Adverts

Mar 18, 2014

KAMISHNA WA TACAIDS ASHTUSHWA NA ULEVI WA WANAOTUMIA ARV! ASEMA NI HATARI

Na Mwandishi wa Indaba Africa

Kamishna wa Tume ya kudhibiti UKIMWI TACAIDS Dk Violet Bakari  ametahadharisha uwezekano wa kutokea vifo zaidi na kutetereka kwa afya za watumiaji wa ARV ikiwa hawatapunguza  matumizi ya pombe.

Alisema ingawa kwa maeneo ya baridi baadhi ya watumiaji wa ARV wamekuwa wakisingizia hali ya baridi kuchangia unywaji wa pombe, amesema vivyo hivyo kwa maeneo ya joto pia imebainika watumiaji wa ARV wamekuwa watumiaji wa kileo hali ambayo amesema isitumike kama kisingizio cha kuhalalisha kuathiri afya zao.

 Akizungumza na vikundi na konga za watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI katika tarafa ya Igamba wilayani Mbozi, Kamishna huyo amesema, imebainika kuwa watu wanaotumia ARV wamekuwa watumiaji wakubwa wa pombe hasa vijiji, hali ambayo amesema kwa sehemu kubwa inachangiwa na kuimarika kwa afya zao hivyo kujiona wapo vizuri kama zamani.

Amesema uzoefu unaonyesha kadiri wanavyotumia dawa hizo na kuona afya zao zikiimarika, ndivyo wengi wao walivyojiingiza kwenye matumizi ya pombe hali ambayo amesema hawajatambua madhara yake kiafya na akawasihi afya zao zinazoimarika ziendane na uzalishaji kwaajili kujiweka vyema kiuchumi.

Alisema lengo la kuwawezesha kupata dawa hizo ni kuimarisha kinga zao na kuwawezesha kutumia fulsa ya afya bora katika kuendelea kutoa mchango wao kwa taifa na familia zao, tofauti na mtazamo wa wengi wao kuelekeza nguvu zao katika matumizi makubwa ya pombe

Kwa upande wake mkurugenzi wa tathmini na ufuatiliaji Dk Meshack Shimwela aliwataka wananchi kutochagua njia moja ya kukabiliana na maambukizi ya VVU na UKIMWI.

Akijibu maswali ya wananchi waliohoji muundo wa mipira ya kiume kutoziba sehemu kubwa ya maeneo ya siri na matokeo yake kusababisha maji maji kutoka kwa mtu mmoja kuhamia kwa mtu mwingine hivyo kuwepo hatari ya kuambukizana ikiwa mmoja atakuwa na majeraha katika mwili.

Dk Shimwela alisema, ni vyema wananchi wakatambua kuwa suala la matumizi ya kondomu za kiume linafanyika pale watumiaji wanapokubaliana na huku wakiwa timamu kiafya, lakini itakuwa maajabu kwa mtu kulazimisha kufanya mapenzi huku akitambua anavidonda mwilini hali ambayo hawezi kulifurahia tendo hilo.

“ni vyema tukatambua kuwa huduma tulizo nazo kila moja wapo hutumika kwa wakati, si vyema tukalazimisha kila jambo lifanyike na huduma moja” alifafanua Dk Shimwela

Katika ziara hiyo, tume imeridhishwa na utendaji wa afua za mapambano dhidi ya UKIMWI  ambapo watu wanaoishi na VVU wamekuwa na miradi ya kiuchumi hali ambayo inapunguza unyanyapaa na ubaguzi kwenye jamii wanazoishi. Takwimu za wilaya zinaonyesha kuna jumla ya wateja 11,500 walisajiliwa kutumia dawa za ARV katika wilaya ya Mbozi
MWISHO