Maandamano yaliyopangwa na wanahabari nchini kote kufanyika
kesho asubuhi huenda yasifanikiwe kwa mikoani baada ya taarifa za ndani
kuonyesha kupenyezwa taarifa kutoka ngazi za juu za jeshi la polisi zikitaka makamanda kuhakikisha hayafanyiki.
Taarifa kutoka mikoa mbalimbali zinaonyesha kuwa maandamano
hayo yamekosa vibali kutoka polisi ambapo mikoa ya Mbeya na Dodoma hadi saa nne usiku kulikuwa na taarifa
za kusitishwa kwa maandamano hayo.
Mkoani Mbeya wandishi
wa habari walikutana kwenye ofisi yao leo jioni ambapo katika hali ya
kushangaza watu wanaojiita wadau wa sekta ya habari walifika kuungana na
wandishi kupanga namna ya kuandamana ambapo miongoni mwake walishtukiwa kuwa ni
askari wa idara ya upelelezi ya jeshi la polisi.
Kutokana na hali hiyo wandishi waliwataka wadau hao wasubiri
mazungumzo ya wanahabari yamalizike ndipo waruhusiwe, lakini baadaye wanahabari
walikubaliana kutoshirikisha watu wengine kwenye maandamano hayo kwani yanahusu
wana taaluma wa habari tu.
Hatua hiyo pia imelenga kuepusha mwendelezo wa ajenda mpya
zinazozaliwa kutokana na tukio la kifo cha mwandishi wa habari Daud Mwangosi
ambapo wanasiasa na makundi mengine ya jamii yanaweza kutumia fulsa hiyo
kupenyeza ajenda zao.
Habari kutoka Dodoma zimesema, wandishi wa habari wa Mkoani
humo walipanga kutekeleza maandamano ya amani ya kimya kimya lakini polisi
imetoa taarifa kuwa haitaruhusu maandamano hayo kwani hayana kibali kutokana na
kuchelewa kuombwa kibali hicho ndani ya saa 12.
Vivyo hivyo Mbeya ambao pia waliomba kibali kwa kuchelewa
nao wamepewa taarifa za kuzuiwa maandamano hayo kwa siku ya kesho na kutakiwa
kujiandaa kwa keshokutwa jambo ambalo litaenda kinyume na tangazo la muungano
wa vyama vya wanahabari na vyombo vingine vilivyotangaza kuandamana kesho.