washiriki wakiandika jambo wakati wa majadiliano |
Na Danny Tweve
Mbozi
Imebainishwa kuwa tangu rais
asaini sheria namba 8 ya kuzuia na
kudhibiti maambukizi ya UKIMWI ya mwaka
2008, wilaya ya Mbozi haijaweza kumshitaki ama kumfikisha mtu mahakamani kwa
makosa yanayotokana na sheria hiyo licha ya kuripotiwa mara kwa mara kwa vitendo
vinavyoambatana na makosa ya sheria hiyo.
Kaimu
Mratibu wa Kudhibiti UKIMWI katika halmashauri ya wilaya ya Mbozi
SADNESS NGETWA amekiri kutofikishwa mahakamani kwa shtaka lolote
linalohusiana na sheria hiyo , licha ya kuwepo malalamiko kwenye jamii
ya vitendo vinavyoonyesha uvunjifu wa sheria hiyo
Wakizungumza kwenye mafunzo ya
Utekelezaji wa sheria hiyo wilayani Mbozi baadhi ya wadau kutoka mashirika yasiyo
ya kiserikali na viongozi wa dini na makundi ya watu wanaoishi na VVU wamesema
hali hiyo inachangiwa na mkanganyiko wa sheria yenyewe juu ya wakati upi mtu
atahesabika anaambukiza kwa makusudi ikiwa sheria yenyewe inazuia taarifa za
mtu mwenye VVU kutangazwa.
Mratibu wa asasi ya Maendeleo ya
jamii katika Mapambano dhidi ya UKIMWI wilayani Mbozi MSCHCD BI ZAINABU MAJUBWA
amesema pamoja na udhaifu wa sheria hiyo, bado kuna umuhimu mkubwa kwa TACAIDS
na wadau wa mapambano dhidi ya UKIMWI kuendelea kuisambaza sheria hiyo ili ijulikane kwa wananchi ambao ndiyo
walengwa wa sheria hiyo.
Wadau hao wamesema licha ya
kuwepo kwa vitendo vya uambukizaji wa makusudi vinavyofanywa na baadhi ya watu
wanaojitambua kuwa na maambukizi, bado kumekuwa na ugumu wa kuwashtaki wahusika
kwakuwa taarifa zao bado ni siri na kwamba sheria hiyo imekuwa mwiba kwa
wanandoa hasa wakati mjamzito anapoenda kliniki na kubainika kuwa na maambukizi ambapo imekuwa vigumu
kumshirikisha mwanandoa mwenzake kwa kuhofia kuvunja ndoa.
Bwana
Loyd Nzowa mmoja wa washiriki katika mafunzo hayo amesema, bado licha
ya kuonyesha kupinga unyanyapaa, sheria hiyo haijaweka misingi
itakayowezesha utekelezaji wake kuwa usiyo na vikwazo kwakuwa hata
upatikanaji wa huduma za tiba bado unachangamoto nyingi hii inatokana na
shughuli za UKIMWI kwa ujumla kutegemea misaada kutoka nje kwa
asilimia 90 kitu ambacho hakitoi uhakika wa huduma kwa WAVIU.
Mafunzo hayo yanaendeshwa na
asasi ya Mbozi Society katika kata
tano ikilenga kueneza sheria ya Kuzuia na kupambana na UKIMIWI ya mwaka
2008, kwa kujielekeza kwenye vifungu vya 7 na 8 vinavyohusiana na haki na wajibu kwa watu wanaoishi na VVU na nisehemu ya ufadhiri wa Foundation for
Civil Society.