Adverts

Nov 14, 2013

WAZIRI WA TAMISEMI ASEMA HAHAMISHI WATUMISHI MBOZI!

 Wajumbe wa kamati ya Ulinzi na usalama ya wilaya pamoja na watumishi wakifuatilia kikao hicho
 Baadhi ya watumishi na madiwani wakifuatilia kikao hicho
 Madiwani wakiwa na watumishi kwenye ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Mbozi
 Waziri Ghasia akizungumza na watumishi na madiwani 
Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI Mh Hawa Ghasia amesema hatahamisha watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbozi kwa sasa mpaka baada ya kutolewa kwa taarifa ya ukaguzi maalumu uliofanywa na Mkaguzi na mdhibiti wa hesabu za serikali.

Akijibu ombi la Mbunge wa Mbozi Mashariki Godfrey Zambi aliyemtaka waziri kufanya mabadiliko makubwa kwa wakuu wa idara wa Halmashauri hiyo kwa kile alichokiita kukosekana kwa uwajibikaji huku akimshambulia moja kwa moja Mkurugenzi wake anayestaafu Bwana Levision Chilewa kuwa yeye na wakuu wake wa idara hawakuwajibika na kuisababishia hasara halmashauri hiyo.

Ingawa Mkurugenzi Mtendaji aliyekuwa anasemwa kikaoni hapo hakuwepo, Mbunge huyo aliendelea kumtaja kuwa hata kama angekuwepo angempa hayo hayo kuwa alimjibu waziri wa nchi  ofisi ya waziri mkuu anayeshughulikia sera na uratibu Mh Lukuvi alipokuja wilayani Mbozi "majibu ya kitoto" kuhusiana na kwanini wilaya ya Mbozi ilipata hati ya mashaka mwaka 2011/2012.


Akizungumzia suala la kuwahamisha watumishi hao kama lilivyoombwa na mbunge Zambi, Waziri Ghasia alisema maamuzi ya watumishi walio chini ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya yapo chini ya Madiwani ambao Mbunge ni sehemu yake

Alisema yeye hata hamisha mtu wakati huu ambapo taarifa ya Ukaguzi maalumu kwa wilaya hiyo haujatolewa na akawataka watumie mamlaka yaliyo ndani yao katika kushughulikia masuala ya nidhamu na utendaji wa watumishi badala ya kusubiria TAMISEMI itekeleze hata kwenye maeneo ambayo wana uwezo nayo.

Waziri Ghasia amesema " ukiachilia Mkurugenzi mtendaji wengine wote ni mali ya halmashauri ya wilaya husika na hawa wanaokaimu nafasi mbalimbali wanapaswa kuthibitishwa na halmashauri za wilaya husika sana sana mnaweza kutuomba TAMISEMI tuwasaidie kuwafanyia upekuzi kabla hawajapandishwa vyeo lakini suala la mapendekezo linatoka kwenu.
 Kikao hicho pia kimezungumzia suala la mgawanyo wa mkoa wa Mbeya na kupata Mkoa wa Momba ambapo waziri Ghasia amesema, yeye pia alipewa maelekezo na Mh Waziri mkuu kufuatilia suala hilo na kwamba hatua ya kwanza amewaagiza wilaya ya Chunya kuomba kugawanywa na kuwa wilaya  Mbili kutokana na ukubwa wa eneo la wilaya hiyo.

hata hivyo amesema suala la kugawanya mkoa huo hataweza kulizungumzia kwakuwa linachangamoto nyingi na kwamba litazungumzwa na waheshimiwa wabunge na ikiwezekana maamuzi yataweza kutolewa baada ya mazungumzo hayo.

Kuhusiana na kuigawa wilaya ya Mbozi na kuwa na halmashauri nyingine, waziri Ghasia alisema wilaya inaweza kuanzisha mchakato huo na kuwasilisha mapendekezo hayoofisini kwake naye ataangalia vigezo katika kufikia maamuzi, tofauti na wilaya ya Chunya ambayo amesema kulingana na ukubwa wa eneo lake ambalo  linafikia kilometa za mraba 29,000 ambayo ni zaidi ya baadhi ya mikoa hapa nchini amelazimika kutoa maamuzi ya papo kwa papo ili waendelee na mchakato wa kugawa wilaya hiyo
 Katika hatua nyingine waziri huyo ametangaza hatua ya kurejesha kwenye ngazi za wilaya baadhi ya ajira za kada za chini baada ya apendekezo yaliyopelekwa kwa mheshimiwa Raisi kusainiwa katka mabadiliko ya utaratibu wa ajira za umma

Alisema kada za chini zitaanza kufanyiwa ajira kwenye wilaya husika lakini, wilaya zisubiri maelekezo ambayo yapo mbioni kutolewa hivi karibuni

Kuhusiana na marekebisho ya mishahara na upandishaji madaraja, waziri amesema serikali tangu iondoe madaraka ya kupandisha na kufanya marekebisho ya mishahara ya watumishi kwenye mfumo wa Lawson, Malalamiko ya muda mrefu ya kucheleweshewa malimbikizo na kutopandishwa madaraka kwa wakati yamemalizika.
Alisema kwa sasa ikitokea kucheleweshwa kwa mtu kupandishwa daraja ama kurekebishiwa mshahara basi ajue ni kutokana na kutowasilisha viambatanisho vyake vikiwemo vyeti . Aidha alisema malimbikizo ya mishahara ya watumishi yatakuwa yamelipwa yote ifikapo 2015.
MADIWANI WANAPEWA PASU NA WATUMISHI!
Katika hatua nyingine amewashambulia madiwani kuwa baadhi yao wamekuwa wakipewa fedha , kugawiwa kilo 3 za sukari na hata kupewa lift ili wapunguze makali ya kuwashambulia watumishi na badala yake wanakuwa wapole wakishapewa ofa hizo.
Akitolea mfano wa sehemu nyingine alisema kuna madiwani wakipewa lifti ya gari hadi kwao, kesho yake wakirejea kwenye vikao vya halmashauri wanakuwa watetezi wa watumishi waliowapa lifti!

Alisema hali hiyo inawadhalilisha madiwani na kuwaondolea uhalali wakusimamia masuala ya maendeleo.

Katika hatua nyingine Mh Waziri amesema kanuni mpya za madiwani zimeruhusu kamati zote za kudumu za halmashauri kushiriki kwenye ukaguzi wa miradi ya Maendeleo ambapo zitaanza kutekelezwa mara zitakapofikishwa wilayani.

Alisema sambamba na hilo Kamati ya fedha itaongezwa wajumbe na hasa kwa halmashauri zenye baraza kubwa la madiwani.