Picha mbili toka Shule iliyotujenga kitabia ya Mzumbe, mwaka 1973-74.
Ya kwanza jioni moja kabla ya jua kutua mwaka 1974. Kilikuwa kikundi cha mabondia. Kawaida shule za kulala za sekondari huwa na uchaguzi ambao enzi hizo tuliziita kwa Kizungu “hobby” ina maana burudani baada ya kazi au masomo. Husaidia wewe kijana kusahau masomo magumu, kujifunza kitu chochote kinachokuongezea nidhamu na bidii ya elimu na kujiendeleza. Kitaifa miaka ya Sabini mwito uliopigiwa kelele na TANU chini ya Mwalimu Nyerere ulikuwa Elimu ya Ujamaa na Kujitegemea. ..
Toka kushoto aliyenyoosha ngumi ni kijana aliyekuja kuwa msomi, mwanafikra, mwandishi wa vitabu (mathalan, Makuadi wa Soko Huria, E & D Limited, 2002) na mhadhiri maarufu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Chachage S. Chachage.
Enzi hizo tulimwita Seti. Alikuwa mchangamfu na alipendwa hadi alipokuja kuwa mtaalamu maarufu wa mambo ya elimu jamii nchini. Leo anakumbukwa kwa jina la Profesa Chachage. Alifariki mwaka 2006.
Wa pili (aliyevaa kofia) na vile vile kifua wazi ni miye mwandishi.
Kati kati nyuma ni John Kihampa aliyekuwa kocha wetu. Sina hakika Kihampa yuko wapi siku hizi. Enzi hizo alikuwa mtulivu, hakusema maneno mengi na tulimheshimu maana aliyajua masumbwi fika. Nguzo kuu ya mchezo wa ngumi (tuseme michezo na riadha) ni ujenzi wa tabia ya kutokubali kushindwa. Kocha Kihampa (kama tulivyomwita) hakuwa na haja ya kujifaragua; alijiamini. Wa nne ni Hussein Laiser. Hussein ambaye kama marehem Chachage alikuwa akipatana na kila mtu pale shuleni alikuwa mzawa wa Arusha.
Baada ya kumaliza Mzumbe niliendelea kujuana na Hussein aliyeishi pia Dar es Salaam. Kila ukipita mitaani miaka hiyo ungekutana na Hussein na mara ya mwisho kumwona ilikuwa pale karibu na mnara wa askari kati kati ya jiji la Dar, mwaka 1984.
Nikiwa Brazil baadaye nilisikia Hussein aliuawa akiwa Italia mwaka 1994. Habari tata zilidai ama kapigwa risasi au katupwa ghorofani. Mambo ya aina hiyo si ajabu nchi ile isiyopenda sana watu weusi. Baada ya kumaliza kidato cha nne sijui kama alizaa mtoto au kuajiriwa; au iwapo aliendelea na mchezo wa masumbwi. Wa mwisho ni Msuya. Sikumbuki jina lake la mwanzo ila ninavyoelewa yeye na kocha Kihampa walikuwa marafiki na wakati tukifundishana mchezo huu wa jasho Msuya alikuwa keshapiga hatua kutuzidi.
Picha ya pili ni ya bendi yetu iliyoitwa The Earthquakes; ilipigwa majuma machache kabla ya machafuko yaliyotokea Mzumbe mwaka 1973.
Toka kushoto, waliosimama ni Haruna na Mecky. Aliyekaa akishika gitaa ni Mzawa wa Afrika Kusini, Thabiso Leshoai …Thabiso alikuwa mbele sana kimuziki. Miye nimekaa na gitaa chini na kulia kabisa Mike Sikawa. Yeye Mike na Tabs (tulivyomwita Leshoai) walikuwa viongozi wa bendi. Mike Sikawa aliyekuja kuwa mwandishi wa habari maarufu Daily News, BBC na This Day alifariki mwaka 2008.
Siku hizo bendi yake Mbaraka Mwinyishehe (Morogoro Jazz) ilikuwa ikija kutumbuiza pale shuleni. Na kila wakipumzika walitupa kile kilichoitwa “kijiko”…hapo ndipo tulipojifaragua na kuonyesha ufundi. Earthquakes ilivunjika baada ya maasi yaliyotokea mwaka 1973. Mike Sikawa na Thabiso Leshoai waliokuwa mstari wa mbele katika kuongoza maasi hawakurudi tena shuleni. Thabiso kama sijakosea alisharudi kwao Afrika Kusini. Sina hakika Haruna au Mecky wako wapi. Nilichobakia nacho hadi leo ni hiyo hiyo fani ya muziki…na kumbukumbu hizi…
" new post