Na francisgodwin.blogspot.com
USAILI wa wagombea wanaowania nafasi mbalimbali za uongozi katika chama cha soka mkoa wa Mbeya, (MREFA), jana uligubikwa na vituko vya aina yake, baada ya mmoja wa wagombea wa nafasi ya Uenyekiti, kumkataa mjumbe wa kamati ya uchaguzi kwa madai kuwa ana mgongano wa kimasilahi na mpinzani wake.
Mjumbe wa Kamati ya uchaguzi aliyekataliwa na kulazimika kutolewa ndani ya chumba cha usaili ili haki itendeke kwa mgombea ni Katibu, Prince Mwaihojo, ambaye anadaiwa kuwa ni Mkwe wa mgombea mmoja wa nafasi ya Uenyekiti John Mwamwaja.
Mtandao huu umeshuhudia katibu huyo wa Kamati ya uchaguzi, akitoka nje muda mfupi tu baada ya mmoja wa wagombea ya nafasi ya uenyekiti Elias Mwanjala, alipoitwa ndani ya chumba cha usaili.
Alisema kuwa haiwezekani mimi nihojiwe na mtu ambaye anamafungamano ya kidamu na mpinzani wangu, ndio maana nilipofika ndani ya chumba cha usaili nilitoa angalizo na nashukuru Mwenyekiti alielewa na kukubali kumtoa nje.
Kwa upande wake, Mwaihojo alipoulizwa juu ya sakata hilo la kukataliwa, alikiri kuwa lilitokea na si la ajabu katika mahala popote ambapo haki inaafutwa, hivyo kitendo hicho hakizuii mchakato wa kuwapata viongozi wa chama hicho.
Akitoa taarifa ya mchakato wa zoezi hilo baada ya kumalizika, Mwaihojo alisema zoezi hilo la usaili kwa limefanikiwa kwa asilimia 90 kwa kuwa wagombea 14 walifanyiwa usaili na kubakiza wagombea wanne tu ambao watamalizia hawakufanyiwa.
Kwa mujibu wa Mwaihojo, wagombea wanne ambao hawajafanyiwa usali ni Katibu anayemaliza muda wake Lawrence Mwakitalu, Andongwisye Panja, Thomas Kasombwe Sinkwembe ambao wote walitoa udhulu kutokana na kukabiliwa na shughuli mbalimbali ikiwemo kusimamia mitihani ya kidato cha nne inayoendelea hivi sasa.
Uchaguzi wa MREFA unatarajia kufanyika oktoba 27, jambo litakalowezesha kupatikana kwa uongozi mpya utakaohudumu kwa miaka mine kama katiba ya chama hicho inavyoeleza.
Amewataja watu waliojitokeza kuomba nafasi za uongozi kwa nafasi ya Mwenyekiti kuwa ni John Mwamwaja ambaye ni makamu Mwenyekiti wa uongozi unaomaliza muda wake, wakati wengine ni Majuto Mbuguyo aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji katika Halmashauri ya Wilaya ya Tanga, pamoja na Elias Mwanjal ambaye katika uchaguzi Mkuu uliopita aligombea ubunge katika jimbo la Kyela na kuangushwa vibaya na mbunge wa sasa Dk. Harrison Mwakyembe, ambaye pia ni Waziri wa Uchukuzi.
Kwa upande mweka Hazina ni Asajile Kavenga, Uswege Luhanga, wakati wajumbe wa kamati ya utendaji ni Lwitiko Mwamndela, Thomas Kasombwe, Boniface Sinkwembe.
Mwisho.