· Waziri waghembe aambiwa Wizara imemshinda
· Serikali Mbeya yajitenga, yasema isiingiliwe
· Wakurugenzi wajitoa, wawaachia wanasiasa
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Mbozi mkoani hapa Aloyce Mdalavuma ambaye ni muhanga wa kura za maoni za Ubunge katika uchaguzi Mkuu 2010, amesema kuwa chama chake ni legelege ndiyo maana kimeunda Serikali legelege
Hayo aliyasema jana katika kikao cha pamoja kati ya Waziri huyo, Mkuu wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro, wakuu na wakurugenzi wa wilaya za Mbozi, ileje, Mbeya Vijijini na Rungwe, wafanyabiashara na wakulima wa zao la Kahawa.
Mdalavuma alisema kuwa, wakulima wilayani Mbozi wamekosa pembejeo msimu wa mwaka 2010-2011 na Serikali imekaa kimya jambo ambalo linamkumbusha kauli ya kwamba chama legelege huunda Serikali legelege.
‘’Ndugu waziri, umekuja hapa tukifikiri kuwa utazungumzia mustakabali wa uuzaji na ununuzi wa kahawa mbivu na upatikanaji wa pembejeo lakini tunashangaa hakuna majibu ya namna hiyo na hii nakumbuka kauli isemayo chama legelege huzaa serikali legelege’’alisema Mdalavuma huku wadau wakiguna na Prof, Maghembe akishika tama.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo ya Mbozi Erick Ambakisye alimtisha Waziri Maghembe kuwa endapo anguthubutu kutekeleza kanuni za wizara yake zinazoruhusu kununua kahawa mbivu wilayani humo ambayo wakulima wanaitaka wakati Halmashauri haihitaji atakuwa tayari kwenda kwa Rais Jakaya Kikwete ili waziri huyo achunguzwe.
Alisema kuwa anavyomfahamu Waziri huyo, anaamini kuwa wizara hiyo ya Kilimo chakula na Ushirika imemshinda na Jimbo lake pia limemshinda ndiyo maana wananchi wake hawana uchumi imara.
Kwa upande wao, wakulima zaidi ya 400 waliofika katika ukumbi wa Halmashauri hiyo ya Mbozi walimzuia Waziri Maghembe kuingia ukumbini hapo kwa madai kuwa waliokuwa ndani ya ukumbi walikuwa ni wafanyabiashara ya kahawa na wala si wakulima na ndiyo maana wao kama wakulima halisi walikataliwa na viongozi wa Halmashauri kuingia ukumbini.
Baada ya hali hiyo ya vuta nikuvute huku Afisa usalama wa wilaya hiyo akijaribu kuwasukuma wakulima hao ili Waziri aingie ndani na kuzungumza na ‘’wakulima maalum’’ waliokuwa wameandaliwa bila mafanikio huku asijue kuwa kulikuwa na wakubwa zake katika msafara huo, ndipo Mkuu wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro alitumia busara ya kuwataka wateue wawakilishi.
Wakulima wengi walisema kuwa taarifa aliyokuwa amepewa na viongozi wa Mkoa wa Mbeya iliyosema kuwa uuzaji wa kahawa mbivu inawaingizia hasara siyo ya kweli bali ililenga kuwanufaisha watu wachache wakiwemo vigogo wa Halmashauri zinazolima zao la kahawa mkoani Mbeya.
Mkulima Abrahamu Nzowa alisema kuwa, wakati Serikali na baadhi ya watendaji wa Halmashauri hizo zikiwa zinaipiga vita biashara hiyo hasa kampuni ya Lima Ltd inayonunua zao hilo kwa bei kubwa kuliko vikundi ambavyo viongozi hao wanamanufaa navyo, vikundi vinaendelea kuwanyonya wakulima hali ambayo wamesema inaleta kutoelewana miongoni mwao.
Aidha walisema kuwa kwasababu kahawa ni mali yao hawataacha kuuza kahawa hiyo mbichi kwa kampuni ambayo itakuwa inanunua kwa bei nzuri licha ya wilaya na mkoa kukataza kuuza kahawa hiyo.
Mkuu wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro alimweleza Waziri Maghembe kuwa msimamo wa Serikali ya mkoa wa Mbeya ni kwamba haitaki kusikia uuzaji na ununuzi wa kahawa mbivu mkoani hapa mpaka pale wakulima watakapoandikishwa na kutambulika.
‘’Sisi kama mkoa wa Mbeya tuliazimia katika vikao halali vya wadau wa mkoa na kwamba hatutaki biashara ya kahawa mbivu na kwasababu hapa hakuna wakulima walioandikishwa hawa wote si wakulima halali kisheria hivyo mpaka hapo tutakapokamilisha zoezi la kuwaadikisha ndipo tutakapochukua maoni yao’’ alisema Kandoro kwa kujichanganya.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya ukumbi huo baada ya kuogopa hoja za Wakuu wa wilaya, wenyeviti wa Halmashauri za wilaya hizo Nne huku wakurugenzi wote wakikataa kuzungumzia suala hilo lililochukuliwa kisiasa zaidi, Waziri Maghembe alisema kuwa hatengui kanuni zenye baraka za Wizara bali anachotaka bei ziboreshwe kwa wakulima.
‘’Mimi sijatengua kanuni za Wizara na Bodi ya kahawa juu ya ununuzi wa kahawa m,bivu bali nilichokuwa nasema ni kwamba lazima wilaya zisimamie sheria na kuhakikisha bei kwa wakulima wa kahawa zinasimamiwa na kulipwa vema lakini Serikali ya mkoa nyie mmeisikia haitaki biashara hiyo’’ alisema Waziri Maghembe.
Alisema licha ya hayo yote kila mfanyabiashara wa kahawa ama mnunuzi ni lazima awe na leseni ya biashara na haruhusiwi kununua kahawa kwa mkulima ambaye hajaandikishwa ili kudhibiti ukwepeji mapato ya Serikali kupitia biashara hiyo kama ilivyo sasa wilayani humo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa bodi ya kahawa nchini Adolph Kumbulu na mwanasheria wa Wizara ya kilimo walisema kuwa ununuzi wa kahawa mbivu umeongeza tija ya ubora wa kahawa Tanzania kutokana na ubora wa usindikaji wake tofauti na usindikaji unaofanywa na wakulima.
Hali hiyo ya mkanganyiko wa uuzaji na ununuzi wa kahawa mbivu (Cherry) imeleta utengano wa baadhi ya wakulima ambapo Serikali hasa vyombo vya usalama vinatakiwa kuliangalia kwa umakini kutokana na hali ilivyo ya wananchi kujengeana chuki ikiwa ni pamoja na kuijengea chuki Serikali.
Ubora wa kahawa upo katika ngazi nne ambazo ni P1,P2,P3 na Ponds, ambapo P1 inatoa madaraja Nane ambayo ni AA, A, B, PB, C, AF na F ambapo madaraja yanayouzwa nje ya nchi ni AA,A,B, PB na daraja C.
Habari na pastor kalulunga |