Mmoja wa madiwani Mh Kalonge kutoka kata ya Igamba akiwasilisha taarifa ya utendaji na uwajibikaji kwa kata yake
Makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya Mbozi Mh Allan Mgula kushoto akiwa na kaimu Mkurugenzi Mtendaji Mbozi Bwana Zabron Lulandala kwenye kikao cha jana
Na Danny Tweve wa Indaba Africa
Mpango wa utoaji
chakula shuleni katika wilaya ya Mbozi , umeendelea kupanuka ingawa kwa meeneo
mengi umekuwa ukifanyika kwa vipindi maalumu imebainika.
Katika kikao cha
kuwasilisha taarifa za utendaji toka ngazi ya kata zilizowasilishwa na madiwani
ikiwa ni utaratibu wa halmashauri kupima
uwajibikaji wa waheshimiwa madiwani, baadhi ya kata zimefanikiwa kueneza
mpango huo kwenye vijiji vyote
Kulingana na taarifa
hizo kuna kata zenye akiba ya chakula cha miezi 8 kwaajili ya kuhudumia
wanafunzi kwenye shule za msingi na kata
zingine bado hazijatekeleza mpango huo kabisa.
Kulingana na taarifa
zilizowasilishwa kuna jumla ya gunia 206 za mahindi zilizochangwa na wananchi
kuwezesha utoaji wa huduma ya chakula mashuleni hasa kwenye ngazi ya elimu ya
msingi, hata hivyo kulingana na idadi ya wanafunzi uwiano wa chakula hicho kwa idadi ya wanafunzi waliopo wilayani
ni sawa na mlo wa siku mbili ambapo
wastani kwa siku mtoto anakula 0.11 kg za wanga.
Wilaya ya Mbozi ina
jumla ya wanafunzi 91,311 ambao kati yao 648 ni wa kutoka shule mbili binafsi
za msingi na wengine 90,663 ni kutoka shule 155 za serikali.
Hali hii inaonyesha
kurudi nyuma katika utoaji wa huduma ya chakula ikilinganishwa na robo ya mwaka
iliyopita ambapo taarifa zilizowasilishwa zilionyesha baadhi ya kata zilikuwa
zimefikia kuchangia gunia 70 za mahindi.
Kulingana na mwelekeo
wa uchangiaji, ni dhahiri katika kipindi hiki cha kuelekea masika, uchangiaji
utapungua badala ya kuongeza kwa kuwa kipindi cha mavuno (Julai hadi Septemba)
hapakuwekwa msukumo mkubwa kwa wananchi kuchangia chakula cha watoto mashuleni.
Kata ambazo zimeonekana
kufanya vizuri katika uchangiaji huo ni pamoja na Myovizi ambayo shule zake
zote saba zinatoa huduma ya chakula, Isandula ambayo shule tano kati ya nane
zinatoa chakula, Isansa ambayo shule 6 kati ya 16 zinatoa chakula, Ipunga shule
Mbili zinatoa chakula kati ya 5 na Mlowo shule 2.
Zingine ni Vwawa shule
2, Nyimbili shule mbili, Iyula shule 3 na Itaka shule 3. Kulingana a na takwimu
hizo kuna baadhi ya kata ambazo katika robo ya kumalizia mwaka wa fedha
2012-2013 ziliweza kutoa chakula lakini sasa zimerudi nyuma zikiwemo Nanyala,
Halungu, Igamba na Ruanda.
Ili kuongeza msukumo
kwenye usimamizi wa suala la chakula, vikao vya mabalaza ya madiwani vya kivyama ambavyo huketi kabla ya baraza la
madiwani la halmashauri, vinapaswa kujadili kwa upana suala hilo ili kuweka
msukumo wa makusudi katika kuwezesha utekelezaji wa mpango wa uchangiaji
chakula mashuleni uweze kutekelezwa.