RISALA YA WANAWAKE
WILAYA YA MBOZI KWENYE USIKU WA MWANAMKE WILAYANI MBOZI
TAREHE 07/03/2013
Ndugu mgeni rasmi,
Wanawake
wilayani Mbozi tunayofuraha kubwa kuwa nawe katika hafla hii ya usiku wa
mwanamke wilayani Mbozi!
Ujio wako
unatupa faraja na kutambua kwamba serikali imeendelea kuthamini jitihada
mbalimbali zinazofanywa na mwanamke katika kujiletea maendeleo , pamoja na
kuchangia katika ustawi wa familia na jamii kwa ujumla
Mheshimiwa mgeni rasmi
Wanawake
wilayani MBOZI kwa kushirikiana na asasi za kijamii wameamua kubuni shughuli
mbalimbali zenye tija katika ukombozi wa mtoto wa kike ambazo zitakuwa
zikitekelezwa kila inapofanyika usiku wa mwanamke. Kwa mwaka 2013 wanawake
wamebuni shughuli ya kuchangisha fedha na bidhaa zingine kwaajili ya kufanikisha
ujenzi wa miundombinu rafiki yenye mtazamo wa kijinsia kwa watoto wa kike
katika shule za sekondari.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi
Kabla hatujafafanua utekelezaji wa mpango huu, tutoe angalau
kwa ufupi chimbuko la siku ya mwanamke duniani. Kimsingi chimbuko lake ni matokeo
ya maamuzi ya dhati ya wanawake kupinga kunyonywa na kudai hali bora katika
mazingira ya kufanyia kazi pamoja na ushiriki katika kupiga kura, Mwanamke
Clara Zeltein aliongoza wanawake katika
maandamano yaliyofanyika Agosti 26 hadi 27 ,1910 kupinga hali hiyo, na
ndipo march 8, 1957 katika mji wa New
York nchini Marekani ilikubalika kuwa kila mwaka maadhimisho ya siku ya
wanawake yatafanyika kila march 08 .
Hivyo hatua zinazoenda
kuchukuliwa na asasi ya Mbozi society
kwa ushirikiano na SWAAT pamoja na wadau wengine wa maendeleo wilayani
Mbozi ni mwendelezo wa harakati hizo.
Ndugu mgeni rasmi,
Kwa ujumla tunakusudia kujenga
tanurutaka kwaajiliya kuchomea taka
maalumu zinazotumiwa na wanafunzi wa kike na walimu wao wawapo katika mazingira
ya shule, Hatua hii ni muhimu katika kuondoa vikwazo vya kimazingira na
miundombinu vinavyowakabili wasichana wawapo kwenye masomo yao, hii inatokana
na kipindi cha mabadiliko ya makuzi kuhitaji mazingira na miundombinu
rafiki ili kuwawezesha kutoathiri
mwenendo mzima wakati wa kupata elimu.
Tunatambua kuwa wakati huu
serikali na wananchi kwa ujumla wanajiuliza
nini kilichopelekea matokeo mabaya ya kidato cha nne kwa mwaka 2012,
Sisi wanawake wa wilaya ya Mbozi tunatambua
changamoto ya miundombinu na hasa ile rafiki kwa wanafunzi wa kike ni miongoni
mwa mambo yaliyosababisha hali hiyo ya matokeo mabaya.
Ndugu mgeni rasmi
Chukulia shule ina wanafunzi wa
kike waliobarehe 500 ambao wanatumia matundu
manne ya vyoo vya shimo, hivi tunategemea katika kipindi chao cha
mzunguko wa kila mwezi ni kiasi gani cha taka kitakachoingizwa kwenye matundu
ya vyoo hivyo na vitadumu kwa kipindi gani, jambo hili limekuwa halitazamwi
sana katika mazingira yetu na hii inachangia pia kuwakatisha tamaa wanafunzi wa
kike kutokana na wakati mwingine kuadhibiwa wakati wakisubiliana kupata huduma
kwenye vyoo hivyo ambavyo kwa vyovyote vile haviwezi kudumu
Aidha watoto wakike walio katika
mabadiliko hayo hawana vyumba maalumu vya kubadilishia taka hizo na matokeo
yake wakati mwingine kulazimika kubaki na taka hizo mwilini kwa siku nzima hadi
muda mwa masomo kumalizika. Kutokana na changamoto hizo wanawake tumeliona
jambo hili kama moja ya changamoto za
elimu wilayani kwetu na tumeamua kuchua hatua kuanza kukusanya raslimali
kwaajili ya ujenzi huo.
Ndugu mgeni rasmi
Tunatarajia kuchangisha kiasi
cha shillingi million million Tano katika kipindi cha mwaka mzima kwaajili ya
kuwezesha kupatikana kwa miundombinu hiyo kwa baadhi ya shule tutakazozibaini
katika maeneo ya ndani ya wilaya ambapo gharama za tanuru taka moja litagharimu
shilingi 500,000 na vyumba vya kubadilishia nguo vitagharimu shilingi 800,000/=
Tunapenda tena kukushuru mgeni
rasmi kwa kuwa nasi usiku huu na sasa tunakukaribisha rasmi katika kuzindua uchangiaji huu
Ahsante
zainab Majubwa
Mratibu-Mbozi Society