Adverts

Jan 3, 2012

BASI LA UPENDO TRAVELLER LA IRINGA LAPINDUKA NA KUUA WAWILI MOROGORO

Askari wa Usalama Barabarani wakichukua maelezo toka kwa majeruhi hospitali ya mkoa wa Morogoro jioni hii
Majeruhi wakifikishwa hospitali ya mkoa Morogoro
Picha na Habari na John Nditi, Morogoro.
ABIRIA wawili wamefariki dunia papo hapo na wengine 29 kujeruhiwa na baadhi yao kulazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, baada ya basi la Upendo ‘Travel Coach’ walilokuwa wakisafiria kutoka Mkoani Dar es Salaam kwenda Iringa kupinduka eneo la Doma , Wilaya ya Mvomero, Barabara kuu ya Morogoro- Iringa.
Ajali hiyo ilitokea majira ya saa 10 jioni ya leo Januari 3, mwaka huu eneo la Kijiji cha Doma, Wilaya ya Mvomero, katika barabara kuu ya Morogoro – Iringa kwa kuhusisha basi lenye namba za usajili T 510 AMZ aina ya Scania.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Adolfina Chialo, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo , ambapo chanzo chake ni baada ya lori lililokuwa likitaka kulipita jingine kutaka kugongana uso kwa uso na basi hilo, kitendo kilichomfanya derava wa basi kulikwepa na hatimaye kupinduka.
Hata hivyo alisema, maiti moja imetambuliwa kwa kina la Hamis Ramadhani Mbwana ( 26) mkazi wa Handeni Mkoani Tanga ,alitambuliwa baada ya kupekuliwa nguo alizovaa na kukutwa leseni yake ya Uderava ikiwa na jina hilo.
Kwa mujibu wa Kamanda huyo, maiti nyingine ambayo ni ya mwanaume bado haijatambuliwa na umehifadhiwa Chumba cha maiti cha Hosipitali ya Mkoa huo ikisubiri kutambuliwa.
Hata hivyo karibu majeruhi wengi walikuwa walikuwa ni wanafunzu wa Vyuo, Shule za Sekondari na Msingi , ambao walikuwa wakirejea kwenye maenao yao baada ya kumalizika kwa sikukuu ya Krismasi na Mwaka mpya.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya majeruhi wa ajali hiyo, Firbert Nyoni , Maneno Abdallah , Aline Mhina pamoja na Salum Mfaume, walisema kuwa juhudi za dereva wa basi kulikwepa lori kiliwezesha
kuokoa maafa makubwa zaidi.
Kwa mujibu wa Mfaume aliyeunguzwa na maji la rejeta tumboni na mgongoni na kulazwa wadi ya majeruhu namba moja katika Hospitali hiyo , alisema , malori hayo yalikua wakifukuzana kwa mwendo kasi, na moja lilitaka kulipita jingine hali iliyosababisha kutaka kugongana basi hilo, ndipo Dereva alilikwepa na kusababisha basi kupunduka.
“ Juhudi za Dereva wa Basi ndizo zimewezesha kupunguza vifo na majeruhi…lakini wenye malori walikimbia baada ya sisi kupatwa na ajali hii…na mimi imeungua sana mgongoni na tumboni” alisema Majeruhi huyo. KUTOKA MICHUZI BLOG