Jan 22, 2012
WATAWALA WAKUMBUSHWA KUMCHA MUNGU
Na, Gordon Kalulunga, Mbeya
VIONGOZI katika jamii wamekumbushwa kumtegemea Mungu katika maamuzi yao kwa ajili ya kutenda haki badala ya kutegemea ushauri mwingi kutoka kwa watu wao wa karibu.
Akihuburi leo katika ibada ya kwanza ya kanisala la Moravian Tanzania Jimbo la kusini Magharibi usharika wa Ruanda uliopo Jijini Mbeya, mhubiri Anna Nandile alisema kuna watawala na watu waliofanikiwa katika maisha kuwabeza wenzao huku wakisahau kuwa hao wanaowadharau wamechangia kuwafikisha hapo walipo.
Amesema watu wengi wamekuwa wakitegemea mamlaka waliyonayo na kusahau kuwa mamlaka zote hutoka kwa Mungu na kwamba mamlka yeyote inayotenda haki kwa kumtegemea Mungu hudumu.
Akinukuu maandiko kutoka katika Biblia takatifu 1Samwel mlango wa 24;1-12 yanayosema kuwa Daud alimtegemea Mungu alipokuwa akiwindwa na Sauli ambapo alipomuomba Mungu alimpa maarifa na akamlaza usingizi mzito Sauli na hatimaye Daud alikata nguo yake kisha akamwambia asisikilize maneno ya watu.
''Daud alishinda vita kwasababu alimtegemea Mungu hivyo wakristo tunatakiwa kumtegemea Mungu kwa kila jambo na kuacha kuwacheka wale ambao hawana chakula bali tuwasaidie kwasababu hata mali ulizonazo ni kwa neema na tukimtegemea yeye atupaye nguvu tutakuwa huru'' amesema Mhubiri huyo.
Mhubiri huyo amewakumbusha Wakristo waliohudhuria ibada hiyo kuhusu umuhimu wa kumtegemea Mungu kwa kila jambo na kwamba wanatakiwa kujiuliza kuwa watamrudishia nini Mungu kwa kuwalinda na kuwapa amani katika nchi huku akinukuu maandiko kutoka katika kitabu cha Zaburi 116;12-13
''Kila wakati tujikumbushe kuwa tutamrudishia nini Mungu kwa kusoma maandiko katika Zaburi 116;12-13 yanayosema Nimrudishie Bwana nini kwa ukarimu wake wote alionitendea.Nitakipokea kikombe cha wokovu na kulitangaza jina la Bwana'' amesema Nandile.
kutoka kalulunga Blog