::Mama wa jamii ya wafugaji wa eneo hilo akiwa na watoto wake watano, huku mmojawapo akipatiwa dawa ya minyoo..
:Bibi wa jamii ya wafugaji wilayani Iramba, akiwa na mjukuu wake alipompeleka kwenye chanjo, na kupatiwa matone ya vitamini A,katika zoezi la chanjo kitaifa lililomalizika novemba 116,mwaka huu.
Singida
JAMII ya Wahadzabe katika kitongoji cha Kipamba,wilaya Iramba,mkoa wa Singida, wamejitokeza kushiriki chanjo ya surua,polio,vitamin A na dawa za minyoo.
Hali hiyo ni tofauti ikilinganishwa na miaka ya nyuma, ambapo walikuwa wakikimbilia porini kila zoezi hilo lilipokuwa likifanyika.
Katika zoezi hilo lililokamilika novemba 16,mwaka huu nchini pote, watoto 86 wa jamii hiyo na wafugaji wanaoishi kwenye kitongoji hicho walikuwa wamechanjwa.
Kitongoji hicho kipo upande wa mkoa wa Singida, mpakani na mikoa mingine ya Manyara na Arusha, na huduma hiyo ilitolewa na timu ya wataalamu wa afya,kutoka hospitali ya wilaya ya Iramba.
Mganga mkuu wa wilaya ya Iramba Dk.Doroth Kijugu, alisema mafanikio hayo, yametokana na ushirikiano baina ya pande hizo mbili, ambapo sasa jamii hiyo imeanza kujenga imani kuhusiana na tiba za kisasa.
Aidha Dk.Kijugu aliahidi kuwa idara ya afya wilayani humo, itaendelea kuwa karibu zaidi na jamii hiyo, kwa kuhakikisha wanapata tiba sahihi, ili kuwaepusha na matumizi ya dawa walizozizoea, za mizizi na magamba ya miti.