Adverts

Jan 16, 2013

WAKUU WA MIKOA WATOA MAONI YA KATIBA MPYA


Wakuu wa Mikoa wakijadiliana jambo nje  ya jengo la Tume ya Mabadiliko ya Katika jijini Dar es Salaam baada ya wakuu hao wa Mikoa kutoka kulia , Abbas Kandoro (Mbeya), Kanali Mstaafu Joseph Simbakalia (Mtwara),  Chiku Galawa (Tanga) na  Dk. Rehema Nchimbi (Dodoma)  kutoa maoni yao kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba jijini Januari 15, 2013.
*****
Wakuu wa Mikoa jana walipata fursa ya kutoa maoni yao mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba yanayoendelea kwa upande wa makundi maalumu.

Tofauti na makundi yaliyotangulia ambayo yalikuwa tayari kuongea na waandishi wa habari kuweka wazi kuhusu maoni waliyoyatoa, Wakuu wa Mikoa licha ya kukubali kuongea na waandishi wa habari lakini hawakuwa tayari kuweka wazi ni mambo gani waliyoyatolea maoni mbele ya Tume ya Katiba.

Akizungumza kwa niaba ya Wakuu wa Mikoa wenzake, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro aliwaambia waandishi wa habari kuwa walichopendekeza ni kuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba inapaswa kuyazingatia maoni yote ya Katiba ambayo Watanzania wameyatoa kwa njia mbalimbali.

Juhudi za waandishi wa habari za kumtaka mkuu wa mkoa huyo kueleza kama walipendekeza nini kuhusu nafasi yao ya Ukuu wa Mkoa ambayo wananchi wengi wamependekeza ifutwe, Kandoro aliwajibu kuwa hawakuja kufanya utetezi wa nafasi yao mbele ya Tume.