya shilingi, bei ya mafuta, bei ya sukari na matatizo ya
umeme. Kuhusu kushuka kwa thamani ya
shilingi Benki Kuu imeendelea kuchukua hatua zilizopo ndani ya mamlaka yake
hususan kubana ulanguzi wa fedha za kigeni, kudhibiti matumizi ya fedha kigeni
kufanyia malipo hapa nchini na kuongeza fedha za kigeni katika masoko ya
fedha. Kwa kweli uwezo wao una
ukomo. Jawabu la uhakika lipo kwenye
uchumi wa mataifa makubwa kuchukua hatua thabiti kuimarisha uchumi wao ili
thamani ya dola irejee mahali pake stahiki na bidhaa zetu zipate masoko ya
uhakika na bei nzuri ili mapato yetu ya fedha za kigeni yaongezeke.
Kwa
upande wa mfumuko wa bei, ni vyema tukatambua kuwa Asilimia 75 ya ongezeko hili imetokana na kupanda kwa bei ya
chakula na mafuta. Asilimia 25 iliyobaki imechangiwa na sera
za fedha. Kwa upande wa mafuta,
tunaamini utaratibu wa kuagiza mafuta
kwa pamoja utasaidia kudhibiti bei za ndani za bidhaa hiyo. Aidha, itsaidia kupunguza makali ya athari ya
bei za dunia zinazopanda. Kwa upande wa
bei za vyakula, tatizo kubwa ni uhaba wa chakula katika nchi jirani
unaosababisha wote kututegema sisi na hivyo kupandisha bei nchini. Tunaendelea kudhibiti magendo ya chakula na
wakati huo kutengeneza taratibu rasmi za kuziuzia chakula nchi jirani.
Kwa
upande wa sukari tumeamua kuruhusu tani 120,000 ziagizwe ili kupunguza uhaba wa
bidhaa hiyo na kushusha bei yake.
Hatuko
Peke Yetu
Ndugu
Wananchi;
Ni vizuri
tukafahamu kuwa, matatizo ya mfumuko wa bei na kushuka kwa thamani ya fedha
yetu siyo yetu peke yetu. Nchi zote za
Afrika Mashariki zinakabiliana na matatizo haya. Kwa mfano, mfumuko wa bei
kwetu ni asilimia 17.9, Kenya
wako asilimia 18.9 na Uganda asilimia 30.5. Wakati mwaka wa jana sote tulikuwa kwa watani
karibu asilimia 5. Kwa upande wa kushuka kwa thamani ya shilingi
dhidi ya dola sote tumeathirika.
Shilingi ya Tanzania imeshuka kwa asilimia
9.4, Kenya kwa asilimia 6.8 na
Uganda kwa asilimia 17.4. Randi ya Afrika Kusini kwa asilimia 18.7, Rupia ya India kwa asilimia 9.8, Pauni ya Uingereza kwa asilimia 6.6. na Euro kwa asilimia 9.7.
Ndugu
Wananchi;
Katika
kukabiliana na tatizo la umeme, Serikali inaendelea kutekeleza mpango wa
dharura wa kuongeza uzalishaji wa umeme.
Serikali imewawezesha TANESCO kukodi mitambo ya kuzalisha umeme kutoka
kwenye makampuni ya Symbion (112 MW) na Aggreko (100 MW) na kununua mafuta ya
kuendeshea mitambo ya IPTL (100 MW).
Napenda
niwahakikishie wananchi kuwa, ifikapo Desemba, 2011 hali ya upatikanaji wa umeme
itakuwa nzuri na mgao utapungua sana baada ya kufunga mitambo mingine mipya ya
kuzalisha umeme ya TANESCO (160 MW) na Symbion (60 MW). Mikakati tuliyonayo ya muda mrefu ni kuongeza
mitambo zaidi na kuongeza upatikanaji wa gesi ya kuendeshea mitambo kwa kujenga
bomba kubwa la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam.
Mchakato
wa Katiba
Ndugu Wananchi;
Kama
mtakavyokumbuka tarehe 31 Desemba 2010 katika hotuba yangu ya kuuaga mwaka 2010
na kuukaribisha mwaka 2011 nilizungumzia maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanganyika
ambayo sasa ni Tanzania Bara tarehe 9 Desemba, 2011. Miongoni mwa mambo ambayo niliyataja kuwa
tutayafanya katika kusherehekea siku hiyo adhimu ilikuwa ni kuanzisha mchakato
wa kuitazama upya Katiba ya nchi yetu kwa nia ya kuihuisha ili hatimaye tuwe na
Katiba mpya.
Nilifafanua
siku ile kwamba tunataka kufanya hivyo si kwa sababu Katiba yetu ya sasa ni
mbaya, la hasha! Nilieleza kwamba Katiba
yetu ya sasa ni nzuri na imelilea vyema taifa letu. Tuna nchi yenye amani, utulivu na umoja pamoja
na watu wake kuwa wa rangi, makabila, dini na itikadi mbalimbali za
kisiasa. Tunayo nchi ambayo imepiga
hatua kubwa sana ya maendeleo ukilinganisha na ilivyokuwa miaka 50
iliyopita. Pamoja na hayo tunataka
kuihuisha Katiba yetu ili tuwe na Katiba inayoendana na Tanzania ya miaka 50
baada ya Uhuru wa Tanzania Bara, Tanzania ya miaka 47 ya Mapinduzi Matukufu ya
Zanzibar na Tanzania ya miaka 47 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Kwa
ajili hiyo nilielezea dhamira yangu ya
kuunda Tume Maalum ya Katiba yaani Constitutional Review Commission
itakayojumuisha Watanzania wa makundi mbalimbali katika jamii yetu na kutoka
pande zetu mbili za Muungano. Aidha,
nilifafanua kuwa jukumu la msingi la Tume hiyo litakuwa ni kuongoza na kuratibu
mchakato wa kupata maoni ya Watanzania kuhusu nini wanachokitaka kiwemo katika Katiba
yao.
Tume
itasikiliza maoni hayo na baadaye kutengeneza rasimu ya Katiba mpya ambayo
baada ya kukubaliwa na Bunge itafikishwa kwa wananchi kutoa ridhaa yao kwa
kupiga kura. Nilisisitiza kuwa mchakato
huo utawahusisha Watanzania wote wa ngazi zote na popote walipo mijini na
vijijini. Hapatakuwa na aina yoyote ya kuwabagua watu kwa itikadi zao za siasa,
shughuli wazifanyazo, dini zao, rangi zao au jinsia zao.
Ndugu
Wananchi;
Nilifarijika
sana na kauli za pongezi kwangu na kwa Serikali kwa uamuzi wa kuanzisha
mchakato wa kupata Katiba mpya. Miongoni
mwa waliotoa pongezi alikuwa Ndugu Freeman Mbowe, Mbunge wa Hai na Mwenyekiti
wa CHADEMA ambaye wakati akichangia
hotuba yangu ya kufungua Bunge Jipya, tarehe 11 Februari, 2011; nanukuu Hansad
ya Bunge aliposema “Mheshimiwa Spika, ninapenda kwenye hili, nimpongeze Rais kwa kuwa
msikivu, na Rais anapofanya jema tutampongeza, Serikali yake inapofanya
jema tutaipongeza na Chama chochote kitakapofanya jambo jema kwa Taifa letu,
tutakipongeza. Napenda kumpongeza
Mheshimiwa Rais kwa sababu moja ya msingi sana, kuridhia mabadiliko au
kuitafuta upya Katiba ya nchi yetu.”
mwisho wa kunukuu. Lakini siku chache baadaye Chama chake kikaja
na msimamo tofauti, wakawa wanalalamikia kunyang’anywa hoja yao na kukataa Rais
asiunde Tume ya Katiba na wala asihusike kabisa na mchakato huu. Tangu wakati huo wameendesha kampeni kubwa ya
kutaka Rais asihusishwe kwenye mchakato wa kubadili Katiba
Kwa kweli watu wengi wanaoitakia mema nchi
yetu walishangazwa na madai hayo na vitendo vya ndugu zetu hao. Hii si mara ya kwanza kwa nchi yetu kufanya zoezi
la marekebisho ya Katiba au hata kuandika upya Katiba tangu Uhuru na
Muungano. Mara zote hizo iliundwa Tume
ya kukusanya maoni ya wananchi ambayo iliundwa na Rais. Ndivyo ilivyokuwa wakati wa Rais wa Kwanza,
Mwalimu Julius Nyerere, Rais wa Pili,
Mzee Ali Hassan Mwinyi na Rais wa tatu Mzee Benjamin Mkapa. Mwalimu Julius Nyerere alifanya hivyo mara
tatu. Mara ya kwanza mwaka 1963 wakati
wa kubadilisha mfumo wa vyama vingi kwenda Chama kimoja, Rais aliunda Tume ya
Mheshimiwa Rashid Kawawa, Amon Nsekela.
Mara ya pili wakati wa kutengeneza Katiba ya Kudumu ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ya mwaka 1977 aliunda Tume ya Mzee Sheikh Thabit Kombo.
Mwaka
1984 Mabadiliko ya Katiba ya 1977 yaliyoweka ukomo wa Urais na kuingiza katika
Katiba Haki za Binadamu, yaliyotokana na mchakato uliokuwa ni wa Kichama,
ambapo CCM ilikusanya maoni kupitia mtandao wa kichama kuanzia Matawi hadi kufikia
Makao Makuu. Wakati wa Rais Ali Hassan
Mwinyi wa Awamu ya Pili, kulikuwa na Tume ya Jaji Mkuu Francis Nyalali
iliyotuletea mabadiliko ya nane ya Katiba yaliyoruhusu vyama vingi
vya siasa. Wakati wa Rais wa Awamu ya
Tatu, mzee Benjamin Mkapa kuliundwa Tume ya Jaji Kisanga iliyoleta mabadiliko
ya 13 na 14 ya Katiba ya nchi.
Hivyo
la ajabu lipi kwa Rais wa sasa kuunda Tume ya Katiba? Amepungukiwa nini Kikatiba na Kisheria ambacho
Marais wenzake walikuwa nacho katika madaraka yao? Hakipo hata kimoja! Madaraka waliyokuwa nayo Marais
waliomtangulia ndiyo aliyonayo Rais wa sasa.
Hajapungukiwa chochote kwa mujibu wa Katiba na Sheria za nchi. Kwa kweli hakuna hoja yoyote ya msingi ya
kumuengua Rais katika mchakato wa kutengeneza Katiba ya nchi. Haipo hoja ya Kikatiba wala ya Kisheria. Hivi Rais asipounda Tume, nani aiunde Tume
hiyo? Na huyo atakayeunda atapatikanaje?
Juzi
Bungeni msemaji wa kambi ya upinzani, katika mjadala wa Muswada wa Kuunda Tume ya Kukusanya Maoni alisema Rais ni dikteta. Ama kweli “akutukanae hakuchagulii tusi” kama ulivyo msemo wa Kiswahili. Hivi mimi kweli ni dikteta? Kwa jambo lipi? Hivi ndugu zangu Rais dikteta anatoa uhuru
mkubwa kama uliopo sasa wa vyombo vya habari na wa watu kutoa maoni yao? Kama mimi ningekuwa dikteta kweli nina hakika
hata yeye asingethubutu kusema hivyo na kama angethubutu basi mpaka sasa asingekuwa
anatembea kwa uhuru. Mimi ninachofahamu
ni kuwa nasemwa kwa kuwapa watu, vyama vya siasa na vyombo vya habari uhuru
mkubwa mno ambao watu wanaona unatumika vibaya kusema maneno yasiyokuwa na
staha au hata matusi, fitina na kupandikiza chuki katika jamii. Labda, nijaribu kuwa dikteta kidogo watu
waone tofauti yake. Naamini kungekuwa na
malalamiko makubwa zaidi ya haya.
Ndugu
Wananchi;
Mimi
na wenzangu Serikalini tumefanya yote ambayo Katiba ya nchi na Sheria
vinaruhusu. Ndivyo Marais
walionitangulia na Serikali zao walivyofanya tena sisi tumefanya zaidi ya wao. Wote waliunda Tume za kukusanya maoni ya Katiba
na wakati wa Mwalimu Julius Nyerere liliundwa Bunge Maalum la Katiba
lililojumuisha Wabunge na wananchi wengine kama tulivyoamua kufanya sisi. Ilifanyika hivyo wakati wa kutengeneza Katiba
ya Tanganyika kuwa Jamhuri na Katiba ya Kudumu ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka
1977. Sisi tulichofanya cha ziada ni kulihusisha
Bunge kutunga Sheria ya Kuunda Tume ya kusimamia mchakato wa Katiba mpya na
vile vile kuwapa wananchi wote ridhaa ya kuamua kwa kuipigia kura Katiba
inayopendekezwa. Ni kutokana na nyongeza
hii ndipo tukaona busara ya kuwepo kwa Sheria maalum ya kuongoza mchakato wa
kupata Katiba mpya. Tumepanua demokrasia
na kuwahusisha wananchi wenyewe siyo tu katika kutoa maoni bali pia kutoa
uamuzi wa mwisho kuhusu Katiba ya nchi yao, badala ya kuwaachia Wabunge na
viongozi wengine Serikalini peke yao.
Kwa kweli tunastahili pongezi badala ya shutuma na lawama zisizokuwa na
msingi.
Pia
inasikitisha kuona au kuwasikia watu wanaojua wakijifanya ukweli huu hawaoni
au hawajui. Baya zaidi ni pale wanapojihusisha na
kupotosha ukweli na kuipaka sura isiyokuwa ya kweli kuhusu kinachofanywa na
Serikali. Mimi hujiuliza kwa nini
wanafanya hivi. Kwa nini wanafanya
hiyana ya upotoshaji wote huu? Kwa kweli
sipati majibu ya uhakika. Labda ndiyo
ile dhamira ya kutaka nchi isitawalike.
Au ndiyo pengine ni ile nia ya kutaka kwenda Ikulu kwa njia ya
mkato. Ati kwa kutumia nguvu ya
umma. Basi hata hiyo nguvu unaitumia
bila ya kuwa na hoja za kweli?
Ndugu
Wananchi;
Nayasema haya kwa sababu kumekuwepo na
upotoshaji mkubwa wa jambo hili tangu baada ya hotuba yangu ya tarehe 31
Desemba, 2010 mpaka wakati wa kuwasilishwa kwa Muswada wa Sheria wa Kuunda Tume
ya Mabadiliko ya Katiba uliomalizika leo Bungeni. Upotoshaji wa kwanza ulikuwa ni ule wa
kujenga dhana kana kwamba Serikali imewasilisha Muswada wenyewe wa Katiba
mpya. Wapo watu wamefanywa waamini hivyo
wakati si kweli hata kidogo. Huu ni
Muswada ambao ukipitishwa, itaundwa Tume ya kukusanya maoni ya wananchi kuhusu nini
wanachokitaka kijumuishwe katika Katiba yao mpya. Kwa maneno mengine, maoni yenu mtakayoyatoa wananchi
kwa Tume ndiyo yatakayotumika kutengeneza Katiba mpya.
Ndugu
Wananchi;
Katika
Muswada huu kuna mambo tuliyotaja kuwa ni ya msingi ambayo yamewekewa wigo wa
kuhakikisha yanalindwa. Mambo hayo ni
yale ambayo yanalitambulisha taifa letu na tunu zake kuu. Mambo yenyewe ni haya yafuatayo: Kuwepo kwa nchi yetu na mipaka yake; kuwepo
kwa Serikali, Bunge na Mahakama; kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
kuwepo kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar; umoja wetu, mshikamano wetu na usalama
wetu; Mfumo wa uchaguzi kwa kura unaotoa fursa kwa wote; Hifadhi ya haki za
Binadamu; Haki za watu; Usawa mbele ya sheria na haki; Uhuru wa kuabudu na
kuvumiliana kwa imani zetu.
Kumekuwepo
na upotoshaji ati huko ni kuwaziba watu midomo.
Siyo hivyo hata kidogo. Mambo
hayo yanajadiliwa, lakini siyo kwa nia ya kuyaondoa bali kuboresha. Kwa mfano, kuhusu Muungano, tunachosema ni kwamba hatujadili kuwepo au
kutokuwepo kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, bali namna bora ya kuendesha
shughuli za Muungano wetu. Lakini,
tulichokifanya siyo kitu kigeni, hata Rais wa kwanza alifanya hivyo mwaka 1963
alipounda Tume ya Mfumo wa Chama Kimoja cha Siasa iliyoongozwa na Mheshimiwa
Rashid Kawawa. Alitoa mwongozo na
aliyataja mambo ya kulinda. Sisi
tulichokifanya ni kuyataja kwenye sheria badala ya kuwa Mwongozo wa Rais.
Ndugu
Zangu, Watanzania Wenzangu;
Kwani Katiba ya Nchi ni kitu
gani. Katiba hutaja nchi na mipaka
yake. Kwetu sisi nchi yenyewe ni Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania inayotokana na kuungana kwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar
na Jamhuri ya Tanganyika. Pili, Katiba
inaelezea jinsi nchi hiyo itakavyoendeshwa kwa maana ya mihimili mikuu mitatu
ya dola ya Utawala/Serikali, Bunge na Mahakama.
Katiba inafafanua jinsi Serikali inavyopatikana, muundo wake na
inavyofanya kazi.
Aidha,
inaeleza jinsi Bunge linavyopatikana, jinsi linavyofanya kazi ya kutunga sheria
na mahusiano yake na mihimili mingine.
Vile vile, Katiba inaeleza jinsi Mahakama inavyofanya kazi ya kutoa
haki, muundo wake na jinsi Majaji na Mahakimu wanavyofanya kazi. Kwa kweli mchakato wote huu unahusu
hayo. Tunatakiwa kutoa maoni juu ya
namna gani bora zaidi na ikiwezekana namna mpya ya kuendesha shughuli za Muungano
wetu na jinsi mihimili yetu inavyopatikana na kufanya shughuli zake.
Ndugu
Wananchi;
Jambo lingine lililopotoshwa ni dhana
ya muswada kusomwa mara ya kwanza. Kwa
mujibu wa utaratibu wa kutunga sheria, Miswada, husomwa mara tatu Bungeni. Muswada kusomwa mara ya kwanza ni pale
unapogawiwa kwa Wabunge baada ya kuchapishwa katika gazeti la Serikali siku 21
kabla ya kuwasilishwa Bungeni. Baada ya
kuchapishwa, hugawiwa kwa Wabunge.
Muswada husomwa mara ya kwanza Bungeni ili kutoa fursa kwa Mheshimiwa
Spika kuwasilisha Muswada huo kwenye Kamati iuchunguze na kuutolea maoni. Mheshimiwa Spika anaweza pia kuielekeza
Kamati kutafuta maoni ya wananchi.
Baada
ya Kamati kukamilisha kazi yake, Muswada husomwa mara ya pilli ambapo
Muwasilishaji atatoa hoja kwamba Bunge liujadili Muswada pamoja na kutoa maelezo
ya Muswada. Mjadala huanza kwa Kamati ya
Bunge kutoa maoni yake ikifuatiwa na maoni ya
Kambi ya Upinzani. Wakati Kamati ya
Bunge inapojadili Muswada, Waziri mhusika huwepo na mara nyingi maoni ya Kamati
ya Wabunge na wadau hujumuishwa wakati Waziri anapowasilisha hoja Bungeni ya
Muswada unaposomwa mara ya pili. Baada
ya mjadala, Bunge hukaa kama Kamati ya Bunge zima ambapo hupitia Muswada
kifungu kwa kifungu.
Katika
hatua hii Wabunge huweza kupendekeza mabadiliko mahsusi kwenye kila kifungu. Aidha, Waziri nae anaweza kutetea marekebisho
ya Muswada. Baadaye Bunge hurejea, taarifa
ya Kamati ya Bunge zima hutolewa kwamba Muswada umepitiwa kifungu kwa kifungu
na kukubaliwa. Kisha Muswada husomwa
mara ya tatu kuashiria kwamba Muswada umepitishwa. Mara nyingi Muswada hutokana na majadiliano katika
hatua hizi zote, mabadiliko hufanywa na wakati mwingine mabadiliko huwa makubwa kiasi kwamba kufanya Muswada uliochapishwa na kusomwa mara ya
kwanza na ule uliokubaliwa mwishoni uwe tofauti kabisa.
Ndugu
Wananchi;
Muswada huu ulisomwa mara ya kwanza
mwezi Aprili na kupelekwa kwenye Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala mwezi
Aprili, 2011. Tangu wakati huo Kamati
imekuwa ikiufanyia uchunguzi Muswada huo na kukusanya maoni ya wadau. Walisikiliza wadau Dodoma, Dar es Salaam na
Zanzibar pamoja na kufuatilia maoni ya makongamano, magazetini na kwenye
mitandao. Kisha Kamati ikayajadili na
kutoa mapendekezo yake ambayo Serikali iliyasikiliza na kuyajumuisha wakati
uliposomwa mara ya pili. Muswada huu
haukuwahi kuondolewa Bungeni. Kwa sababu
hiyo, hakuna sababu ya kurudia kusomwa mara ya kwanza kwa mujibu wa taratibu za
kuendesha Bunge.
Tukumbuke
kwamba baadhi yao waliahidi kwamba wangetoa Katiba Mpya katika siku mia moja tu. Serikali imechukua miezi kumi na mmoja na wanalaumu
kwamba eti inawahisha mchakato!! Hiyo
Katiba ya siku mia moja sijui wangeipataje bila kuwashirikisha wananchi?
Ndugu
Wananchi;
Ni
kutokana na hoja hizo Spika akaamua Muswada uendelee kujadiliwa na Bunge na leo
Bunge limeupitisha Muswada huo. Baadae
Muswada utaletwa kwangu kwa ajili ya kutiwa saini uwe Sheria. Baada ya hapo itabakia kazi yangu na Rais wa
Zanzibar kuunda hiyo Tume ili mapema mwakani kazi ya kukusanya maoni ya
wananchi ianze. Lengo letu ni kuwa
ifikapo mwaka 2014 zoezi zima liwe limekamilika ili mwaka 2015 tufanye uchaguzi
tukiwa na Katiba mpya. Itapendeza
tukisherehekea miaka 50 ya Muungano na Katiba mpya. Ni matumaini yangu kwamba wananchi wote
watashiriki kwa ukamilifu kutoa maoni yao kwa Tume hiyo.
Ndugu Wananchi;
Nimechukua
muda wenu mwingi kuyafafanua masuala haya kwa umuhimu wake. Nia ni kutaka watu waelewe maoni ya upande wa
Serikali. Matatizo ya kiuchumi yanayotukabili
tunaendelea kuyashughulikia. Yale yaliyo
kwenye uwezo wetu tutayamaliza na yale yaliyo nje ya uwezo wetu tutaendelea
kuchukua hatua za kupunguza makali.
Aidha, tutaendelea kutoa wito kwa mataifa husika kuchukua hatua thabiti
kutatua matatizo yao kwani tunaoumia ni wengi.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa
mchakato wa kupata Katiba mpya nawasihi Watanzania tujiandae kwa maoni ya kutoa
kwenye Tume ya Katiba mara itakapoanza kazi.
Kwa wale ambao hawatapata walichokitaka nawaomba warudi kundini, sote
tuungane kwa hatua inayofuata. Najua
wanayo maoni mengi mazuri wayatayarishe na kuyawasilisha kwa Tume
itakayoundwa. Njia ya maandamano na
vurugu si ya busara kufuata. Haijengi
bali inabomoa, haina faida bali hasara nyingi, haina faraja bali machungu kwa
pande zote. Busara ituongoze sote
kuchagua njia inayojenga, yenye faida, furaha na faraja kwa wote. Tutofautiane bila kupigana. Serikali itaendelea kutekeleza wajibu wake wa
kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa nchi ya amani na utulivu.
Mwisho
Ndugu Wananchi,
Naomba
nimalizie kwa kuwashukuru wananchi kwa kuwa na subira kwa kipindi chote hiki
toka tutangaze nia yetu ya kuanza mchakato wa kupata Katiba mpya. Kwa mara nyingine tena nawaomba mjiandae
kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kupata Katiba mpya mara utakapoanza ili
tuendelee kuijenga na kuiendeleza nchi yetu na vile vile tuendelee kuithamini
na kuitunza amani ya nchi yetu.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Asanteni sana kwa kunisikiliza!